KHADIJA ALI WA CHIMBA: MNUFAIKA WA TASAF ALIYEJIKUSANYIA SHUNGU YA MIRADI, MBIONI KUJENGA NYUMBA YA KUDUMU
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
KHADIJA Ali Mohamed 45, wa Chimba
Micheweni Pemba, sasa ana mtaji wa zaidi ya shilingi 700,000, anayo matofali
500 na kiwanja, biashara ya mitumba nchini Kenya.
Mpango wake
huo, ni zao la ule mpango wa kunusuru kaya maskini, unaosimamiwa na TASAF tokea
mwaka 2014, ambapo kila baada ya miezi mwili, hujipatia ruzuku kati ya shilingi
30,000 hadi shilingi 44,000.
Ijapokuwa
mlengwa mmoja na mwengine hutofautiana upatikanaji wa ruzuku hiyo, lakini zipo
fedha za msingi (lazima) ambapo kila mlengwa, hupata shilling 20,000.
Anakiri kuwa,
mpango ya kuingizwa kwenye utaratibu wa TASAF, kwake ulikuwa sahihi, kwani hapo
kabla, alikuwa akiishi kiwango cha shilingi 5000 kwa mwezi.
KABLA YA KUINGIA TASAF
Kwake mlo wa
siku, hakuwa na hakika nao, kutokana na kutokuwa na hata njia moja, ya uhakika
ya kujiingizia kipato, licha ya kutegemewa na watoto wake wanne wakati huo.
“Asubuhi
nikiamka, ilikuwa najiuliza kwanza nisuke makuti ya mnazi niuze nipate kiamsha kinywa,
au niende shambani kulima muhogo, jambo hilo lililoniweka roho juu,’’anasimulia.
Kwa wakati
huo, huku akipambana na maisha bila ya mafanikio, alikuwa akiishi kwenye nyumba
ya tope, iliyoezekwa makuti ya mnazi, iliyokuwa na mlango mmoja wa bao moja
lisilo rasmi.
Huduma za
watoto alioachiwa na mume wake, zilikuwa za omba omba tena bila ya mafanikio,
na wakati mwengine kujifungia ndani, pasi na kifungua kinywa.
Suala la
watoto wake kwenda skuli, kutasaka haki ya elimu na madrssa, lilikuwa la
kubahatisha, kutokana na maisha yake kuzungurukwa na changamoto hasa za kipato.
“Ilikuwa
nikihitaji shilingi 1000, kama ninae hitajia shilingi 500,000 hapo ni kusuka
makuti, ili kutatua changamoto zangu na watoto wangu za kimaisha,’’anasimulia.
Anakumba
vyema, wakati anapodaiwa michango ya familia, iwe ya kufiwa, harusi na ugonjwa
na kuieleza familia juu ya kukosa kwake, hakuwa akifahamika juu ya hilo.
Hakuna hata
siku moja, aliyoota ndoto ya kuondokana na hali hiyo ngumu au kuishi kwenye
nyumba ya kisasa, kama walivyo wetu wengine.
Hii ni
kutokana na mipango yake ya kimaisha, hasa ya kutafuta fedha, haikuwa na
mwelekeo, achia mbali mlo wa kila siku ambao ni wa lazima.
BAADA YA TASAF
Kuanzia
mwaka 2014, anasema baada ya kuitwa na kuhojiwa na uongozi wa shehia ya Chimba
wilaya ya Micheweni, hakuamini alichoelezwa.
“Si unajua
kila mmoja atapita, huyu atakuhoji, huyu atakuandika, yule atakupiga picha na
mwengine hadi kuchora ramani ya unapoishi, lakini mwisho wa siku, hakuna
jambo,’’anasema.
Hata kwa
upande wa mpango huo wa kunusuru kaya maskini, rasmi alijenga roho ya tamaa na
furaha, baada ya mara ya kwanza kupokea ruzuku ya shilingi 44,000.
“Fedha hizo,
kwanza niliwanunulia watoto wangu vifaa vyote vya skuli na madrassa, na kisha
saa siku hiyo 7:00 mchana nilipika chakula kizuri na samaki
mnene,’’anahadithia.
Miaka nenda
miaka rudi, Khadija sasa akawa anaendelea kupokea fedha hizo, kati ya shilingi
30,000 hadi shilingi 80,000 wakati mwengine, hutegemeana uwepo wa ajira za
muda.
Baada ya
miezi minane, kuona mpango huo umedumu mikononi mwake, alianza mikakati ya
kuziendeleza fedha hizo, huku moja akipiga hesabu, namna ambavyo ataanzisha
ujenzi wa nyumba ya kisasa.
‘’Hapo baada
ya kuzaa wazo la ujenzi, nikaanza kuzigawa fedha nusu nakula na kuhudumia
watoto, na nyingne nafundika (akiba) pembeni hadi zikatimia shilingi
150,000,’’anasema.
Hapo sasa
aliwaita watoto wake, na hasa baada ya familia kumkubalia ombi la kununua
kiwanja cha ujenzi wa nyumba.
‘’Kiwanja
niliuzia shilingi 300,000 na mimi nikatoa shilingi 150,000 na watoto wangu wakanisaidia
kima kama hicho, na sasa nn ummiliki rasmi,’’anasimulia.
Huku watoto wakienda skuli, bila ya shaka na
kazi zake nyingine aliendelea zao kama vile kilimo, kuuza nazi naususi wa
makuti ya mnazi, wazo sasa likawa ni kuanzisha biashara.
“Nilimshauri
mtoto wangu anaekwenda kwa uvuvi nchini Kenya, aninunulie nguo za mtumba, na
kisha azipeleka huko, maana biashara hiyo inakwenda,’’anasema.
Kwa hatua za
mwanzo, alinunua mitumba ya shilingi 150,000 na baada ya kuuza, alipata faida
ya shilingi 50,000 na kuingia ari mara mbili.
Walishasema
wahenga kuwa, utamu wa sukari huja mwisho, nae sasa baada ya kupata faida hiyo
ya awali, mara ya pili alituma mzigo wa shilingi 250,000.
Kwa awamu ya
pili, biashara haikuwa mzuri, ingawa mlengwa huyo wa kaya maskini, alijipatia
faida ya shilingi 30,000 ambapo mara ya tatu, alituma tena mzigo wa shilingi
300,000.
“Kwa sasa
sipungui wastani wa mtaji wa shilingi 700,000 kama mtaji ambapo naendelea na
biashara yangu hiyo, na tayari pia nimeshanunua matofali 500,’’anaeleza.
Kumbe wakati
huu akiendelea na ujasirimali wake wa nguo za mitumba, akiwa anamilki kiwanja
cha kujenga nyumba na matofali yake 500, pia ni mkulimwa wa mboga.
“Nataka
nyumba yangu iwe na vyumba vinne na vyoo viwili, ili sasa familia yangu na hasa
wajukuu, wapate utulivu zaidi kupitia matunda haya ya TASAF,’’anasema.
Kwenye
kilimo cha mboga, alikojiegesha na wenzake wa mpango wa kunusuru kaya maskini,
hujipatia faida kati ya shilingi 30,000 hadi shilingi 40,000 kwa mwezi hutegemea
na soko lilivyoamka.
Kwenye mfuko
wa ushirika wao wa kuweka na kukopa, mlengwa huyo anatimiza shilingi 350,000
kama mtaji wake binafsi, ambpo wakati mwengine, hukopa na kulipa.
‘’Unajua
TASAF ilitutaka tuhakikisha fedha za ruzuku wanazotupa zisiishie kwenye dishi
pekee, bali tuziekeze ili zizae, na hili nalifanya kwa vitendo,’’anasema.
Kwake yeye
anaamani siku moja TASAF itakapoondoka mikononi mwake, na kwenda kwa wenzake,
awe na jambo la kujisifia kimaisha.
MALENGO YAKE BAABADAE
Moja ni kuwa
na mlango wa wa duku, ambapo hapo sasa anatarajia kuwa na biashara ya nguo,
zisizokuwa za mitumba, na kuhakikisha wajukuu anaowalea, anasomesha hadi chuo
kikuu.
Kwa sasa
mlengwa huyo wa kaya maskini, anaendelea na shughuli zake kama kilimo, ususi wa
makuti akiongeza na ujasriamali wa nguo za maitumba.
SHEHA
Sheha wa
shehia ya Chimba wilaya ya Micheweni Saleh Salim Khamis, anasema shehia yake,
inawananchi 168 waliomo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini, kati ya
wananchi 4,215.
Anacho cha
kujivunia ndani ya shehia yake, ikiwemo walengwa hao kuanzisha vikundi saba vya
ushirika, vyenye wanachama zaidi ya 150.
“Kwenye
shehia yangu, pamoja na mlengwa mmoja mmoja kujiajiri, ipo miradi ya mikubwa,
ambayo wananchi wote wamenufaika nayo,’’anasema.
Hata hivyo
Katibu wa sheha wa shehia hiyo Omar Salim Hamad, anasema TASAF, imeikomboa
shehia yao kwa kuwepo vikundi ambavyo kwa njia ama nyingine, wanachama wake wameshaondokana
na umaskini wa kipato.
‘’Mfano
ushirika wa maskini hajengi, wanaolima mboga na ufugaji wa kuku, lako jicho ni
ushirika wa ufugaji, uwekaji hisa na kilimo cha mboga na kukusanya walengwa
20,’’anasimulia.
TASAF
Mratibu wa
TASAF Pemba Mussa Said, anasema wapo walengwa 14,280 kwa Pemba ambao
wanaendelea kupata fedha za kunusuriwa na umaskini.
Walengwa hao
wapo kwenye shehia 78, ikiwemo za Tumbe Mashariki, Chimba, Makangale, Kiwani,
Ndagoni, Ukunjwi na Fundo.
Ambapo
tayari TASAF Pemba, imestumia shilingi bilioni 14.4 kwa ajili ya kuwapa ruzuku
walengwa hao, fedha za kazi na zile za msingi, pamoja na za masharti.
Tayari kila
shehia, kati ya hizo 78, zimesafikiwa na wastani wa zaidi ya shilingi milioni
230, ambapo kwenye walengwa wote 14,280 wa Pemba, na kila mmoja ameshasaini
shilingi milioni 274.619, ingawa inategemeana na eneo husika.
Mratibu wa
TASAF, alimtolea mfano wa kuigwa mlengwa Khadija wa Chimba, Amina wa Mgogoni na
mwenzake Mfaki kuwa wameyatekeleza kwa vitendo malengo hasa ya mpango huo.
‘’Wenzetu
kama hawa ambao wapo zaidi ya 50,000 kwa Pemba nzima, wamekwenda sambamba hasa na
malengo na mwelekeo wa TASAF, wa kumtoa mwananchi katika unyonge hasa wa
kipato,’’anasema.
Jengine ambalo
ni jema, ni kwa walengwa hao kuanzia mwaka
2014 hadi mwaka 2018 kuibua
miradi ya jamii 146, kwa ajili ya wananchi, kama vile ufufuaji wa mito ya asili
na ujenzi wa daraja ndogo.
‘’Mfano wa
miradi hii hata Makangale upo wa upandaji miti, ujenzi wa matuta ya kuzuilia
maji ya chumvi, mfano Ndagoni, Tumbe na Micheweni,’’anafafanua Mratib wa TASAF
Pemba.
Achia mbali idadi ya watu 50,000 waliojiwekeza
wenyewe, vipo vikundi 942 vikizaa walengwa 12,000 vilivyoanzishwa, kuanzia
mwaka 2014 hadi sasa, ingawa vilivyosajiliwa ni 700.
SERIKALI KUU
Makamu wa
Pili wa rais Zanzibar Hemed Suleiman Abdall, anasema lengo la TASAF ni kuona
mwananchi mmoja mmoja anaondoka kwenye wingu la umaskini hasa wa kipato.
Anasema,
fedha zilizotumiwa na TASAF Pemba pekee wastani wa shilingi bilioni 14.4 lazima
zizae matunda, ili wananchi waweza kuongeza pato lao.
Mwisho
Comments
Post a Comment