NA SALUM VUAI, ZANZIBAR@@@@ KUFUATIA uteuzi wa Mawaziri wapya Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu uliokirudisha madarakani Chama cha Mapinduzi, waandishi wa habari hawakusita kutoa ya moyoni wakieleza matumaini waliyonayo katika kuimarika zaidi kwa sekta ya habari. Wadau wa habari na waandishi waliozungumza na gazeti hili, wamesema kwa miaka mingi, sekta ya habari visiwani Zanzibar imekuwa ikipata mafanikio kadhaa, ingawa pia wamebainisha changamoto mbalimbali zinazowabana katika utekelezaji wa majukumu yao. Wamesifu kuongezeka kwa uhuru wa habari kwa kiasi fulani, lakini wakaeleza kuwa bado baadhi ya watu wanatawaliwa na dhana potofu kwamba waandishi wa habari hawapaswi kuwa marafiki wa kudumu bali ni wa msimu tu hasa pale maslahi yao binafsi yanapohusika. Kutokana na fikra kama hizo, mara kwa mara waandishi wamekuwa wakinyimwa taarifa au kuamriwa kutozitangaza hasa ikiwa jambo linalotakiwa linahusu uzembe, hujuma au makosa ya mtu...