NA ZUHURA
JUMA, PEMBA@@@@
VIONGOZI, wanaharakati na wataalamu wa masuala ya
saikolojia wameonya kuhusu athari za muda mrefu zitakazotokea kisiwani Pemba na
Zanzibar kwa ujumla, endapo vitendo vya ubakaji vitaachwa bila kuchukuliwa
hatua.
Katika miaka ya karibuni, kumekuwa
na matukio mengi ya mabinti ambao hawajafikia umri wa kuruhusiwa kushiriki
ngono kubakwa, lakini wahusika kuachiwa baada ya kesi kuondolewa mahakamani.
Katika mahojiano
yaliyofanywa kati ya mwandishi wetu na makundi tofauti, ilielezwa kwamba hali
hii ya sasa kama itaendelea, kuna hatari ya jamii ya Pemba kupata athari za
muda mrefu.
Moja iliyotajwa ni wingi
wa watoto wasio na familia, waathiri wa ubakaji wenye msongo wa mawazo na
kujengeka kwa utamaduni wa watu kutotii sheria.
Mkaazi wa Shehia ya Minungwini, Maulid Saleh Hamad, anasema
hofu yake kubwa, ni kwamba kuna athari nyingi zitajitokeza ikiwa ni pamoja na
wabakaji kuzidi kusambaa kwenye mitaa yao na kupata nguvu zaidi ya kudhalilisha
watoto.
Bakari Suleiman Juma wa Shehia ya Kambini anasema wana hofu
kubwa kwamba vitendo hivyo vitakuwa endelevu na pia watoto wataendelea
kufanyiwa ubakaji kila siku kwa vile wale wanaomdhalilisha hawapati hukumu
yeyote.
“Mtoto anapofanyiwa udhalilishaji ni vigumu kutimiza malengo
yake aliyoyakusudia kwani walio wengi hawarudi tena skuli kusoma”, anaeleza.
Mkaazi mwingine wa Shehia ya Mitondooni Kambini, Riziki
Abdallah anaeleza kuwa, mtoto anayekataa kutoa ushahidi ataendelea
kudhalilishwa na watoto wengine watakuwa wanashawishiana kuendelea na vitendo
hivyo.
“Aghalabu wanapokwenda hurubuniwa kwa pesa, hivyo anapoona
nikienda kwa fulani ananipa pesa, anamwambia na mwenzake na mwisho wa siku ni
kuambukizana mchezo mchafu”, anasema.
Mwanaharakati Siti Faki Ali anasema, watoto wataathirika
kisaikolojia na kimaumbile kwa sababu kuna kesi nyingi ambazo daktari huthibitisha
tayari ameshaharibika fuko la uzazi au haja ndogo na kuharibika sehemu za siri.
“Kwa hali hiyo, inawezekana huko mbele kukosa kizazi kwa sababu
tayari ameshakuwa mbovu na hivyo taifa kukosa nguvu kazi”, anaeleza
mwanaharakati huyo.
Khadija Hassan Ali mkaazi wa Piki anaeleza kuwa athari ni
kubwa kwani, waathirika wa vitendo vya ubakaji huathirika kiakili, wengine hukosa
kizazi na pia huwa watu wenye kuona aibu bila sababu katika maisha yao yote.
Hakimu wa Mahakama Maalumu ya kushughulikia kesi za Udhalilishaji
Mkoa iliyopo Wete, Ali Abdulrahman Ali, anataja athari kubwa ya kuachia
washitakiwa ni kuwa haki inashindwa kupatikana.
“Kesi za ubakaji zilizofikishwa mahakamani mwaka 2020 ni tisa (9),
kati ya hizo watoto wenye miaka 15-17 ni kesi tatu ingawa moja tu ndio
iliyopata hatia na mbili ziliondoshwa”, anafafanua.
Afisa Ustawi wa Jamii Pemba, Omar Mohamed, anaeleza kuwa athari
kubwa inayoweza kutokea ni kuongezeka kwa vitendo hivyo vya ubakaji hasa pale
wahalifu watakapoona hatua hazichukuliwi kwa vitendo vyao.
‘’Vilevile watoto wataendelea kudhalilishwa na hatimaye
kuambukizwa maradhi mbali mbali, ikiwemo ukimwi na mwisho wa siku watashindwa
kutimiza ndoto zao za kimaisha walizokuwa nazo kwa muda mrefu,’’anaeleza.
Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA)
Pemba, Fat-hiya Mussa Said, anasema athari ni kutokuwepo kwa kesi itakayopata
hatia kwa sababu kesi yeyote haiwezi kupata hukumu bila ya kutolewa ushahidi
mahakamani.
‘’Tena unatakiwa ushahidi usio na shaka, hivyo ikiwa ushahidi
hakuna, kila siku matukio yatazidi kwa sababu washtakiwa itakuwa hawapati
kutiwa hatiani’’, anaeleza.
Baba mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe mkaazi wa Kiuongoni anakumbuka
kuwa, kuna kesi ilitokea kijijini kwao hivi karibuni, ambapo familia zote mbili
walikubaliana mtoto aharibu ushahidi, ili wazazi wake wapewe shilingi milioni
mbili.
“Na kweli mtoto huyo mwenye miaka 15 alibadilisha ushahidi na ilikuwa
kila wanapoitwa hawataki kwenda mahakamani, hatimae kesi ilifungwa, kilichowafanya
wajutie sasa, baada ya mtuhumiwa kutoka mpaka leo hawajapewa pesa”, anasimulia.
Anasema kwamba, sasa familia hiyo imebaki kulalamika na kusema
wataenda tena kuifungua kesi hiyo, jambo ambalo linamshangaza sana kwani chungu
ni moto wa mwanzo wahenga walisema.
“Hiyo ndio athari kwa sababu mtoto wao ameshabakwa, baadaye
wakamshawishi asiseme ukweli, hivyo sasa yupo ameshakosa haki yake huku
mwanamme akidunda mitaani”, anaelezea.
Sheikh Mussa Saleh Ali anasema, athari zinazoweza kutokea iwapo
watoto hao wataendelea kukataa kutoa ushahidi, ni kwamba aliyefanya kitendo
hatopata kuhukumiwa, kwani ushahidi itakuwa umepotea.
Taarifa za kimahakama
zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2020 hadi
2021, jumla ya kesi zinazohusu ubakaji wa mabinti wadogo zilikuwa ni 49 huku za
watoto kati ya umri wa miaka 15-17 zikiwa 19. Katika kesi hizo, kesi ambazo
wahusika wamefungwa ni nne tu huku mbili wahusika wakitozwa faini na nyingine
13 zikiwa zimeondolewa mahakamani.
Pia, takwimu hizo zinaonyesha kwamba kwa mwaka 2021, kesi za
kubaka zilizofikishwa mahakamani ni 25, huku zinazohusu watoto wenye miaka
15-17 ni 16, ambapo kesi 11 zimeondolewa, kesi tatu washtakiwa wamefungwa na
kesi mbili washtakiwa wametozwa faini kutokana na kuwa wapo chini ya miaka 18.
Uchunguzi wa mwandishi kuhusu suala hili umebaini kwamba moja wapo
ya sababu zinazosababisha kesi za ubakaji kuishia namna hii ni ukweli kwamba
wahusika huwa wanajuana kwa ama kuwa jirani, familia moja au ndugu wa karibu.
Kumekuwa na kesi nyingi ambazo hufutwa kituo cha Polisi na
mahakamani kwa kukosa ushahidi, hasa zile za watoto wenye umri kuanzia miaka 15
hadi 17, jambo ambalo linaleta athari mbalimbali kwa familia, jamii, taifa na mtoto
mwenyewe.
Pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuweka
mikakati itakayosaidia kesi hizo kusikilizwa kwa haraka na kupatiwa hukumu kwa
lengo la kutokomeza vitendo hivyo, lakini bado kesi za watoto wenye umri huo
zinaendelea kufutwa.
Mwisho
Comments
Post a Comment