NA HANIFA SALIM, PEMBA
RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema
kila mwenye uwezo anawajibu wa kutoa sadaka kwa kuwasaidia ambao hawana uwezo
hususani katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Alisema katika mwezi huu mtukufu wafadhili wengi
wamejitoa katika kuwasaidia watu ambao wana hali duni za kimaisha, hivyo
aliwataka wananchi wenye uwezo kujitolea kutoa sadaka kwa wenzao ambao wako
katika mazingira magumu.
Aliyasema hayo kwa nyakati tofauti, katika hafla ya
kukabidhi msaada wa futari kwa wazee, mayatima, wajane na watu wenye ulemavu
kwa Mkoa wa Kusini Pemba, iliyofanyika ofisi ya Mkuu wa wilaya Mkoani na
Tibirinzi Chake chake.
"Ni kweli wanaopata ni wachache na wanaohitaji ni
wengi, lakini hii ni taasisi moja tu zipo na taasisi nyengine ambazo zimesaidia,
ikiwemo kampuni ya Olympic na mashirika mengi yamesaidia kwa Wilaya ya
Micheweni na Wete", alisema.
Dk. Mwinyi alisema, kwa niaba ya serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar amewashukuru watoaji wa sadaka hiyo kutoka nchini Quwait na nchi
nyengine ambazo zilijitokeza kuisaidia Zanzibar.
Aidha, aliwataka ambao wamepatiwa sadaka hiyo kuwaombea
dua wafadhili hao ambao wamejitolea kuwasaidia ili Mwenyezi Mungu awaongezee
kipato kitakachopelekea kuwasaidia tena kwa mara nyengine zaidi.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud
amesifu utaratibu unaofanywa na wenzao wa nchi mbali mbali wa kuwasaidia watu
wenye mahitaji maalum kwa kuwapatia sadaka kila ifikapo mwezi mtukufu wa
Ramadhani.
Alisema, utaratibu huo unaofanyika umekua ukiwafikia
makundi yote yenye hali ngumu ya kimaisha ikiwemo yatima, wazee wasiojiweza, wajane
na watu wenye mahitaji maalumu.
Alisema kuwa, misaada kama hiyo imekua ikijenga mahusiano
mema baina ya Serikali taasisi za watu binafsi na wananchi na serikali yao.
Baadhi ya wanufaika wa msaada huo kutoka Vitongoji Chake
chake Shuwekha Abdalla Saleh alisema, amemshukuru Rais wa Zanzibar Dk. Hussein
Mwinyi kwa kuwapatia msaada huo ambao ni msaada wa mwanzo kwa upande wa mwezi
huu mtukufu wa Ramadhani.
Nae Mohamed Omar Mohamed mwenye ulemavu wa viungo mkaazi
wa Machomane Chake chake alisema, utaratibu huo ni vyema ukawa endelevu, kwa
kila mwaka kwani umekua ukiwasaidia katika maisha yao ya kila siku kutokana na
hali zao duni za kimaisha.
Zaidi ya wananchi 800 wa makundi ya watu wenye ulemavu,
wazee, wajane na mayatima wamepatiwa msaada wa vyakula mbali mbali ikiwemo
unga, sukari, tende na mafuta uliotolewa na Dk. Sughad Al-Swabah na Mubarrak
Al-Swabah kutoka nchini Quwait kupitia kwa Suheil Muzammil.
MWISHO.
Comments
Post a Comment