NA HAJI NASSOR, UNGUJA
WAAANDISHI wa habari wameshauriwa kutoa maoni
yao katika kupata sheria mpya ya habari,. ambayo itapelekea kufanya kazi zao kwa
ufanisi bila kukandamiza uhuru wao.
Mjumbe wa Bodi ya Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania (TAMWA), Shifaa Said Hassan, alieleza hayo Febuari 8, 2023 wakati akifungua
mkutano wa majadiliano kuhusu sheria zinazokandamiza uhuru wa habari Zanzibar
kwa vyombo vya habari uliofanyika katika ukumbi wa Mfuko wa Hifadhi wa Jamii Zanzibar ZSSF Kariakoo mjini Unguja.
Alisema kupatikana kwa uhuru wa vyombo vya
habari nchini ni fursa ya kuwa na sheria na muundo huo utakaoendana na wakati
uliopo.
Alibainisha kuwa tasnia ya bahari ni muhimu
katika nchi kwani inachochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla
kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Aidha alisema wanabari ndio wanaojua changamoto
wanazokabiliana nazo katika utelelezaji wa majukumu yao ikiwemo kukosa taarifa katika
wizara na tasisi za serikali hali ambayo inakandamiza uhuru wao hasa wa
kikatiba hivyo vyema kutoa maoni yao ambayo yatasaidia kupata sheria nzuri.
Mjumbe Shifaa alibainisha kuwa Zanzibar kuna
sheria kuu mbili za habari ikiwemo ile ya magazeti na vitabu ya mwaka 1988,
sheria ya vyombo vya utangazaji ya mwaka 97 na sheria nyengine kadhaa ambazo
zinakandamiza na kukinzana na uhuru wa habari.
Hivyo alisema ni imani yake kwamba baada ya
mafunzo hayo watapata matokeo mazuri ya kuwa na sheria mpya ya habari ambayo
itawafanya wanabari kufanya kazi zao kwa ufanisi na umahiri mkubwa.
“Zipo sheria ambazo zinakinzana katika masuala
ya habari mtoe maoni yenu na michango ambayo itasaidia na pale itakapopelekwa
Baraza la Wawakilishi basi iwe nzuri na kuwapa uhuru wanahabari katika utoaji
wa taarifa,” alisema.
Mbali na hayo aliwataka wanahabari kupaza sauti
zao kupitia vyombo vyao vya habari katika kuhakikisha wanapata sheria nzuri
ambayo itaendana na wakati wa sasa.
Aliiwapongeza Intervews na Shirika la USAID
kushirikiana pamoja kutoa mafunzo hayo ambayo ambayo anaamini sheria mpya ya
habari itakayokuwa nzuri na itatoa uhuru kwa vyombo vya habari vilivyokuwepo
nchini.
Mkuu wa Chuo cha Uandishi wa Habari wa Chuo
Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Iman Duwe alisema katiba ya Zanzibar kifungu
cha 18 (1) kimetoa haki ya wananchi kupata taarifa na habari katika nchi yao.
Alisema vipo vifungu vingi katika sheria ya
habari vinatakiwa kubadilishwa kwani baadhi yake vinanyima uhuru wa habari
kwani sheria nzuri ni ile inayoainisha kila kitu.
Alibainisha kuwa vipo baadhi ya vifungu katika
sheria ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu namba 5 ya mwaka 1988
licha ya kufanyiwa marekebisho kadhaa.
Mkuu Duwe alivitaja vifungu hivyo kuwa ni cha 27
(1) cha sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu nambari 5 ya mwaka 1988 kinachotoa
mamlaka kwa ofisa yoyote wa Polisi kufanya ukaguzi na kumamata gazeti lolote
limechapishwa iwapo atashuku kuwa limechapishwa kinyume na sheria.
Alisema kupitia kifungu hicho Polisi amepewa
mamlaka ya kushikilia mali za gazeti jambo linalonyanganya haki ya kutoa habari
iliyoainishwa na katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Kwa upande wa Sheria ya Tume ya Utangazaji ya Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997, alisema kifungu cha 7 (2) hakijakaa sawa kwani
kinampa uwezo tume kufanya kazi nyengine yoyote atakayopangiwa hivyo ni vyema
sheria hiyo ikaeleza au kutaja kazi hizo ili kuepusha kutumika vibaya kifungu
hicho.
Juma Khamis Juma ni Mwandishi wa Habari ambae
pia ni Mwanasheria wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, sheria ya
kufuta sheria ya Baraza la Wawakishi (Kinga, Uwezo na Fursa) namba 4 ya 2007 na
kutunga sheria mpya ya Baraza la Wawakilishi (Kinga, Uwezo na Fursa) kutekeleza
kazi na mambo mengine yanayohusiana na hayo namba 6 ya mwaka 2022 ina vifungu
vinavyominya uhuru wa habari.
Alisema katika kifungu cha 27 cha sheria hiyo
kinaeleza kwamba utaratibu wowote Baraza au Kamati ambapo mtu yoyote atatakiwa
kutoa ushahidi au kuwasilisha nyaraka, utahesabiwa kama amekiuka utaratibu wa
kimahakama.
Mwanasheria Juma alisema hali hiyo inaathiri
uandishi wa habari za uchunguzi na ni kinyume na kanuni ya uwazi na
uwajibikaji.
Hata hivyo akizungumzia sheria ya kufuta sheria
ya uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984 na kutunga sheria ya uchgazi ya mwaka 2017
na masuala mengine yanayohusiana na hayo kuna vifungu vinavyokataza mtu
kutangaza matokeo ya uchaguzi ambayo hayathibitishwa na tume licha kuwa
yametolewa na maofisa wa tume katika ngazi za vituo au jimbo.
Alibainisha kuwa vifungu hivyo vinatoa adhabu
kubwa ambazo kimsingi vinawapa hofu waandishi wa habari kufanya kazi vizuri.
“Vifungu hivi vinakiuka utu wa mtu na umuhimu wa
waandishi wa habari hivyo ni vyema nyinyi wadau kuendelea kupaza sauti zenu ili
tasisi zinazohusika na sheria kuzipatia
upya ili ziendane na wakati,” alisisitiza.
Mbali na hayo alisisitiza umuhimu kwa wanahabari
kuwa na sheria na kanuni mbalimbali kwa ajili ya kuzisoma ili ziweze kusaidia
katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Aliwataka wanahabari kuacha mihemko ya kubeba
wagombea na kufanya kazi kwa mujibu wa taaluma yao inavyowaelekeza.
Nao waandishi wa bahari wakichangia katika
mkutano huo walisema sheria nyingi zilizokuwepo Zanzibar zimeshapitwa na wakati
na zinahitaji kuwangaliwa.
Hivyo walisema ipo haja ya kuangaliwa kwa makini
vifungu vinavyokwaza uhuru wa habari katika baadhi ya sheria ili kuongeza
ufanisi wa kazi zao za kila siku.
Mkutano huo wa siku mbili, mada mbalimbali
ziliwasilishwa ikiwemo ya sheria ya usajili
wa wakala wa habari magazeti na vitabu namba 8 ya mwaka 1997, sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar namba 7 ya mwaka
1997 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010 na sheria ya makosa
ya mtandao 2015.
Mkutano huo umeandaliwa na Chama cha Waandishi
wa Habari Wanawake(TAMWA) Zanzibar na kuwashirisha
waandishi wa habari wa Unguja na Pemba chini ya ufadhiliwa mradi wa boresha
habari INTERNEWS na Shirika la Marekani
USAID.
Comments
Post a Comment