NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANASIASA Kisiwani Pemba, wamesema
kazi iliyofanywa na PEGAO, ZAFELA na TAMWA ya kuibua kero za wananchi na kuzifikisha
eneo husika, na kisha kuchukuliwa hatua, hakuna mwanasiasa yeyote engeweza kuifanya
kazi hiyo.
Walisema,
taasisi hizo zilifika katika wilaya zote nne za Pemba, na kukutana wananchi,
wakiwemo wanawake na kuzisikiliza changamoto zao, na kisha kuzifika tasisi
husika kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.
Wakizungumza
kwenye mkutano maalum wa kuwasilisha utendaji kazi kwa wahamasishaji jamii hao,
kupitia mradi wa kuiwezesha jamii kudai haki zao za uongozi, siasa na
demokrasia, na kufanyika ofisi ya KUKHAWA, walisema kazi iliyofanywa ni kubwa.
Mwenyekiti
wa Chama cha wakulima cha AAFP, taifa Said Soud Said, alisema kazi hiyo anaona
kusingekuwa na mwanasiasa yeyote, engeweza kuwafikia wananchi na kuchukua kero
kwa lengo la kuzipatia sulhu.
Alieleza kuwa,
kazi hiyo inafaa kuthaminiwa na kuungwa mkono na serikali kuu, kwa kuziwezesha
tasisi hizo tatu, ili kuendelea kuisaidia serikali.
‘’Kama
ingekuwa taasisi zote hapa Zanzibar, zinafanyakazi kubwa kama iliyofanywa na
PEGAO, ZAFELA na TAMWA- Zanzibar wananchi wengekuwa wanaishi bila ya changamoto
kubwa,’’alisema.
Nae mwanasiasa
kutoka CHADEMA mkoa wa kusini Pemba, Time Ali Mohamed, alisema kwa kiasi
kikubwa taasisi hizo zimesaidia sana, na kusababisha wananchi kupatiwa huduma
za kijamii.
Alieleza
kuwa, hata wanawake wamekuwa wahanga wakubwa wa kukosa nyaraka za lazima, mfano
vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho, kufuata hudua za afya masafa marefu, lakini
sasa juhudi za ZAFELA, PEGAO na TAMWA-Zanzibar zimesaidia,’’alifafanua.
Nae mwanachama wa CUF Mohamed Haji Kombo na mwenzake wa ACT-Wazalendo Juma Khamis Ali, walizitaka tasisi hizo, kuendelea kuwaelimisha wanawake juu ya haki zao za uongozi, siasa na demokrasia.
Mwakilishi wa
Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba Dk. Massoud Suleiman Abdalla, alisema bado
suala la uzalendo limekuwa changamoto kwa wananchi, na kupelekea huduma nyingi
kukwama.
‘’Inawezekana
dawa zipo hospitali, au wakati mwengine mfanyakazi anakabidhiwa vitendea kazi,
lakini kwa kule kukosa uzalendo, jamii hukosa huduma hiyo,’’alieleza.
Nae
mwakilishi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Harith Bakar Waziri,
alisema changamoto ya makaazi kwa wanafunzi, uhaba wa waalimu karibu litatuka historia
jambo hilo.
‘’Awamu hiyo
ya serikali ya nane, imedhamiria kuajiri waalimu karibu 1000 kwa Pemba, ujenzi
ya vyumba vya madarasa 1000, ili kuhakikisha hakuna, skuli yenye mikondo miwili
ya wanafunzi,’’alieleza.
Akifungua
mkutano huo, Mratibu wa TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hya Mussa Said,
alisema wamegundua kuwa, katiba za vyama, sheria za ajira zimekuwa changamoto
kwa wanawake wanaogombea nafasi za kisiasa.
Alieleza kuwa,
suala la kurejeshwa ama kutorejeshwa tena kazini baada ya kukosa nafasi kwenye
uchaguzi mkuu, limekuwa likiwatia woga wanawake.
Mratibu wa
mradi wa kuwawezesha wanawake kudai haki zao za uongozi, siasa na demokrasia ‘SWIL’
kutoka PEGAO Dina Juma, alisema kama huduma za kijamii haziko sawa, mwanamke
hafikirii kugombea.
‘’Mwanamke
ni mtu anayeishi kwenye dimbwi la changamoto za kifamilia, sasa kama na huduma
za kijamii hazijaimarishwa, wazo la kudai haki yake ya uongozi, huwa mbali naye,’’alieleza.
Akifunga mkutano huo, Mkurugenzi wa PEGAO
Hafidh Abdi Said alisema, bado katiba za vyama vya siasa na viongozi wakuu wa
vyama, hawajaona umuhimu wa wanawake kushika uongozi.
‘’Wanawake
hata kwa takwimu ya sensa ni wengi kuliko wanaume, lakini kwanini kwenye nafasi
za uongozi hawaonekani, bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa,’’alieleza.
Tayari wahamasishaji
jamii kisiwani Pemba ambao wanatekeleza mradi wa ‘SWIL’ unaoendeshwa na PEGAO,
ZAFELA na TAMWA-Zanzibar wameshazifikia shehia 56, kwa wastani wa wananchi 3,000
kuwapa elimu ya umuhimu wa wanawake kuwa viongozi.
Mwisho
Comments
Post a Comment