NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MWEMVULI wa asasi za kiraia Pemba ‘PACSO’
umekutana na wadau wake, ili kuibua changamoto za kisheria na kisera,
zinazotajwa kurejesha nyuma, utendaji wa kazi zao na jamii kwa ujumla.
Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika leo Novemba 3, 2024 ukumbi wa Maktaba
Chake chake, Katibu Mkuu wa ‘PACSO’ Sifuni Ali Haji, alisema lengo la mkutano
huo, ni kuibua changamoto hizo na kuzifanyia kazi.
Alisema, ‘PACSO’ kwa sasa inaendelea na utekelezaji wa mradi
wa urai wetu, ambapo moja ya eneo la utekelezaji wake, ni kuibua changamoto za
kisheria na sera, zinazokwaza makundi ya vijana, wanawake na watu wenye
ulemavu.
Alieleza kuwa, changamoto hizo kisha, huziwasilisha kwa
jumuia pacha wanaotekeleza mradi huo pamoja, ambayo ni Jumuiya ya wanawake
wenye ulemavu Zanzibar ‘JUWAUZA’.
Katibu Mkuu huyo alifahamisha kuwa, mfano wa jambo kama hilo,
tayari zipo changamoto ambazo awali ya mwaka huu, ziliibuliwa na ‘PACSO’ na kuzifikisha
kwa ‘JUWAUZA’ kwa hatua ya kuzifikisha serikalini.
‘’Mkutano huu wa siku moja, ni muendelezo wa mikutano yetu
mbali mbali, inayofanywa kupitia mradi wa uraia wetu, na leo (jana), tunataka
muufahamu mradi na kisha kuwasilisha changamoto za kisheria na sera,’’alieleza.
Hata hivyo Katib Mkuu huyo, alisema kama asasi za kiraia
zikungana kwa dhati, hakutakuwa vikwazo, kwenye utendaji wa shughuli zao.
‘’Ikiwa tutaendelea kujifungia na kufanyakazi kila mmoja
peke yake, tutaendelea kuandamwa na changamoto za kikazi kila siku, lakini
umoja wetu, ndio hatma yetu,’’alifafanua.
Mapema akifungua mkutano huo, Mratibu wa miradi kutoka ‘PACSO’
Mohamed Najim Omar, alisema uraia wetu ni mradi wa kukuza mazingira wezeshi,
kwa asasi za kiraia zenye uwezo wa kushiriki, katika utawala wa kidemokrasia
nchini.
Alisema, mradi huo unatekeleza na ‘the foundation for Civil
society’ kwa kushirikiana na ‘PACSO’ kwa Pemba na kituo cha majadiliano kwa
vijana ‘CYD’.
Alieleza kuwa, mradi huo umegawika maeneo matatu makuu,
ikiwemo ngazi ya kitaifa, taifa na utekelezaji kwenye makundi maalum, wakiwemo
wanawake na vijana.
Mratibu huyo alifafanuwa kuwa, kwa ngazi ya kitaifa mradi unatekelezwa
na asasi kadhaa ikiwemo Jukwaa la Katiba Tanzania ‘JUKATA’, Tanganyika law
society kwa upande wa Tanzania bara na JUWAUZA kwa Zanzibar.
‘’Kupitia mradi huu, tayari tumeshakutana na makundi ya watu
wenye ulemavu, wanawake, vijana, waandishi wa habari na maafisa wa serikalini, nao
waliibua changamoto zao za kisheria na kisera,’’alifafanua.
Akizungumzia lengo la mradi, Mratibu huyo alisema ni kuchangia
kuwepo kwa mfumo wa sera na kisheria, ambao umeimarishwa na kuwezesha mazingira
mazuri ya ushirikishwaji wa asasi za kiraia, kama watendaji wakuu wa utawala bora
na demokrasia.
‘’Lakini malengo mahasusi moja wapo ni asasi, kuwa na taarifa
sahihi ya kila eneo, pili ni kupanga na kuimarisha uwezo wa asasi kuwa na ushirikiano
na serikali na kusaidia asasi hizo, kuendesha midahalo ya wazi na serikali,’’alifafanua.
Mapema akichangia utoaji wa changamoto za kisera na kisheria,
Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Mkoani Nassor Hakim Haji,
alisema moja ni kutopewa mikataba kwa baadhi ya wafanyakazi wa kampuni za
kigeni.
Nae Abdi Nassor Abdi, alisema pia kuna changamoto kwa
wafanayabiashara ya kudaiwa tozo la risiti mara mbili, wanapotoka kisiwa kimoja
na chingine wanapokuwa na bidhaa zao.
Kwa upande wake, Juma Bakar Alawi, alisema kuna fedha za mikopo kwa watu wenye ulemavu, kupitia
mabaraza ya miji na halmashauri, ingawa kumekuwa na changamoto ya upatikanaji
wake.
Nae mjumbe kutoka Jumuiya ya wenye dalala na gari za mizigo
mkoa wa kusini Pemba ‘PESTA’, Ali Hemed Soud, alisema changamoto ya kisera, ni
eneo la ulipajwa fedha za bima kwa
mwaka, ingawa gari za abiria, wanafanya kazi miezi sita.
Mkutano huo, ni sehemu ya
utekelezaji wa mradi wa ‘uraia wetu’ unaotekelezwa na ‘PACSO’ kwa muda wa miaka
minne, kwa ufadhili wa ‘the foundation for civil society’ kupitia Umoja wa nchi
za Ulaya ‘EU.’
Mwisho
Comments
Post a Comment