NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI wa shehia ya Mtambwe kusini
wilaya ya Wete Pemba, wamesema kwa sasa huduma ya maji safi na salama katika
vijij vyao, inapatikana kwa urahisi, tofauti na hapo zamani.
Walisema,
kwa sasa wamekuwa na wakati mzuri wa kujipangia shughuli zao mbali mbali za
kimaisha, na wala upatikanaji wa huduma hiyo, sio changamoto inayowatengulia rataiba
zao za kimaisha.
Wakizungumza
na waandishi wa habari waliofika kijijini hapo, walisema kwa sasa huduma hiyo,
iko karibu vijiji vyote, tena bila ya mgao, jambo ambalo limechangia kufikia
malengo yao.
Walieleza
kuwa, upatikanaji wa huduma hiyo kwa miaka minne mfululizo sasa, unawapa
uhakika wa maisha yao, hasa kwa vile kila mmoja, anaendesha shughuli zake kwa
urahisi.
Salma Hamad
mkaazi wa kijiji cha Kivumoni, alisema kwa sasa huduma hiyo iko vyema na haina
shida kwao, ikilinganisha na miaka 20 iliyopita.
‘’Awali sisi
wananchi wa kikijiji cha Kivumoni shehia ya Mtambwe kusini, tukifuata maji masafa
ya mbali, ingawa kwa sasa tunaishukuru serikali,’’alieleza.
Nao
mwananchi Mafunda Abdalla Omar na Neema Abdalla Omar wakaazi wa kijiji cha
Mkanjuni shehiani humo, walisema kilichobakia kwao, ni kuyatunza miundombini ya
maji safi salama iliyopo.
Mwananchi
Jabiri Saleh Jabir (65) alisema awali aliwahi kutoka nywele kichwani, kutokana
na ubebaji wa maji wa masafa marefu, ingawa kwa sasa, huduma hiyo imewafuata
kwenye makaazi yao.
‘’Zamani
ilikuwa ni kazi kubwa kupata huduma ya maji safi na salama, inabidi uende
mabondeni kufuata huduma hiyo, tena maji hayakuwa safi na salama kama haya ya
sasa,’’anaelezea.
Sheha wa
shehia ya Mtambwe kusini Othman Ali Khamis, aliwataka wananchi, kuhakikisha
wanaendelea kuchangia huduma ya maji safi na salama, ili huduma hiyo iwe
endelevu.
Alieleza
kuwa, ndani ya shehia hiyo ipo mifereji 42 ya nje, ambayo wananchi wanaweza
kupata huduma saa 24, na wakati wowote.
‘’Wapo
wananchi walioamua kuvuta huduma hiyo ndani, lakini kwa wasiokuwa na uwezo,
serikali imeamua kuweka mifereji nje, ili iwarahisishie kupata huduma
hiyo,’’alieleza.
Sheha huyo
alisema, kwa sasa huduma hiyo, inapatikana saa 24, na ikitokezea kukosekana,
iwe hakuna hduma ya umeme, au kuharibika mashine.
Aidha sheha
huyo amewakumbusha wananchi kuendelea kutunza mazingira, na hasa kuacha ukataji
wa miti ovyo, karibu na vyanzio vya maji.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji Zanzibar ‘ZAWA’
Ofisi ya Pemba, Suleiman Anas Massoud, alisema huduma kwenye shehia hiyo
imeimarika, baada ya kushirikiana kwa karibu na tasisi ya Zanzibar Milele
Foundention na mfuko wa Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe.
Alisema,
kisima kilichopo Daya Mtambwe, kinauwezo wa kuzalisha kati ya lita 55,000 hadi
60,000 kwa saa, ambapo yanakwenda samba mba mahitaji na matumizi.
Hata hivyo
amewakumbusha wananchi wa shehia hiyo, kuendelea kuchangia huduma ya maji safi
na salama, ili iwe rahisi inapotokezea hitilafu.
‘’shehia za Mtambwe
kusini na Kaskazini kuna mradi maalum na sasa wanakusanya takwimu ili
kuimarishiwa hudum na hasa kwa vile sasa idadi ya watu imeongezeka,’’aliongeza.
Wananchi 4,733
wakiwemo wanawake 2,323 na wanaume 4,210 wa vijiji vya Makoongweni, Kivumoni,
Mkanjuni, Kinazini, Kokota shehia ya Mtambwe kusini wilaya ya Wete,
wanavitegemea visima viwili vilivyopo Daya, Mkanjuni na kile cha Kinazini
kikiwa kimeharibika mashine yake.
Mwisho
Comments
Post a Comment