NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WATUHUMIWA wengi wa makosa ya ubakaji wa watoto wa kike kisiwani
Pemba huachiwa huru baada ama kesi kumalizikia nje ya mahakama au waliobakwa
kuwatetea mahakamani, imefahamika.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa gazeti hili kwa kufuatilia
mwenendo wa kesi mbali mbali kisiwani humo, umepata ushahidi wa jinsi mabinti
wenye umri chini ya miaka 18 waliopata ujauzito wakiwa shuleni, walivyotoa
ushahidi mahakamani kwamba hawakubakwa bali walikwenda wenyewe kwa waliowabaka.
Mmoja wa watoto waliopewa mimba wakiwa wadogo lakini wakaenda
mahakamani kutoa ushahidi kuwa, hawakubakwa ni Hamida Issa (sio jina lake
halisi), ambaye wakati akipata mimba alikuwa anasoma kidato cha pili katika
skuli ya Sekondari Piki.
“Mahakamani nilisema
sijabakwa nilimfuata mwenyewe, kwa sababu sitaki kesi wala sitaki afungwe, sijabakwa
bali nilimfuata mwenyewe na nimeridhia, sikulazimishwa na ndio maana sikutaka
kutoa ushahidi mahakamani kwa sababu sitaki afungwe,” anasema binti huyo.
Binti huyo mwenye umri wa miaka 16 sasa, alifanyiwa kitendo cha
ubakaji mwaka jana katika kijiji cha Mgoli, Shehia ya Piki Wilaya ya Wete na
alimtaja aliyemfanyia kitendo hicho kuwa ni Nassor Mohamed Juma, mkazi wa
shehia hiyo, ambaye alimlaghai na mwisho wake kumbaka mtoto huyo aliye chini ya
uangalizi wa wazazi wake.
Mtoto huyo anasema, ni kweli alibakwa na kijana huyo na
kumsababishia ujauzito, ingawa alipofika mahakamani alikataa kutoa ushahidi kwa
makusudi ili kuzuia Nassor asifungwe.
Akizungumza na mwandishi kuhusu kwa nini alifanya alivyofanya huko
mahakamani, anasema kwamba hata angetoa ushahidi kijana huyo akafungwa, bado
asingeweza kuondoa ukweli kuwa huyo ndiye baba wa mtoto na angetaka kumwona
mtoto akitoka chuo cha mafunzo (jela).
“Hata angefungwa ni kazi bure kwa sababu ikiwa ni kunibaka, tayari
kashanibaka na mimba kashanipa na nikizaa mtoto atamuona tu akitoka jela, kwa
hiyo sikutaka kesi mimi”, anaeleza binti huyo.
Uchunguzi wa mwandishi umeonyesha kwamba kesi ya Hamida ni moja wapo
tu ya kesi nyingi za namna ambapo watoto katika Wilaya ya Wete wamekataa kutoa
ushahidi na kusababisha kesi hizo kufutwa.
Takwimu za mwaka 2020 za Jeshi la Polisi Wilaya ya Wete zinaonyesha
kesi takribani 85 za watoto kudhalilishewa ziliripotiwa, huku kesi 30
zikiwa ni kesi za ubakaji zinazohusisha watoto wenye umri wa kati ya miaka
15-17.
Kati ya hizo kesi 30, zilizoripotiwa, ni kesi nne (4) tu ambazo
zilitolewa hukumu huku 17 zikfutwa katika kituo cha Polisi, kesi saba (7)
zilifutwa mahakamani na kesi mbili (2) zikiwa katika upelelezi.
Kwa mwaka 2021, takwimu zinaonyesha kwamba kesi zilizoripotiwa
zilikuwa 44, huku kesi 28 zikiwa za watoto wenye umri wa miaka 15-17
ambapo ni kesi nne (4) tu ndizo zilizotolewa hukumu kama mwaka 2020,
huku kesi 12 zikifutwa Polisi na saba (7) mahakamani na kesi tano (5)
upelelezi wake bado unaendelea.
Katika
mazungumzo na gazeti hili, mama wa Hamida, Bi Aisha Ali Hamad (sio jina halisi) mwenye umri wa miaka 45,
anasema alifuata hatua zote mpaka kesi kufika mahakamani, ingawa mwisho wa siku
mwanawe alikanusha kubakwa mbele ya mahakama na kusema kuwa alikwenda mwenyewe.
“Nilijitahidi kumuelekeza na kumuelewesha mwanangu kuhusu kutoa
ushahidi, lakini ilipofika wakati wa kutoa ushahidi alikana mbele ya mahakama,
jambo ambalo liliniumiza sana”, anahadithia mama huyo.
Anasema kwa uzoefu wake, watoto wa kike wenye umri huo ni wagumu
kutoa ushahidi kwa sababu ni kweli wengine wanawafuata wanaume wenyewe huku
wakijua kisheria hawana ridhaa ya kuwa na mahusiano ya kingono na watu wengine.
Mama huyo anaiomba Serikali ifanye utaratibu mwengine wa
kuzishtaki kesi za aina hiyo kwa kuchukua ushahidi wa daktari, kwa vile watoto
wenye umri huo hawana ridhaa ya kushiriki vitendo vya ngono.
“Serikali isiziache kesi hizi eti kwa sababu mtoto amesema
amemfuata mwanaume mwenyewe, mtoto chini ya umri wa miaka 18 kisheria hana
ridhaa, hivyo akitaa mtoto, uchukuliwe ushahidi wa daktari”, anafafanua mama
huyo.
Hata hivyo, mapendekezo hayo ya mama huyo yanaonekana kuwa na
ugumu kwenye utekelezaji kwa vile daktari peke yake anaweza tu kuthibitisha
kuingiliwa kwa mwanamke lakini hawezi kuthibitisha ni nani aliyefanya tukio
hilo.
Kwa mujibu wa Hakimu wa Mahakama Maalumu ya Kushughulikia Kesi za
Udhalilishaji, Ali Abdulrahman Ali, ambaye pia anaifahamu kesi ya Hamida, anasema
itakuwa vigumu kwa Mahakama kuwatia hatiani watuhumiwa kwa kutumia ushahidi wa
daktari pekee.
“Hatuwezi kumtia hatiani mtuhumiwa kwa ushahidi wa daktari pekee
kwa sababu, cheti cha daktari kinaonesha mtoto kutendewa kitendo (ubakaji) na
sio kujulikana mtuhumiwa”, anafafanua.
Anaeleza kuwa, ushahidi wa daktani unafafanua tu na ndio maana
hawautimii pekee kwa kumtia hatiani mshitakiwa, mpaka pale atakapokiri
(kukubali) mtoto kuwa kijana huyo ndiye aliembaka, jambo ambalo kwenye kesi ya
Hamida halikuwezekana.
Anataja kesi za kubaka ambazo zimefikishwa mahakamani kuanzia
mwaka 2020 hadi 2021 ni 49 huku za watoto kati ya umri wa miaka 15-17 zikiwa
19, ambapo nne washtakiwa wamefungwa, mbili wametozwa faini na kesi 13 zimeondolewa
(kufungwa).
Mama Hamida bado anasikitika kuona kwamba mtoto wake amebakwa na
kupewa ujauzito, lakini mwisho wa siku anakanusha mwenyewe ushahidi eti
anampenda, huku akimuacha mtendaji kosa kudunda mitaani.
“Nikimuona kijana huyo roho inaniuma, kwa sababu ameshamuharibu
mwanangu halafu yeye anadunda mtaani, sina raha wala furaha zaidi ya kusemwa na
kuchekwa kwa wanafamilia ya kijana huyo”, anasimulia.
Mratibu wa Dawati la Jinsia Wilaya ya Wete, Hassan Khamis, anasema,
kesi ya mtoto huyo iliwasumbua sana katika kumtafuta na kumfuatilia kijana huyo
ingawa mwisho binti hakuwaunga mkono.
“Mtuhumiwa alikuwa anakimbia, kwa hiyo akionekana sehemu tu, sisi
tunapigiwa simu na tunakwenda hatumkuti, siku moja tulimfukuza mpaka
mabondeni, tulipomkamata tulikuwa taabani sote”, anaelezea.
Kilichowashangaza na kuwahuzunisha ni baada ya kuifikisha kesi
hiyo mahakamani na hatimae mtoto wa kike kusema hakubakwa bali alikwenda
mwenyewe.
Kwa maelezo yake, watoto wenye umri wa miaka 15 hadi 17 wanasumbua
sana katika usimamizi na ufuatiliaji kesi, kwa sababu wanakuwa vigeugeu sana na
wakati mwengine wanakanusha ushahidi.
VIONGOZI WA SERIKALI
Sheha wa Shehia hiyo, Assaa Khamis Mussa, anaeleza kuwa kesi hiyo
anaifahamu na iliripotiwa kituo cha Polisi Wete, ingawa mtoto alipofika
mahakamani alisema, alimfuata mwenyewe kijana huyo na si kwamba alibakwa kama
wazazi wake wanayodai.
“Mtoto aliyefanyiwa kitendo cha ubakaji ndiye shahidi namba moja,
hivyo ikiwa amekataa kutoa ushahidi, Mahakama haiwezi kumtia hatiani
mtuhumiwa”, anaeleza sheha.
Pia Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii Pemba, Omar Mohamed, anasema wamekuwa
wakikosa ushirikiano kwa watoto hao wanapofikishwa mahakamani, huenda kuna
vitisho dhidi yao kutoka kwa wale wanaowabaka au hawatoi ushirikiano kutokana
na kuwalinda wapenzi wao.
“Kwa sababu wanajua kuwa wakitoa ushahidi wa kukiri kutendewa
kitendo hicho na wapenzi wao, kuna uwezekano wa wenzao hao kufungwa jela,
lakini pia wengine wana tatizo tu la kukosa kujiamini na kushindwa kujieleza
mbele za watu”, anafafanua.
Tatizo hilo limesababisha uwepo wa kiasi kidogo cha kesi
zilizoamuliwa, akitoa mfano wa takwimu za Polisi zinazoonyesha kwamba kwa
kipindi cha miaka miwili kati ya mwaka 2020 na 2021 jumla ya kesi 58
ziliripoitiwa zinazohusiha watoto kati ya umri wa miaka 15-17.
Katika miaka hiyo miwili, ni kesi nane tu ambazo washitakiwa
walihukumiwa ukilinganisha na kesi 43 zilizofutwa ama mahakamani au katika
vituo vya Polisi.
WANANCHI
Mkaazi wa Kijiji cha Tundwa kwenye shehia hiyo, Khalfan Juma Ali anaeleza,
aghalabu watoto wenye umri huo mara nyingi hulingana kiumri na wenzao huku
kukiwa na uwezekano pia wa kuwa na uhusiano wa mapema baina yao.
Akitolea mfano kesi ya mtoto Hamida Issa, anasema licha ya wazazi
wake kuwa mstari wa mbele kupigania haki ya mtoto wao, waligonga mwamba baada
ya binti kufika mahakamani na kukanusha kuwa alibakwa.
“Kwa kweli umri huu uliowekwa kisheria ni mkubwa kwa sababu huwa
wanakubaliana na mtuhumiwa, ndio maana wakawa ni wagumu kutoa ushahidi wanapofika
mahakamani”, anaeleza.
Mkaazi wa shehia ya Kiungoni Time Ali Bakari, anasema sababu kubwa
inayosababisha watuhumiwa waachiwe bila kufungwa ni shinikizo la wazazi kwani
baada tu ya kujulikana mtoto amefanyiwa udhalilishaji, wenyewe ndiyo hushawishi
watoto wasifungue kesi.
“Wakisharudi Polisi, wanaambiwa wasitoe ushahidi, ili wasije
kugombana familia au majirani, hivyo kwa hali hiyo mtoto hata umuwekee kisu
shingoni hasemi ukweli”, anaeleza.
Anahadithia kesi iliyotokea kijijini kwao mwaka huu kuwa, baada ya
mtoto kubakwa, wazazi wa pande zote mbili walikubaliana na kukaahidiwa kupewa
milioni mbili, hivyo akaamriwa asitoe ushahidi, jambo lililosababisha kesi
kufutwa.
VIJANA
Kijana Mohamed Suleiman Said (23) mkaazi wa Shehia
ya Kambini anaeleza, sababu ni kwamba wazazi wakishajua kuhusu kesi, wanakubaliana
pande zote mbili kumalizika kesi nje ya Mahakama na hivyo siku ya kuitwa
mahakamani, mtoto anabadilisha ushahidi.
“Pia inaweza kuwa hivyo kwa sababu ya vitisho
kutoka kwa familia ya mvulana au mhusika mwenyewe wa ubakaji, lakini ushahidi
wa mtoto aliyefanyiwa ndio wenye nguvu zaidi, kwa hiyo ikiwa atabadilisha
au atakataa, mtuhumiwa hawezi kutiwa hatiani”, anasema.
Kwa upande wake, Salma Hamad Omar (19), mkazi wa
Mzambarau Takao, anasema kwa maoni yao watoto wenye umri huo kwa sababu hao
wanaume ni wachumba zao, hivyo wanaona shida kusema wamebakwa.
“Wakati mwengine anatishiwa kwa kuambiwa, iwapo
atasema, atamfanyia kitu kibaya ajute katika maisha yake yote, hivyo anajiona
yupo hatarini atakapotoa ushahidi”, anaeleza.
“Pia anajihisi kwamba akitoa ushahidi itakuwaje? Au huyo kijana akifungwa ndiyo itakuwaje? Kwa hiyo anapofikiria hayo huona hakuna haja kutoa ushahidi”, anasema.
Binti mwenye umri wa miaka 17, Maryam Faki Ali,
ambaye pia ni mkaazi wa shehia ya Minungwini anaeleza, ajuavyo yeye, watoto
wenye umri huo hawapendi kutoa ushahidi kwa sababu huwa kuna makubaliano baina
yake na mwanaume.
“Vijana wengi siku hizi hawapendi kuwa ‘single’, kwa hiyo anaweza kukwambia ikiwa unanipenda tufanye mapenzi ili unithibitishie na lazima watafanya, hivyo mwanamke atakapopelekwa mahakamani hatoi ushahidi”, anaeleza.
Anafafanua, mtoto huyo anaona kuwa, akitoa
ushahidi wazazi wake na hata jamii kwa ujumla itajua kwamba hajalazimishwa
kufanya kitendo hicho bali itakuwa amekiridhia mwenyewe na ndio maana
anashindwa kusimama kutoa ushahidi.
WADAU
Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Pemba, Fat-hiya Mussa Said, amemuambia
mwandishi kuwa watoto hao wana changamoto kubwa ya kukataa kutoa ushahidi
mahakamani au kukataa ushahidi ambao wameshautoa vituo vya Polisi kutokana na
kutokujielewa.
“Huku tunakotoka hatujawafundisha watoto masuala
ya kujiamini, kujithamini, kujitathmini, ili waweze kufikia ndoto zao, sasa
wanakwenda kujingiza kwenye mambo mabaya na wanapodhalilishwa wanashindwa
kusimulia haki yao”, anasema.
Anasema, wao wanaona kuwapendelea
waliowadhalilisha itawasaidia kuolewa au labda ni wazazi wanataka kesi ife na
njia wanayoitumia ni kumshawishi mtoto kuharibu ushahidi.
Hafidh Abdi Said Mkurugenzi wa PEGAO Pemba
anasema, watoto wenye umri huo tayari wameshajitambua kwa maana hiyo wanafanya
makusudi kubakwa na ndio maana wanapoteza ushahidi.
“Kwa vile walichokifanya wanajua kuwa ni
makusudi, katika hukumu na wao wawajibishwe kama wanaume, kwa sababu mtoto ambaye
amefanyiwa kitendo hicho bila ridhaa yake hawezi kuficha”, anaeleza Hafidh.
VIONGOZI WA DINI
Kiongozi wa Dini ya Kiislamu kutoka Ofisi ya
Mufti Pemba, Sheikh Mussa Saleh Ali, anasema, watoto wenye umri huo hawatoi
ushahidi wa kweli Polisi au mahakamani kutokana na muhali, vitisho, kurubuniwa
na woga wa kimaumbile kutokana na umri wao.
Mchungaji Zeno Marandu kutoka Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT) Chake Chake amemueleza mwandishi kwamba kesi za
udhalilishaji zimekuwa zikikosa kupata hukumu kutokana na watoto hao kukataa
kutoa ushahidi, kutokujielewa au muhali uliopo ndani ya jamii, kwani asilimia
kubwa ya vitendo hivyo vinatokea ndani ya familia.
MWISHO.
Comments
Post a Comment