NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WAHITIMU kidato cha nne skuli ya sekondari Wambaa wilaya ya Mkoani Pemba, wamekumbushwa kuwa, elimu waliyoipata bado ni ndogo, hasa kwa ulimwengu ulivyo, na badala yake, watafute namna ya kujiendeleza.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba ‘TUJIPE’ Tatu Abdalla Msellem, kwenye mahafali ya 18 ya wanafunzi hao, yaliofanyika skulini hapo.
Aliwaambia wahitimu hao kuwa, kwa sasa elimu imeongezeka thamani, na ndio maana kidato cha nne ni kama mwanzo wa kutafuta elimu, hivyo wahakikishe wanashirikiana na familia zao, ili kujisomea zaidi.
Alieleza kuwa, kwa sasa kuanzia kidato cha sita na kuendelea, ndio mwanzo wa elimu, hivyo kwa wale wanafunzi ambao hatobahatika kuendelea kidato cha tano na sita, wasivunjike moyo.
‘’Elimu ya kidato cha nne, kama ndio mwanzo wa elimu kwa dunia ya sasa, na wale ambao hawatobahatika, bado nafasi ya kujiendeleza kimasomo wanayo,’’aliwakumbusha.
Aidha Mkurugenzi huyo Mtendaji wa ‘TUJIPE’ aliwasisitiza wahitimu hao, kutojiingiza kwenye vitendo viovu muda wote wanpokua uraiani.
Katika hatua nyingine, aliahidi kusaidia gharama za wanafunzi watakaokaa kambi hapo mwakani na kusaidia vifaa kwa watakaoendelea kidato cha tano na sita moja kwa moja.
Akizungumzia nafasi ya wazazi na walezi, Mkurugenzi huyo aliwataka kuendelea kuwaelekeza watoto wao mambo mema ya kufanya, ili wawe raia wema muda wote.
‘’Nje kunaudhalilishaji, kuna matumizi ya dawa za kulevya, kuna wizi na matumizi ya bangi, bado wazazi tunalojukumu la kuhakikisha viajana hawa, hawaingii kwenye majanga hayo,’’alifafanua.
Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo Mohamed Abdi Mohamed, alisisitiza uendelevu wa nidhamu kwa wahitimu hao, kwani kwa sasa, inakuwa rahisi mkono wa sheria kuwakumba.
Mapema Mwenyekiti wa kamati ya wazazi skulini hapo Abdalla Salim Juma, aliwakumbusha, kuhakikisha wanajisomea zaidi, elimu ya kumjua Muumba, ili wapate radhi zake.
‘’Ili utafute maisha na kujua misingi yake, jambo la kwanza ni kupata elimu ya kumjuua Muumba, ili kila unalolifanya, liwe rahisi na lenye baraka,’’alieleza.
Mwalimu Khamis Khatib Khamis, akitoa salamu kwa niaba ya waalimu wenzake, aliwataka wahitimu hao kujipanga vyema, ili kuyashinda mazingira yao.
Akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Mohamed Khamis Abdalla, alisema wamejifunza mingi wakiwa skulini hapo, na kuahidi kuyaendeleza wakiwa uraiani.
Hata hivyo, walisema changamoto kubwa inayokabili ni uwepo wa ukaribu wa wanafunzi wa msingi na kupelekea, kukosa utulivu wa uzingatiaji wa masomo.
Mwalimu mstaafu wa skuli hiyo Juma Suleiman, alisema elimu ndio msingi mkuu wa maisha ya mwanadamu, hivyo hilo katika maisha yao, liwe ndio kipaumbele pekee.
Katika mahafali hayo ya 18, wanafunzi hao 97, waliandaa utenzi, ambao ulijaa huzuni, maono yao, mwelekeo, ushauri kwa wanafunzi wenzao, wazazi na waalimu, ambapo kwa mwaka jana wanafunzi 86, kati yao 10 waliingia kidato cha tano.
Mwisho
Comments
Post a Comment