NA ZUHURA JUMA,
PEMBA@@@@
'DUNIA
imebadilika...kwani ya jana sio ya leo'
Katika miaka ya sasa, wanaonekana wanawake wengi wanaojihusisha
na masuala ya uongozi, katika sekta mbali mbali.
Ikiwa ni katika vikundi vya ushirika, uongozi kwenye jamii,
shehia, majimbo na hata kwenye taasisi za umma na binafsi.
Hii ni kutokana na elimu inayotolewa kupitia vyombo vya habari
na kwenye jamii, kuhusu ushirikishwaji wa wanawake kwenye masuala ya uongozi.
Na ndio maana hata mfumo wa elimu uliopo sasa, unatambua kwamba
watoto wa kike wanapaswa kujengwa mapema kiongozi, ili kila hatua anayopitia
aweze kujiamini na kuwa jasiri.
Tangu wakiwa skuli, wanafunzi wanajengewa uwezo wa kuwa viongozi
bora na huwashirikisha wakike na kiume bila ubaguzi, lengo ni kutengeneza taifa
lenye viongozi bora wa baadae.
Mwanafunzi Aisha Khamis Ayoub ambae ni Waziri wa Fedha skuli ya sekondari
ya Idrissa Abdulwakil Kizimbani Wete anasema, mwanzo alikuwa anaogopa kugombea
nafasi za uongozi, kwani alikuwa hawezi kuzungumza.
Baadae alijiamulia mwenyewe na kuona kwamba ni bora agombee
nafasi hiyo, ambapo sasa anajiamini na anatekeleza majukumu yake vizuri
aliyopangiwa.
Aisha malengo yake ni kugombea ubunge atakapomaliza masomo, ili
aweze kutetea wananchi hasa wanawake kwenye mambo yanayowahusu, kwa ajili ya
kujenga jamii iliyobora.
"Kwenye serikali ya wanafunzi tuna jukumu la kusimamia
wanafunzi wote, tunawasaidia waalimu wetu majukumu, ingawa wanafunzi ni wakaidi
lakini tunasuluhisha wenyewe linapotokezea tatizo," anaeleza.
Mwanafunzi Salum Khamis Salim wa skuli hiyo, anasema kitu
chochote unatotaka kukianza unatakiwa uombe Mungu na baada ya kukipata basi
ukifanyie kazi ipasavyo huku ukiwa na nidhamu.
Anasema, wao wamejengeka kinidhamu na wanafunzi wanaowaongoza
wanawajengea mazingira bora ya kuwa na nidhamu, ambapo hukaa nao na
kuwaelimisha.
"Serikali ya wanafunzi inawasaidia sana waalimu kwenye
paredi, usafi na kusimamia wanafunzi wenzao, ili walimu wafanye shughuli nyingine,
ingawa changamoto zinazotukabili ni uhaba wa vifaa vya kufanyia usafi,’’anafafanua.
Rais wa skuli hiyo Juma Said Mohamed anasema, wanawake wanapewa
fursa za kugombea, ingawa hawataki kwani wanaogopa.
"Nawashawishi sana kwa sababu utendaji wao ni mzuri na wanawajibika
ipasavyo, hivyo nimekuwa nikiwashari mpaka wengine wanakubali," anasema.
Anasema serikali yao inaviongozi 25 wanawake watano na wanaume
20, ingawa wanawake wanahitaji kuongezeka, ili kazi niende vizuri.
Mwanafunzi wa skuli ya sekondari Limbani Shuwekha Khamis Mohamed
anaeleza kuwa, wanawake wanapokuwa viongozi wanasaidia, upatikanaji wa haki kwa
wote na kupata kujiamini.
Ingawa nafasi yake ni ya kuteuliwa, lakini anafanya kazi kwa ushirikiano
mzuri na waalimu pamoja na wanafunzi, huku akiendelea kujifunza mambo ya
uongozi.
"Nimepata mafanikio makubwa, kwani wanafunzi wananiheshimu,
nimejenga upendo na waalimu pamoja na wanafunzi, sasa najiamini kwenye kazi
zangu,"anasema.
Rais wa skuli hiyo Ahmed Hamad Mabwana anaeleza, ipo haja kwa
wanawake kujengewa uwezo mapema, kuhusu uongozi ili kuwe na hali ya usawa.
"Ni vyema washirikishwe ili wasidharauliwe kwani kwa sasa
uwezo wao sio mkubwa, ingawa kupitia Serikali ya wanafunzi naamini watakuwa vizuri,"
anasema.
Changamoto inayowakabili ni tabia ya wanafunzi kuwa wajeuri na kiburi,
jambo ambalo linarudisha nyuma juhudi zao, ingawa ndizo zinazowajenga ujasiri
na kujua aina ya watu wanaowaongoza.
Wamekuwa wakipewa elimu mara kwa mara, ambayo yanawajenga kuwa
viongozi bora wa sasa na baadae, watakapokwenda kwa jamii.
Mwalimu Mlezi wa serikali ya wanafunzi skuli ya sekondari
Limbani Maryam Omar Mohamed anasema, Serikali ya wanafunzi inawaandaa watoto
kuwa viongozi kwa asilimia 75, kwani wanawapa majukumu mazito, ambayo
wanayatekeleza kwa ufanisi.
"Wana uwezo wa kusimamia na kujieleza, tunaamini watakuwa
viongozi bora kwa sababu, wanawasaidia waalimu majukumu yao, pia wanawaelewesha
wanafunzi wenzao mara kwa mara," anasema.
Anafafanua, wanashughulikia paredi, usafi, inategemea na nafasi
yake aliyopangiwa, hivyo wanawajibika vizuri.
"Umuhimu ni mkubwa wa serikali ya wanafunzi kwa sababu
wanatupunguzia baadhi ya majukumu, uzoefu wa wanafunzi, kuwasaidia wanafunzi
wenzao, ‘’anasema.
Serikali ya wanafunzi katika skuli hiyo ina jumla ya viongozi
14, wanawake tisa (9) na wanaume watano (5).
Mwalimu anaesimamia serikali ya wanafunzi skuli ya sekondari ya
Idrissa Abdulwakil Kizimbani, Ghalib Said Mohamed, anasema lengo lao ni
kumfanya mwanafunzi, aweze kujiamini kwani wanamfuatilia jinsi anavyoweza
kuwajibika.
"Uongozi huo hauwakwazi wanafunzi bali unawajenga vizuri
kiakili kwa sababu hawatolewi kwenye vipindi vya masomo, muda wa kusoma
wanasoma na muda wa kuwajibika kiuongozi wanawajibika," anasema.
Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed
Nassor Salim anasema, mtaala wao kuanzia maandalizi mpaka sekondari ya juu,
kuna masomo maalumu yanayoongeza vipaji na maarifa.
Mtaala wao umekuja na somo la historia na maadili, linalosaidia kutengeneza
viongozi, kwani mada hio inaimarisha uzalendo, historia na maadili, ambavyo ni
vitu muhimu katika uongozi wa baadae.
Wanawasaidia zaidi watoto wa kike kwa kuimarisha dakhalia,
ambapo wamekubaliana wizara, kwamba wanafunzi watakaofaulu vizuri masomo yao na
kupata daraja la A na B, wataweka skuli maalumu za michepuo, hivyo mabinti
wanafaidika zaidi.
Mdhamini anafafanua, hiyo ni kwa sababu katika skuli za kawaida
za kwenda na kurudi, watoto wa kike wanapata vikwazo vingi zaidi, ambavyo
vinawanyima nafasi ya kufanya vizuri kwenye masomo.
"Kwa mfano wanalazimika kutembea masafa marefu na mazingira
mengine ni hatarishi, pia baadhi ya familia tamaduni zao haziwapi nafasi ya
kusoma, wanapofika nyumbani wanakuwa ni mama wa nyumba," anaeleza.
Mdhamini huyo alitaja jambo jingine linalowaandaa watoto wa kike
kwamba, ni namna ya uchawanyaji wa skuli katika visiwa vidogo vidogo na maeneo
tengefu, kwani wasichana walikuwa wakipata shida kuvuuka ingawa baada ya kujenga
skuli hizo, kikwazo hicho kimewaondokea.
"Tumeimarisha utaratibu wa ushauri nasaha kwa kuwapa
mafunzo walimu na skuli zilizojengwa tumeweka vyumba maalumu kwa ajili ya
walimu wa ushauri nasaha," anafafanua.
Kumbe uwepo wa vyumba maalumu vya kubadilishia nguo, wakiwa katika
mizunguko yao ya heidhi, ili wapate fursa ya kusoma kwani kufanya hivyo ni
kutengeneza mama na kiongozi bora wa baadae.
Anaeleza, wamekuwa wakishirikiana na taasisi mbali mbali za serikali
na binafsi ikiwemo chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar
(TAMWA), na chama cha Wanasheria Zanzibar (ZAFELA) katika kuimarisha
uongozi kwa wanafunzi.
Mdhamini huyo anafafanua, kwa sasa mabadiliko yapo kwani watoto
wa kike wa miaka hii wana uwezo mkubwa ukilingalisha na mwanafunzi msichana wa
miaka ya 70 na 80.
"Kwanza ufaulu katika masomo ya sayansi umeimarika kwa
wanafunzi wa kike, na kilichosaidia ni kujiamini kwao kutokana na walivyojengwa
kuwa na uwezo wa kuzungumza popote bila ya woga," anasema.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba ‘PEGAO’ Hafidh Abdi Said, ni jambo
jema lililofanywa na wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa kuwaandaa watoto
mapema kuujua uongozi kupitia klabu mbali mbali skulini.
Anasema, wanaamini kwamba lengo lao la kufikia 50 kwa 50 katika safu
ya uongozi yatafanikiwa, kwani elimu wanayoipata watoto wakiwa skuli, itawasaidia
kuwajengea ukakamavu na kujiamini.
"Wasichana wataanza kujiamini mapema kwani nafasi
wanazopewa skuli ni kubwa na zinawajengea ujasiri wa kuzungumza mbele ya jamii, na kupata uzoefu wa kuongoza akiwa mdogo.
MWISHO.


Comments
Post a Comment