NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
WATENDAJI wa taasisi kisiwani Pemba wametakiwa kuacha tabia ya kutumia makaratasi kwenye shughuli zao za kiofisi na badala yake waendelee kutumia mfumo wa kidigitali, ili kuwarahisishia katika utendaji wa kazi zao za kila siku.
Akifungua mafunzo ya mfumo wa vibali vya safari za nje ya nchi (ZanVibali), leo Machi 4, 2024 Chake chake Pemba, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandis Zena Ahmed Said alisema, mfumo wa kidigitali ni rahisi na mtumishi atapata kibali kwa haraka.
Alisema kuwa mfumo huo ni muhimu sana kwani kutakuwa na uwazi na uwajibikaji, Serikali itaona fedha zote za gharama zitakazotumika kwenye safari pamoja na kurahisisha upatikanaji wa vibali kwa watumishi hao ambapo wakitumia makaratasi huchukua mda mrefu.
"Tumeweka mfumo huu kwa ajili ya kuleta tija kwetu kwa sababu mfumo wa makaratasi una changamoto nyingi, hivyo huu utaturahisishia kila kitu na utapata kibali kwa urahisi zaidi pasi na kikwazo chochote," alisema.
Mhandis huyo alizielekeza taasisi zote kutumia mfumo wa kidigitali wa ZanVibali na ZanMalipo ili kuipatia Serikali mapato ambayo ndio yanayotumika katika kuwalipa wafanyakazi na kujenga miundombinu mbali mbali kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
"Tutumie hii mifumo, tutoe na tudai risiti ili tupate mapato mengi yatakayotusaidia kupata maendeleo katika nchi yetu," alieleza Katibu huyo.
Aidha Mhandis Zena aliwataka viongozi wa taasisi kuzisoma Sheria, kanuni na kuzisimamia, ili kuwajibika ipasavyo sambamba na kuchukua hatua za kinidhamu kwa mtendaji ambae atakwenda kinyume na maadili ya Utumishi wa umma.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Wakala wa Serikali Mtandao Zanzibar Said Seif Said aliwataka viongozi hao wa taasisi kukubali mabadiliko ya kidigitali ili yapatikane kwa urahisi.
"Mambo mengi sasa yatabadilika kutoka analogi kuja kwenye digitali, hivyo tujitahidi sana makusanyo ya mapato ya Serikali yapitie kwenye mfumo wa digitali na tushirikiane kuhakikisha tunatimiza lengo la Serikali kwa haraka na kwa ufanisi," alifahamisha Mkurugenzi huyo.
Nae Afisa Mdhamini Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Pemba Halima Khamis Ali alieleza kuwa, kila mmoja kwa nafasi yake ana wajibu wa kusimamia na kutekeleza yale ambayo yanaleta mageuzi katika Serikali.
"Tuna mifumo tofauti, mengine imeshaanza kutumika na mengine wataendelea, zile changamoto zilizopo tuzione ni fursa, hivyo tusiwe ni miongoni mwa wanaokwamisha bali tusimamie ili kufanikiwa," alieleza.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo Awena Rajab Mohamed kutoka eGAZ alitaja miongoni mwa faida kuwa ni kuongezeka kwa uwazi wa taarifa za vibali na kufanya maamuzi sahihi kwa wakati unatakiwa.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamewashirikisha watendaji wa kada mbali mbali kwa siku tofauti, yameandaliwa na Wakala wa Serikali Mtandao Zanzibar ambayo yamefanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha Gombani Chake Chake.
MWISHO.
Comments
Post a Comment