NA HANIFA SALIM, PEMBA
WADAU wa kupinga udhalilishaji Kisiwani Pemba wamesema, kukimbizwa kwa watuhumiwa hususani kesi za wanafamilia na kesi ikawa ndio mwisho wake huku jamii ikilalamika kwamba askari wanachangia kuchelewa kufuatilia ni miongoni mwa changamoto walizokumbana nazo wakati wa utendaji wa kazi zao.
Waliyasema hayo katika kikao kazi cha kuwasiliasha ripoti kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Juni mwaka huu kwa kamati za kupinga udhalilishaji Kisiwani humo, kilichofanyika ukumbi wa ofisi ya Chama cha waandishi wa habari wanawake (TAMWA) Mkanjuni Chake chake.
Afisa ustawi wa Wilaya ya Wete Salma Saleh Hamad, akiwasilisha ripoti ya udhalilishaji wa wanawake na watoto kwa kipindi cha miezi sita, alisema kuchelewa kwa kipimo cha DNA na rushwa muhali bado pia ni changamoto kubwa kwa jamii.
Alisema, malalamiko 64 ya matunzo na mvutano wa malezi yaliripotiwa katika kitengo cha ustawi wa jamii, ikiwemo 39 ya matunzi ya watoto na 25 ni mvutano wa malezi, ambapo malalamiko hayo yalipatiwa ufumbuzi na mawili yanaendelea kusikiliza katika ofisi zao za Wilaya.
Akichangia mada katika mkutano huo Makame Kombo Makame kutoka Mahakama ya Mkoa Wete alisema, ili ndoa ziweze kusimama zinahitaji msingi na msingi huo ni wazazi na ofisi ya kaadhi kutoa elimu ya ndoa kwa wanandoa kabla ya kufunga ndoa ili kuepuka udhalilishaji kwa watoto.
Ishaka Sultani Said kutoka TUJIPE alisema, katika utendaji wa kazi zao walibaini kwamba uwelewa mdogo kwa masuala ya udhalilishaji kwa jamii ya Wilaya ya Micheweni ni mdogo hivyo elimu inahitajika kwao.
"Jamii bado haijakubali kujitoa katika kuondosha udhalilishaji licha ya viongozi wa Wilaya na Mkoa wa Kaskazini kuwa tayari kupambana kwenye masuala haya lakini bado jamii haijawa na uthubutu", alisema.
Mwendesha mashitaka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka DPP Mussa Khamis akiwasilisha ripoti ya ofisi hiyo Mkoa wa Kusini alisema, wamepokea majalada ya kesi za udhalilishaji 66 ambapo kati ya hayo 37 yalifunguliwa mahakamani.
Nae Abdalla Issa Abdalla kutoka chuo cha mafunzo Pemba alisema, kuanzia mwezi Januari hadi Juni wamepokea wanafunzi sita, huku wakiwa na watuhumiwa 37 ambao bado mashauri yao yanaendelea na upelekezi.
Mapema, akifungua mkutano huo kwa niaba ya Katibu tawala Wilaya ya Mkoani Muumini Abeid alisema, uwepo wa kamati hizo unalenga dhana ya kulinusuru taifa kwani, udhalilishaji ni janga ambalo lipo na linaendelea kuitia dosari nchi yao.
"Mashirikiano ni jambo muhimu katika kutokomeza janga hili la udhalilishaji wa wanawake na watoto, lazima jamii tuwe tayari kila mmoja kwa nafasi yake aoneshe utayari wa kupambana na hili naamini hapo tutafanikiwa kupunguza matendo haya", alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa Tamwa Pemba Fat-hiya Mussa Said alisema, wadau hao kazi yao kubwa ni kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na masuala mbali mbali ya udhalilishaji, kuibua kesi katika jamii pamoja na kutoa msaada wa kisheria na kisaikolojia kwa hatua za mwanzo wakati yanapotokea matukio ya udhalilishaji.
"Tunawasaidia wahanga wanapotokewa na matukio ili waweze kuziripoti kesi na kuwapa moyo wakati wanapofanya ufuatiliaji wa kesi hizo kwa kwenda nao mahakamani, kituo cha mkono kwa mkono na wanapovunjika moyo sisi tunakwenda kuwatia ari, ili kwa pamoja haya mapambano yaweze kufanikiwa", alisema.
Hata hivyo alisema, watuhumiwa wengi ambao wanaripotiwa na kesi za udhalilishaji hutoroka hivyo, alivishauri vyombo vya sheria kuhakikisha wanawarudisha watuhumiwa pamoja na kuwadhibiti ili wasikimbie baada ya kufanya kosa.
MWISHO.
Comments
Post a Comment