NA HAJI NASSOR, PEMBA
WANANCHI kisiwani Pemba, wametakiwa
kuitumia Kamati ya maadili ya watumishi wa mahakama, kwa kufikisha malalamiko
yao pale wanapoona wamekwazwa kwa njia moja ama nyingine, na mtumishi yeyote wa
mahakama.
Kauli hiyo
imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Jaji wa mahakama kuu Zanzibar, Rabia
Hussein Mohamed, wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, juu ya uwepo wa
kamati hiyo.
Alisema kwa
wananchi waliopo Pemba, wanaweza kufikisha malalamiko yao kwa njia ya maandishi
kwenye jengo la mahakama kuu Chake chake, na kisha kamati hiyo kuyasikiliza kwa
kina.
Alisema,
kamati hiyo baada ya kusikiliza hupeleka mapendekezo kwa Jaji mkuu kwa ajili ya
hatua nyingine za kinidhamu, kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa
umma.
Jaji Rabia
alieleza kuwa, kamati hiyo ambayo inaundwa na wajumbe watano, inalengo la kuona
watumishi wa mahakama wanafanyakazi zao kama sheria na kanuni za utumishi zinavyoelekeza.
Aidh
Mwenyekiti alisisitiza kuwa, huu sio wakati tena kwa wananchi kulalamika chini
ya meza, pale wanapoona wamefanyiwa ukiukwaji wa kimaadili ya kazi.
“Kamati
yangu, moja ya jukumu lake kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa mahakama ya
mwaka 2018, ni kuchunguuza na kutoa mapendekezo kwa Jaji mkuu na tume ya
utumishi wa mahakama, kwa kuchukua hatua,’’alieleza.
Kuhusu uwepo
wa kamati hiyo, alisema ni kuweka kwa ufanisi nzuri kwa watendaji wa mahakama,
ili kuwapa nafasi wananchi kuendelea kukitumia chombo hicho, kwa uwazi.
Katibu wa
kamati hiyo, Hussein Makame Hussein alisema, baada ya kupokea malalamiko hayo
na kuyachunguuza, huwafikisha mapendekezo kwa ngazi husika.
‘Sisi kamati
yetu haina uwezo kisheria kutoa adhabu, bali ngazi ya Jaji mkuu na mamlaka ya kinidhamu
ndio wanaoweza kumuwajibisha mtumishi husika,’’alieleza.
Hata hivyo
Katibu huyo alisema, mwananchi anaweza kumlalamikia Jaji mkuu, Jaji wa mahakama
kuu, mtendaji mkuu, kadhi au naibu kadhi mkuu, ingawa sio kupitia kamati hiyo.
“Kamati hii
imefungwa miguu na mikono kupokea malalamiko ya viongozi hao, maana wanangazi
nyingine kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984,’’alieleza.
Nao wajumbe
wa kamati hiyo Mohamed Bakar Shamata na kadhi wa mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe sheikh Idi Said Khamis,
walisema ni fursa kwa wananchi, kuitumia kamati hiyo.
Walisema, wananchi
wasiwe na sababu ya kulalamika pembeni, bali sasa serikali, imewaletea chombo
huru kwa ajili ya kupokea malalamiko au kero wanazofanyiwa na watumishi wa
Mahkama.
Kadhi huyo
alieleza kuwa, wananchi hata wanapoona kuna tuhuma za rushwa au uvunji mwengine
wa maadili, wasisite kufikisha malalamiko yao mahakama kuu Chake chake wa Pemba
na Vuga kwa Unguja.
Baadhi ya
wananchi kisiwani Pemba, wamesema kamati hiyo ni nzuri, ikiwa itakuwa huru na
kufanyakazi zake bila ya kuingiliwa kama ilivyo kwa vitengo vyengine.
Hadia Khamis
Chumu alisema, wataitumia kamati hiyo, hasa kwa vile wapo baadhi ya watendaji
wamekuwa wakishindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
Jokha Mnubi
Iddi alisema, anachoomba kwa wajumbe wa kamati hiyo, kuendelea kutekeleza
wajibu wao kama sheria inavyoongoza.
Kamati hiyo yenye
wajumbe watano wakiwemo wanawake wawili, ambayo imeasisiwa April 15 mwaka jana,
wajumbe watadumu kwa miaka mitatu, na tayari imeshapokea malalamiko manne,
kutoka kwa wananchi wakiwalalamikia watumishi wa mahkama.
Miongoni mwa
majukumu yake ni kushughulikia kesi, tuhuma za rushwa, tabia isiyoendana na
kanuni na maadili ya mahkama au kushindwa kutekeleza wajibu wake.
Mwisho
Comments
Post a Comment