Zawadi: mwakilishi wa Konde anaepambania kuzitatua changamoto za wananchi ‘Asema, watu wayasemee mazuri anayoyatekeleza sio kumbeza’
NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@ "NIMECHIMBA visima nane katika Jimbo langu, visima sita ni vipya na viwili vilikuwepo zamani lakini vilikuwa havitumiki tena kutokana na uchakavu," si maneno ya mtu mwengine bali ni ya mwakilishi wa Jimbo la Konde Zawadi Amour Nassor. Zawadi ni mwanamke anaepambania kuzimaliza changamoto ndani ya jimbo lake ambazo zilikuwa zikimkosesha usingizi kabla ya kuwa kiongozi. Mama huo wa makamo anaendelea kutimiza malengo yake aliyojiwekea baada ya kuingia kwenye chombo cha kutoa maamuzi, ambayo ni ndoto yake ya muda mrefu. Katika kipindi hiki cha muda mfupi cha uongozi wake, amefanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa visima, hali ambayo imewapunguzia usumbufu wananchi hasa wanawake na watoto ambao ndio wahanga wakubwa. Mwakilishi huyo anasema, upatikanaji wa maji katika jimbo lake ulikuwa ni wa kusuasua kiasi ambacho watu hutumia muda mrefu kutafuta huduma hiyo na kushindwa kufanya shughuli nyengine za maendeleo. ...