Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Abeida Rashid Abdallah amesema Wizara hiyo imepokea maoni yaliyotolewa na Wazee kuhusu kuifanyia marekebisho sheria ya Masuala ya Wazee, sheria namba mbili (2) ya mwaka 2020 katika kifungu kinachozungumzia umri wa mzee.
Akizungumza baada ya kikao cha pamoja baina ya watendaji wa wizara hiyo ,Kamati ya Kanuni na Sheria ndogo ndogo ya Baraza la Wawakilishi, wazee kutoka Jumuiya ya wazee (JUWAZA) pamoja na wazee wanaoishi katika makao ya wazee, kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika ukumbi wa Makao ya Wazee Sebleni, Unguja.
Alisema wazee wametaka kifungu cha sheria hiyo kifanyiwe marekebisho umri wa mzee uwe miaka 60 badala ya miaka 70. Hivyo watendaji wa wizara hiyo watakaa chini na kutafakari.
“Kamati imekuja kututembelea katika makao ya wazee, pamoja kupata maoni ya kanuni, ya masuala ya wazee iliyotungwa hivi karibuni lakini majadala mkubwa umejitokeza, baada ya kanuni hiyo kuonesha umri wa mzee ni miaka 70, na umri huo umewekwa kwa mujibu wa sheria ya masuala ya Wazee, hivyo wazee wametaka turudi kwenye sheria tuifanyie marekebisho ” Alisema katibu Mkuu huyo.
Aidha alisema kwamba Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussuin Ali Mwinyi amewaagiza watendaji wake kwamba endapo sheria ikionekana inaleta changamoto basi ifanyiwe marekebisho ili iendane na wakati uliyopo.
Alisema zaidi wajumbe wa kamati hiyo katika kikao cha majumuisho watatoa maelekezo kuhusiana na hilo, pamoja na wadau wengine ambao wanafanya kazi katika jumuiya za wazee katika kusimami masuala ya wazee.
Alieleza muda sio mrefu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto itatoa elimu dhidi ya kanuni ya Masuala ya Wazee (Utowaji Huduma za Makaazi ) kupitia makundi mbali mbali ndani ya jamii ili kila mtu aifahamu kanuni hiyo. kwani kanuni hiyo imetoa fursa mtu yeyote anaweza kuanzisha Makao ya Wazee.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mwera Mhe. Mihayo Juma N’Hunga amesema wako katika utaratibu wa kuchua maoni kwa wadau na kuangalia kama Kanuni hiyo inafanya kazi na kama kuna mapungufu basi ifanyiwe marekebisho
Alisema kanuni hiyo imetungwa mwezi April mwaka huu, hivyo kamati inafuatilia utekelezaji wake na ndio maana walianza na ziara ya kuwatembelewa wazee katika makao ya Wazee, Limbani Pemba, na kwa upande wa Unguja Welezo na Sebleni na kuwauliza masuala mbali mbali kuhusiana na kanuni.
Kwa upande wa Wazee akizungumza Bi Salama Kombo Ahmed kwa niaba ya wazee wa Jumuiya wa Wazee Zanzibar (JUWAZA) alisema Serikali ya Zanzibar inamuachisha mtu kazi anapofikia umri wa miaka 60 na sio 70, hivyo sheria ifanyiwe marekebisho.
Mwisho
Comments
Post a Comment