NA HAJI NASSOR, PEMBA
WANAWAKE wa kisiwa kidogo cha Fundo
wilaya ya Wete Pemba, wamesema umbali wa kilomita zaidi ya 60 kwa usafiri wa
baharini kutoka kisiwani hapo, hadi kilipo kituo cha Polisi Wete, ni moja ya
changamoto zainazowafanya wasiyaripoti mara kwa mara, matukio ya kihafalifu wanayofanyiwa.
Wamesema
wamekuwa wakifanyiwa vitendo viovu kama vile kuharibiwa mitego yao, kilimo chao
cha mwani na kisha kutukanwa, ingawa wamekuwa na uzito kukifuata kituo cha
Polisi Wete.
Walisema,
suluhushi la wao kuyaripoti matendo wanayofanyiwa na vijana wa kisiwa hicho,
ni kujengewa kituo kidogo cha Polisi ili karibu yao.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi kisiwani hapo, walisema hawaishi kwa amani na
utulivu kama walivyo wanawake wengine vijiji vyengine, kutokana na kutishiwa
hata usalama wao.
Mmoja kati
ya wanawake hao Mwajuma Rashid Salmin, alisema wanapoharibiwa mashamba yao ya
mwani na vijana kisha hurejea kuwatukana.
Alieleza
kuwa, pamoja na hivyo, wamekuwa wakiwatishia matusi jambo linalowakosesha
furaha katika maisha yao, jambo ambalo linawarejesha nyuma.
“Suluhisho
la hili tunalofanyiwa na vijana wetu, sasa ni kuwepo kwa kituo cha Polisi, ili
iwe rahisi sisi kufikisha malalamiko yetu, maana kituo cha Polisi cha wilaya
yetu kiko mbali,’’alilalamika.
Nae Hidaya
Omar Hassan, alisema wapo baadhi ya vijana wamekuwa wakiingia ndani kwa nia ya
ubakaji na wizi, ingawa unapowakamata hukutishia kwa maneneo maovu.
“Wanatuahidi
hata sisi wazazi kutubaka, na kutuharibia vipando vyetu pindi tukiwakataza,
sasa wakati umefika wa serikali kuangalia uwezekano wa kutujengea kituo cha
Polisi,’’alieleza.
Kwa upande
wake Hadia Hassan Mkombe alisema, wanaoendesha vitendo hivyo ni watoto wao wa
kuwazaa, wanaochukua mazoezi miji ya Nungwi na Wete mjini.
“Kwanza
huanza kuvuta sigara kisha bangi na kisha hujiingiza kwenye vitendo vya wizi
na baade kutoa matusi ya hadharani bila ya woga,’’alieleza.
Kwa upande
Omar Haji Ussi, alisema kilichokosekana kwenye shehia yao ya Fundo ni
kutokuwepo kwa kikundi cha ulinzi shirikishi na vijana kufanya watakavyo.
Nae Othman
Hamad Pandu mwenye ulemavu wa viungo, alisema ujenzi wa kituo cha Polisi
kinaweza kuwa suluhisho, iwapo watendaji wa jeshi la Polisi, watazitumia vyema
sheria.
Sheha wa
shehia ya Fundo Khamis Abeid, alisema kutokana na kisiwa hicho kuongezeka wa
idadi ya watu, navyo vitendo vya uvunjifu wa maadili vimeongezeka.
“Ni kweli
sasa wakati umefika kwa kisiwa kidogo cha Fundo kujengewa kituo cha Polisi, na
huwenda ikawa suluhisho la kupunguza kasi ya vitendo viouvu,’’alieleza.
Vijana
Hassan Kombo Mwadini na Hashim Ngome Is-haka walisema bado kwa kisiwa chao, hakihitaji ujenzi wa kituo cha Polisi kwa vile hakuna uhalifu wa kutisha.
“Wazazi
wakae pamoja kuwashughulikia wale wachache wanaojihusisha na uvutaji bangi na
wizi, hata kutumia malezi ya pamoja ili kisiwa kiwe salama,’’alieleza.
Mwinjaa
Shavui Masiku ambae anaulemavu wa viungo, amesema uhalifu uliopo unaweza
kudhibitiwa ikiwa kutaimarishwa kwa ulinzi shirikishi.
“Kunaweza
kujengwa kituo cha Polisi lakini kisipewe ushirikiano na uhalifu pengine
ukazidi, jambo linalotakiwa ni wazazi kukutana na kukubali kuwa vijana wao ndio
wakosaji,’’alieleza.
Mkuu wa
wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Hamad alisema kuwa, wakati umefika kujengewa
kituo hicho, ili kuepukana na usumbufu wa kukifuata kisiwa cha Fundo.
Alisema
tayari Kamishna wa Polisi Zanzibar ameshapata taarifa hiyo na kinachosubiriwa ni ruhusa ya kuanza kwa ujenzi huo, hasa kwa vile wananchi wenyewe wako tayari.
‘’Ni kweli
wananchi hao wanaomba kujengewa kituo cha Polisi, na sisi kama wilaya kazi iliyobakia
ni kukumbisha makao makuu ya Polisi, maana hili ni jambo la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania,’’alifafanua.
Hivi karibuni Kamishan wa Jeshi la Polisi Zanzibar Awadh Juma Haji, alinukuliwa na vyombo vya habari, akisema amekiri kupokea ombi hilo na fedha zikipatikana kitajengwa.
Kisiwa cha
Fundo kilichoasisiwa na wavuvi wadago miaka 80 iliyopita, kikiwa na wakaazi
50, sasa kinawakaazi zaidi ya 5000, kipo wilaya ya Wete mkoa wa kaskazini
Pemba, kimepakana na visiwa vya Uvinje na kijiji cha Raha.
Mwisho
Comments
Post a Comment