NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANAHARAKATI wa haki za watoto shehia ya Mfikiwa
wilaya ya Chake chake, wamesema tamaa ya mahari na haki ya wazee (kilemba cha
wazee), ni miongoni mwa sababu, zinazochangia watoto kukatishwa masomo kwa
kuozwa waume mapema.
Walisema, baadhi ya wazazi wamekuwa wakikimbilia haki ya wazee
na mahari, wakati mtoto wake anapotokezea muume, na hivyo kumkatisha masomo kwa
tamaa hiyo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo,
walisema hiyo ni miongoni mwa sababu moja kubwa, ambayo sasa husababisha watoto,
kukatishwa masomo.
Mratibu wa wanawake na watoto shehiani humo Kheriyangu Mohamed
Ali, alisema pamoja na elimu wanayoitoa, lakini bado wapo wazazi wamekuwa
wazito kubadilika.
Alieleza kuwa, na hasa pale inapotokezea kuna mtoto ni
mtoro masomoni, ndipo hapo wazazi huchukua nafasi hiyo, kuwakatisha masomo.
‘’Hapa shehiani, wapo wazazi na walezi wamekuwa
wakivutiwa mno na yale mahari na fedha za wazazi (kilemba cha wazee), hivyo
huwa rahisi kuwaoza watoto wao,’’alieleza.
Kwa upande wake mazazi Masika Mohamed Ali, alikiri kuwepo
kwa tamaa hiyo kwa baadhi ya wazazi, bila ya kujali athari yake, hapo baadae.
‘’Watoto wa kike hapa kijijini waliowengi wamekuwa wakivunjiwa
ndoto zao, maana huolewa mapema na moja ya sababu ni utoro na wazazi kupenda fedha
za mahari,’’alieleza.
Nae Mkubwa Ali Khatib alishauri jamii, kutowakatisha masomo
watoto wao wa kike, na wawaache waendelee kutimiza ndoto zao za kielimu.
Sheha wa Mfikiwa Bimkubwa Rajab Tangwi, alisema wamekuwa
wakali mno, pale wanapohisi kunaharakati za kufungwa ndoa ya mtoto shehiani
mwake.
Alieleza kuwa, wamekuwa wakijitahidi kutoa elimu kwa
jamii, ingawa wamekuwa wajanja na wakati mwingine kuzifungisha ndoa hizo nje ya
shehia ya Mfikiwa.
‘’Ni kweli tamaa ya mahari imekuwa ikisababisha watoto
wengine kukosa kuendelea na masomo, maana wazazi wingine hukimbia aibu ya mimba
kabla ya ndoa,’’alifafanua.
Mratibu wa TAMWA-Pemba Fat-ya Mussa Said, alisema lazima
jamii iweke mkazo wa kipekee, ili kuhakikisha watoto wa kike wanamaliza masomo
ya lazima.
Kwa upande wake Mratibu wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria
wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, alisema moja ya changamoto iliyopo
ni wazazi kutohudhuria mikutano ya wazi na kujifunza.
‘’Kupitia mikutano ya wazi, huelezwa athari za mtoto
kumkatisha masomo na kisha kumuoza, akiwa bado viungo vyake havijakomaa, lakini
hawahudhurii,’’alieleza.
Akizungumza hivi karibuni, Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba Mattar
Zahor Massoud, aliwatahadharisha masheha kutosogelea vikao vya sulhu, kwa kesi
za udhalilishaji.
Matukio ya ubakaji na
ulawiti yanayowakumba wanawake na watoto kwa miezi ya February na Machi mwaka 2023/2024
yaonekana kupungua na kufikia 300, upungufu wa matukio 24 kwa mwaka jana.
Kulingana na takwimu zilizoripotiwa kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa serikali,
inaonesha miezi hiyo Febuari na Machi mwaka uliopita, zinaonesha kuwa ndani ya
siku 59 ya miezi hiyo miwili, kumeripotiwa matukio sita, kwa kila siku moja.
Taarifa zinaeleza matukio ni 624, yaliyoripotiwa kwa miezi minne kwa
Zanzibar, na kuonesha wastani wa matukio 56 kuripotiwa kila wilaya, kati ya 11 za
hapa Zanzibar.
Mwisho
Comments
Post a Comment