NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@@
MKUU wa wilaya ya Mkoani Dk. Hamad Omar Bakari, kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, katika mashindani ya tano ya tahafidhil-quran, ya kanda ya Wambaa wilayani humo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Katibu wa Jumuiya ya tahafidhil qur-an kanda ya Wambaa, Mwalimu Abdalla Haji Ali, alisema tayari maandalizi ya shughuli hiyo, yameshakamilika.
Alisema, mkuu huyo wa wilaya, atawashuhudia wanafunzi wakishindana kwa juzuu ya kwanza, pili, tatu, tano, saba, 10 na 15 wakiwemo wanafunzi wa kike na kiume.
Alieleza kuwa, mashindani hayo ya aina yake kwa mwaka huu, yanatarajiwa kufanyika msikiti wa Ijumaa, uliopo kijiji cha Chumbageni Wambaa wilaya ya Mkoani Pemba.
Alisema, baada ya majaji kukamilisha kazi yao hiyo na kutoa matokeo, mgeni rasmi huyo atatoa zawadi ikiwemo fedha taslimu, kwa washindi na washiriki wote 42.
āāNi kweli asubuhi hii, ndani ya msikiti wa Ijumaa Chumbageni, mkuu wetu wa wilaya ya Mkoani Dk. Hamad Omar Bakari, atayashuhudia mashindani ya tano ya tahafidhi qur-an, yanayoandaliwa na jumuia yetu,āāalifafanua.
Akizitaja madrassa saba zitakazoshiriki kwa mwaka huu, Katibu huyo, alisema ni pamoja na almadrassatul- raufu rrahim ya kijiji cha Andikoni, allah kadiri ya kijiji cha Wambaa.
Madrassa nyingine zilizothibitisha kushiriki ni minatu rrahman ya Kwazani, nur-ddin ya Ndongoni, hidayatul- islamiya ya Andikoni, kaafur ya Tumbi na imaniya ya Chumbageni.
Katika hatua nyingine, Katib huyo aliwaomba waumini wa dini ya kiislamu wa shehia za Wambaa na Chumbageni na shehia jirani, kuhudhuria katika mashindani hayo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Hassan Othman Khamis, aliwashukuru waumini wa dini ya kiislamu na mashinrika mingine, kwa kutoa michango yao, iliyofanikisha kufanyika kwa mashindani hayo.
Alisema, michango ya wazazi, walezi, viongozi wa jimbo la Chambani, ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mkoani, waalimu wa skuli za Tumbi, Kunguni, Wambaa na baadhi ya wawekezaji, imesaidia kwa kiwango kikubwa.
Mwalimu mkuu wa almadrassatui Allah kadiri ya Wambaa Awesi Abdalla Ali, alisema maandalizi kwa upande wake, yameshakamilika ikiwemo wale wanafunzi wa juzuu ya kwanza hadi ya 10.
Mshika fedha wa Jumuiya hiyo, Ali Juma Khamis, alisema walipanga kukusanya shilingi milioni 1.6 kwa ajili ya zawadi za washindi na sadaka kwa washiriki, ingawa wamefanikiwa kukukusanya shilingi milioni 1.34.
āāKwa fedha tulizokusanya mwaka huu, zimesaidia kwa kiwango kikubwa kufanikisha shughuli yetu, ikilinganishwa na mwaka jana, jambo ambalo tunaona tumepiga hatua,āāalifafanua.
Baadhi ya wananchi wa shehia za Chumbageni na Wambaa walisema, wamefurahishwa kwa kukamilika kwa maandalizi hayo, na kuwaomba wenzao kuhudhuria.
Fatma Abuu Fakih, alisema ni vyema kwa wazazi na walezi, kushiriki ili kuwanga mkono watoto wao, kuzidi kukihifadhi kitabu cha Muumba.
Raya Juma Khamis na Asha Haji Ali, walisema ni wakati wao wazazi, kuwashajiisha watoto namna bora ya kukihifadhi kitabu cha Allah, ili kikawe muombezi kwao.
Hii ni mara ya tano, kwa Jumuia hiyo tahafidhi qur-an kanda ya Wambaa na Chumbageni wilaya ya Mkoani Pemba, kuendesha mashindani hayo, ambapo kwa mwaka jana ilihusisha madrassa sita pakee.
Mwisho
Comments
Post a Comment