IMEANDIKWA
NA ZUHURA JUMA, PEMBA
NAIBU
Mrajis Mahakama Kuu Pemba Faraji Shomari Juma amesema, kuanzia mwaka mpya wa
mahakama 2023 wamejipanga kutumia mitandao katika shughuli mbali mbali za kudai
na kutoa haki mahakamani, ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa mahakama, wadau
na wananchi.
Alisema kuwa, utumiaji wa mitandao hiyo katika kudai, kutoa na
kufuatilia haki mahakamani kutapelekea kukuwa kwa uchumi wa nchi na ustawi wa
jamii kwa ujumla.
Aizungumza na waandishi wa habari mjini Chake Chake ikiwa ni
katika kuadhimisha wiki ya sheria, Naibu Mrajis huyo alisema kupitia kauli mbiu
ya mwaka huu ya ‘Haki Mtandao Kwa Kukuza Uchumi na Ustawi wa Jamii’ mahakama imeanza kutumia mitandao kwa
kuanzisha mfumo wa kusimamia kesi, malipo kwa njia ya Zan malipo na mfumo wa
usajili wa mawakili.
“Kupitia kauli mbiu hiyo wananchi na wadu wakubwa wa mahakama
wataweza kusaidia kukuza uchumi na ustawi wa jamii kwa sababu itakuwa
tunadhibiti fedha, itapunguza gharama kwani mwananchi anaweza kufungua kesi
hata akiwa nyumbani, kesi itachukua mda mfupi na mashahidi watapatikiana hata
wakiwa nje ya Pemba”, alisema.
Naibu huyo alisema kuwa, mwaka 2022 mahakama za Pemba
zilipokea kesi za jinai 2,318 ambapo 2,107 zimetolewa maamuzi (hukumu) na kesi
211 zinaendelea kusikilizwa, huku kesi za madai zikiwa ni 84 ambazo 67
zimepatiwa ufumbuzi na keasi 16 zinaendelea.
“Kati ya kesi hizo za jinai, kesi za udhalilishaji zilifikishwa 48 kwa Mkoa wa Kusini Pemba, kesi 40 zimepata hukumu na zinazoendelea ni nane (8), lakini kwa Mkoa wa Kaskazini Pemba zilifikishwa mahakamani kesi 46, ambapo 33 zimepata hukumu na 13 zinaedelea”, alifafanua.
Aidha alisema kuwa, kesi 26 za madawa ya kulevya Mkoa wa
Kusini Pemba zilifikishwa mahakamani na kupatiwa hukumu kesi 17 huku Mkoa wa
Kaskazini Pemba zikifikishwa kesi 14, ambazo zote zimepata hukumu.
Kwa upande wake Kadhi wa Rufaa Pemba Daud Khamis Salim akitaja
sababu zinazopelekea ndoa kuvunjika ni kubadilika kwa tamaduni za asili katika
jamii, kukosa elimu ya ndoa, kukosa ustahamilivu pamoja na utandawazi.
“Vijana wa sasa hawataki kufundishwa na wala hawana elimu ya
ndoa, hawana ustahamilivu, hivyo wanapokosana kidogo hakuna suluhu inayoendelea,
lakini zamani ilikuwa linapotokea tatizo wazazi huwaita na kuwasuluhisha”,
alisema Kadhi huyo.
Nae Naibu Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi Pemba Haji Ibrahim
Haji aliwaomba waandishi wa habari kupitia vyombo vyao, kushirikiana na
mahakama katika kuwaelimisha wananchi juu ya kauli mbiu ya mwaka huu, ili
wananchi waitumie kwa vitendo.
Wiki ya Sheria mwaka huu imeanza Febuari 6 na kilele chake
kinatarajiwa kuwa Febuari 13, ambapo watafanya ziara za kutoa elimu katika
kisiwa Kojani, Makoongwe, kijiji cha Micheweni na Uwandani pamoja na kufanya usafi katika hospital ya
Wete.
MWISHO.
Comments
Post a Comment