NA HAJI NASSOR, PEMBA
WATAALAMU wa sheria Zanzibar,
wameitaka Idara ya Katiba na Msaada wa sheria Zanzibar, kuongeza jitihada za
elimu ili kusaidia kubadili mawazo, mitazamo na uwelewa wa watu maskini, ili
kuongeza matumizi ya huduma za msaada wa kisheria.
Walisema, Idara inapaswa kuweka kipaumbele cha
pekee cha kutoa mafunzo hayo, ili kuona walengwa wa mfumo wa kutoa elimu,
ushauri na msaada wa kisheria ambao ni watu maskini wanafaidika nao.
Kwa mujibu
wa tafsiri ya ripoti ya tathmini ya awali ya hali halisi ya msaada wa kisheria
Zanzibar ya mwaka 2020, iliyotolewa na wizara ya Katiba na sheria, walisema
azma ya uwepo wa msaada wa kisheria ni kwa watu wasio na uwezo.
Wataalamu
hao kwenye ripoti hiyo walisema, suala la utoaji wa msaada wa kisheria
linazingatiwa kuwa ni miongoni mwa viashiria vya msingi ya upatikanaji haki.
Walieleza
kuwa, taifa lolote lile duniani haliwezi kufurahia uwepo wa baadhi ya haki za
binadamu bila ya kunawiri mfumo wa utoaji wa msaada wa kisheria.
Aliyekuwa
Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, kwenye ripoti hiyo alisema wasaidizi
wa sheria na watoa msaada wa sheria wanafanyakazi kubwa ya kuisaidia jamii
kuwapa ufahamu wa sheria.
Wakili wa
serikali Mwandamizi Afisi ya Mkurugenzi wa Mashataka Ali Rajab, alisema bado
watoa msaada wa kisheria hawajawafikia ipasavyo watu katika maeneo hasa ya
vijijini, ambao wengi wao hawana uwezo wa kulipia gharama za mawakili.
“Jengine
ambalo ni kasoro inaonekana watoa msaada wa kisheria wengi wao ni waajiriwa wa
serikalini au sekta binafsi, hivyo hawana muda mwafaka wa kutoa
huduma,’’alieleza.
Rais mstaafu
wa chama cha mawakili Zanzibar Omar Said Shaaban, alisema sasa mawakili hawana
tena mtazamo mbaya kwa watoa msaada wa kisheria, kama ilivyokuwa hapo mwanzo.
Wakili wa
mahakama kuu Pemba Khalfan Amour Mohamed, alisema wananchi walio wengi waliopo
Pemba, hawajafurahia utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kutokana na
jiografia ya kisiwa chenyewe.
Aidha
Mkurugenzi wa Jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar ‘ZAFELA’ Jamila Mahamoud,
alisema wasaidizi wa sheria hawana muda wa kutosha wa kuwahudumia watu katika
maeneo yao.
“ZAFELA
imegundua kuwa, wasaidi wa sheria waliopata mafunzo na ZLSC hawakai katika
maeneo ambayo walipojisajili wakati wanaomba mafunzo hayo,’’alifafanua.
Katika
ripoti hiyo, wataalamu hao wa sheria walipendekeza kuwa, wakati umefika sasa
kuongeza ufahamu wa watoaji wa masaada wa kisheria ili kutambuliwa rasmi.
Hata hivyo
walipendekeza kuwa, ni vyema watoa msaada wa kisheria kushirikiana kwa karibu
na mawakili katika ofisi zao, ili kutoa huduma za kujitolea kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza
hivi karibuni Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na msaada wa kisheria Zanzibar,
Hanifa Ramadhn Said, alisema licha ya uchanga wa idara, wameshafanya makubwa,
ikiwa ni pamoja na elimu kwa jamii.
“Hivi sasa karibu
kila shehia tumeshaifikia, nab ado tunaendelea kukutana na jamii, ili kuwapa
elimu na ushauri wa kisheria tena bila ya malipo,’’alieleza.
Ripoti hiyo
ya tathmini ya awali ya hali halisi ya msaada wa kisheria Zanzibar, inaangalia
taarifa za awali kuhusiana na historia, hadhi, asili ya shughuli za masaada wa
kisheria hapa Zanzibar.
Ambapo
ripoti hiyo, itasaidia kubainisha mambo yatakayoimarisha huduma za utoaji
msaada wa kisheria pamoja na kupendekeza mfumo mzuri, utakaopelekea kupatika
kwa urahisi kwa watu wote.
Mwisho
Comments
Post a Comment