NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI wa vijiji vya Tironi na Kionwa,
wilaya ya Mkoani Pemba, wameikumbusha wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, kuwafikiria ujenzi wa barabara yao kwa
kiwango cha lami, iliyoanzia Mbunguwani.
Walisema, wanaona wivu mkubwa kuona zipo barabara za
ndani, kwa sasa zinaendelea na ujenzi, ambao yao haijaanza hata kupimwa.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo,
walisema wakati umefika kwa sasa, kwa wizara husika, kuwatupia jicho, ili
waondokane na usumbufu hasa kipincdi cha mvua.
Walisema, barabara yao imekuwa ikitoa kwa wingi zao la taifa
la karafuu, hivyo ni vyema sasa mapato ya nchi hii, yakaelekezwa kwao, kwa
ujenzi wa barabara yao.
Mmoja kati ya wananchi hao Maryam Haji Khamis, alisema
wamekuwa wakipata dhiki, hasa wanapopata uhamisho wa kimatibabu.
‘’Kwa mfano sisi wazazi, wakati mwingine tunahitajika
kwenda kirufaa hospitali ya wilaya ya Mkoani, lakini usumbufu, ni uwepo wa barabara
iliyochakaa,’’alieleza.
Nae Hasina Juma Abdalla, alisema bado barabara yao licha
kuwekewa kifusi kwa yale maeneo yenye shida, wanapata usumbufu mvua zikianza.
Kwa upande wake Muhamad Khamis Muhamad, alisema huu sio
wakati tena, wa kupita juu ya barabara za mawe na udongo, bali iwe ni juu ya lami.
‘’Wenzetu kama barabara za Likoni, Mtale, Kiuyu Mbuyuni,
Mtangani zinatangaazwa kwamba, ujenzi wake umeshaanza, lakini ya kwetu bado,’’alilalamika.
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Khatiba Juma Mjaja, alisema
barabara hiyo na nyingine za wilayani humo, zimo kwenye mpango wa uhakika wa ujenzi.
Alisema, Dk. Mwinyi ameshaazimia kuzijenga barabara zote
za ndani, kwa kiwango cha lami, ikiwemo hiyo ya Mbuguani- Tironi hadi Kionwa,
hivyo wananchi wendelee kuwa wastahamilivu.
‘Mimi taarifa nilizozo kuwa, ujenzi wa barabara hiyo
wakati wowote utaanza, maana zipo kazi zimeshafanywa kwa ajili ya matayarisho
hayo,’’alieleza.
Mapema Afisa Mdhamini wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi Pemba, Ibrahim Saleh Juma, alikiri kuwa, matayarisho ya ujenzi wa
barabara hiyo, tayari umeshawiva.
Alisema, zoezi la upimaji limeshakamilika na tayari
kamati ya watu tisa (9), imeshahimitisha kazi yake, ambayo imeshaleta mapendekezo
juu miti ambayo itaondoka, wakati wa ujenzi.
‘’Kwa sasa tunaomfumo wa ujenzi wa barabara unaozingatia
mazingira, na ndio maana tunayokamati maalum, ambayo moja ya kazi yake ni hiyo,’’alieleza.
Alifafanua kuwa, kamati hiyo yenye wataalamu, huangalia
barabara iegemee upande gani, ili kuepusha ukataji wa miti, usiokuwa wa lazima
wakati wa ujenzi ukianza.
Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi wa vijiji vya Tironi
na Kionwa, kuendelea kuwa wastahamilivu kw amuda mfupi, wakijua kuwa ujenzi wa
barabara yao utafanyika.
‘’Unajua kasi ya Dk. Mwinyi ni ya mfano wa pekee, maana
kati ya zile kilomita 275 za kwa Zanzibar, nasi Pemba kwa awamu ya kwanza, tunakilomita
134 ambazo kazi inaendelea kwa kasi,’’alieleza.
Imefahamika
kuwa, Zanzibar yote inaomtandao wa barabara usiozidi kilomita 1,344, na wakati
anagia madarakani miaka minne iliyopita, kulikuwa na wastani wa asilimi 40 ya
barabara, zilizojengwa kwa kiwango cha lami, na asilimia 60, zilizobakia
zilikuwa na kifusi na udongo.
Akizungumza
hivi karibuni, Waziri wa wizara hiyo Dk. Khalid Salum Mohamed, alisema moja ya
kipaumbele ndani ya awamu ya nane, ni kuhakikisha barabara zote, zimejengwa kwa
kiwango cha lami, ikiwemo la Tironi.
Mwisho
Comments
Post a Comment