NA NAFDA HINDI, ZANZIBAR
Ni takriban miaka 20 sasa, shauku ya waandishi wa habari
pamoja na watetezi wengine wa haki za binaadamu Zanzibar kuona nchi yao inapata
sheria rafiki za habari imekuwa ikitimizwa kwa maneno. Viongozi wa ngazi
mbalimbali serikalini wamekuwa wakitoa ahadi lakini utekelezaji wake unasuasua.
Tangu alipoingia madarakani, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekuwa akionesha kutambua
umuhimu wa sekta ya habari kusimamiwa kwa kutumia sheria zilizo rafiki, kwa
vile si mkosefu wa kujua ukweli kuwa sheria zilizopo ni kongwe zisizoendana na
mazingira mapya yanayochagizwa na kasi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia.
Akiwa amekalia kiti cha Ikulu baada ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2020, Dk. Mwinyi hakuchukua muda kusikika akitoa matamshi yenye mtizamo
wa kupendelea waandishi wawe na uhuru zaidi wa kufanya kazi zao, kwa kuamini
kuwa itarahisisha manufaa ya utendaji wao kuwafikia wananchi kwa ukamilifu.
Mara baada ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) kutoa ripoti
ya utendajikazi wa vyombo vya habari, mwaka 2021/2022, ikieleza kuwa Zanzibar
inahitaji sheria “mpya kabisa” za kusimamia sekta ya habari, Serikali ilijikuta
inakumbushwa jukumu au wajibu wa kufanyia kazi suala hilo kwa kuwa limepigiwa
kelele muda mrefu. Harakati za waandishi na wadau kutaka mageuzi ya sheria
zilianza mwaka 2002.
Ni hapo, Rais Dk. Mwinyi alipojibu kutambua “sheria za
habari za Zanzibar ni za muda mrefu na Serikali anayoiongoza ipo tayari
kushirikiana na wadau wa habari, kuzifanyia kazi kulingana na mapendekezo
yatakayotolewa.” Alisema, “pendekezo lenu la kwamba Zanzibar imefika wakati wa
kupata sheria nzuri, tutalifanyia kazi.”
Ilipofika mwaka 2023, kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku
ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Mei 3, Rais Mwinyi aliiambia hadhara kwamba
serikali yake itaendelea kuheshimu na kuthamini haki ya uhuru wa habari na
kujieleza. Maadhimisho yalifanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip
Uwanja wa Ndege.
“Serikali zote mbili zitaendelea kushirikiana kwa karibu na
vyombo vyote vya habari katika kuhakikisha serikali inatatua changamoto
zinazowakabili wanahabari,” alisisitiza.
Mbele ya Rais, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa
Zanzibar, Tabia Maulid Mwita, akikazia muelekeo wa Rais, alisema mchakato wa
sheria ya habari Zanzibar umefikia asilimia 80 kukamilika na akasihi wadau wa
habari kuendelea kuwa na subira.
“Serikali yenu ni sikivu, tunawahakikishia kuwa na sheria
nzuri zitakazokidhi matakwa ya sasa, tutawasilisha Baraza la Wawakilishi na
taratibu nyingine ziendelee,” Waziri Tabia alisema.
Kuonesha kuwa serikali inakumbuka kilio cha waandishi wa
habari kutaka sheria rafiki za kusimamia sekta ya habari, na kwamba haijasahau
wajibu wake wa kuona hilo limetimia, serikali ilirudia msimamo wake wakati wa
maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani Mei mwaka huu.
Katika maadhimisho yaliyoandaliwa na kuratibiwa na serikali
kupitia Wizara ya Habari, tarehe 4 Mei, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Fatma Rajab
akimwakilisha Waziri Tabia, alisema “Serikali itahakikisha mageuzi ya sera na
sheria za habari nchini yanaenda sambamba na kanuni pamoja na maadili ya vyombo
vya habari.”
Kauli hiyo ilizingatia kauli mbiu ya kitaifa ya wadau wa
habari Zanzibar ya mwaka huu 2024, iliyosema: Uhuru wa Vyombo vya Habari.
Mageuzi ya Sera na Sheria za Habari Zanzibar.”
Kaulimbiu hii ilitiliwa mkazo na mantiki yake kufafanuliwa
vizuri Mei 23 mwaka huu wakati wa wadau wa taasisi za habari na washirika wao katika
utetezi wa haki za binaadamu, lilipoalika watu mbalimbali kwenye maadhimisho
waliyoandaa na kukaribisha Katibu Mkuu, Fatma kuwa mgeni rasmi. Alimtuma Katibu
Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Suleiman Abdalla ambaye alisema:
“Kwa sasa sheria ya habari, ipo kwa Mwanasheria Mkuu wa
serikali na tunatarajia hivi karibuni itapelekwa Baraza la Wawakilishi kama
muswada na tunaomba walioko huko waichangie vizuri ili iweze kupita na
kupatikana sheria mpya.”
Ni kwanini waandishi wa habari watoe kilio chao cha kutaka
mageuzi ya sheria za habari? Analo jibu Dk. Mzuri Issa, Mkurugenzi wa Chama cha
Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA-ZANZIBAR). “Haiwezekani kuwa na sheria za
udhibiti mpaka sasa, ukitaka kufanya usajili wa gazeti lazima Waziri aamue,
asipotaka huwezi (kusajili). Katika mazingira haya hatuwezi kwenda kwa wakati
huu tunapozungumza utawala wa demokrasia.”
Utambuzi wa uhuru wa vyombo vya habari, unaanzia Umoja wa
Mataifa ambako mwaka 1948 Baraza lake la Usalama lilipitisha azimio lililojenga
msingi wa imani kwamba ni muhimu haki na uhuru wa vyombo vya habari ikijumuisha
uhuru wa kupata habari na ule wa watu kujieleza, ukaheshimiwa na kulindwa. Ibara
ya 19 ya tamko hilo la kilimwengu inaelekeza hivyo.
Kiutaratibu, baada ya azimio hilo, kilichofuata ni kwa kila
nchi mwanachama wa umoja wa mataifa, kuridhia kwa kusaini azimio; na kupitia
bunge lake, itunge sheria ya kutambua mantiki na kujipa dhima ya kusimamia
utekelezaji wa azimio kulingana na mazingira iliyoko.
Zanzibar baada ya kuungana na Tanganyika, maslahi yake
katika suala hilo yakabebwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo iliridhia
azimio na kupaswa kutunga sheria ya kuchukua dhima ya kulitekeleza. Zanzibar
ilikuja kutambua rasmi haki na uhuru wa habari ilipoandika katiba yake ya pili mwaka
1984 baada ya kufutwa kwa Katiba ya Kwanza ya mwaka 1963 na kuweka dhima katika
Ibara ya 18.
Miaka minne baadaye, yaani mwaka 1988, ilitunga sheria ya kwanza
iliyoiita Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Na. 5 ya
mwaka 1988. Ikapata marekebisho ya kwanza kupitia Sheria Na. 8 ya mwaka 1997. Sheria
nyingine maarufu ni iliyohusu utangazaji ambayo ni Sheria ya Tume ya Utangazaji
Zanzibar Na. 7 (1997), na yenyewe ikiwa imerekebishwa kwa Sheria Na. 1 (2010).
Ni msimamo wa waandishi na taasisi za kibahari kwamba sheria
hizi haziendani na mazingira ya sasa. Ni kongwe zinazopingana na dhamira na
dhima ya kuheshimu na kulinda haki na uhuru wa habari. Sheria hizi zinatajwa
kuzorotesha wananchi kufaidika na uhuru unaokusudiwa na umoja wa Mataifa.
Kwa mfano, kifungu cha 27(2) cha Sheria ya Usajili wa Wakala
wa Habari, Magazeti na Vitabu Na. 5 (1988) iliyorekebishwa kwa Sheria Na. 8
(1997), kinasema: “Hakimu yeyote anaweza kutoa hati kumuidhinisha Afisa wa Polisi
yeyote, wa cheo cha Inspekta kwa msaada au bila msaada, kuingia na kupekuwa
mahali popote pale inaposhukiwa kuwa kuna gazeti linachapishwa kinyume na
sheria hii, au kanuni zozote zililotungwa, ama limefanya au linafanya au
linakaribia kufanya kosa, hivyo anaweza kukamata gazeti lolote linalopatikana
humo ama kwa kushuku kuwa kuna gazeti lililochapishwa au linachapishwa pamoja
na ushahidi mwengine wowote kwa kutenda kosa chini ya sheria hii, au kanuni
zozote zilizopo zitakazopatikana”.
Kwa muktadha huo, kifungu cha maneno yaliyotumika yana utata
ndani yake. Hayaeleweki sawasawa kwa sababu kimekusanya maneno mengi na tata yasiyofahamika,
na dhana ya kushuku tu inamruhusu Polisi kuingia kwenye ofisi ya gazeti,
kupekuwa, na akijiridhisha tu na shuku yake, anaweza kukamata au kuzuia gazeti
husika kuchapishwa.
Ni imani ya waandishi
wa habari na watetezi wa haki za binaadam kuwa uandishi wa habari, ni fani kama zilivyo udaktari, uhandisi, uuguzi,
uanasheria na ualimu, ni kazi ya kitaaluma. Je ofisa wa polisi anaijua taaluma
inavyoelekeza? Je, dunia ingali kwenye wakati wa kuendesha mambo kwa kushuku?
Hawra Shamte, mwandishi mwandamizi nchini, akigusia ubaya wa
kifungu hicho, anasema: “Kinampa mamlaka Hakimu atowe kibali kwa Inspekta wa
polisi kupekuwa jengo kwa kushuku tu ikiwa sehemu hiyo inachapishwa gazeti
linalokwenda kinyume na taratibu labda za maadili ya nchi, mila na desturi au
kuhatarisha amani na utulivu.”
“Hichi kifungu hakiko sawa na kina dalili za ukandamizaji wa
uhuru wa habari kwa sababu hatwendi kwa dhana na shuku. Tunashauri kirekebishwe
kwa maslahi ya nchi na wananchi,” anasema. Pia anatanabahisha kuwa sheria
yenyewe haikueleza maana ya “maadili ya nchi, mila na desturi au kuhatarisha amani
na utulivu.”
Malalamiko pia yanaihusu Sheria ya Tume ya Utangazaji
Zanzibar Na. 7 (1997), na marekebisho yake kupitia Sheria Na. 1 (2010), kwamba
inawapa viongozi wa serikali mwanya wa li kuingilia shughuli za utangazaji ambazo
kimantiki ya azimio la Umoja wa Mataifa, zinapaswa kufanywa kwa uhuru mpana.
Mwandishi mwandamizi wa habari nchini, Jabir Idrissa,
anasema: “Sheria hii inaipa nguvu Tume ya Utangazaji, kufungia na kufutia
leseni vyombo vya utangazaji, hivyo kwenda kinyume na viwango vya kimataifa
vinavyoitaka tume kuwa huru na inayojitegemea.”
Mwanasheria na Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU), Said
Ali, anasema Sheria ya Tume ya Utangazaji, inatoa mamlaka makubwa kwa viongozi
serikalini kuchukuwa maamuzi yoyote anayoona yanafaa kwa kisingizio cha amani
na utulivu ingawa haikufafanuliwa tafsiri yake rasmi kwenye sheria.
“Kifungu 27(2), Waziri amepewa mamlaka makubwa ya kuchukua
maamuzi yoyote, mfano kama ana tofauti binafsi na mtu fulani ambae ni mmiliki
wa chombo cha habari, anaweza akaitumia sheria hii vibaya na kumtia hatiani mtu
huyo kwa kufungia chombo hicho cha habari."
Uzoefu unaonesha kuwa kiongozi anaweza kuamka na matatizo
yake binafsi na kwa kuwa anayo mamlaka ya kisheria, akayatumia hayo vibaya kwa kutoa
amri dhidi ya ustawi wa uhuru wa habari, akasababisha chombo kufungwa na hivyo
kukwamisha manufaa yanayotarajiwa na umma.
Najjat Omar ni mwandishi wa habari ambaye anahofia kuendelea
kwa Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar, kutasababisha waandishi kutofanya
kazi kwa uhuru na weledi kwa vile wanagubikwa na woga. Kwa hapo, watashindwa
kutimiza wajibu wa kuishauri serikali kuhusu kudhibiti watumishi wake wanaozuia
taarifa muhimu kwa kisingizio cha kulinda maslahi ya usalama wa taifa, ambayo
hayajafafanuliwa katika sheria.
“Hatutoweza kuwawajibisha wanaokula fedha za umma tofauti na
matarajio ya serikali, muhusika anaweza kusema mradi huu umetumia shilingi milioni
mia moja kumbe tathmini inaonesha matumizi sahihi ni shilingi milioni 20. Mwandishi
akikaa kimya kufumbia uovu huo, na mtumishi mwengine atapiga milioni mia
mbili,” anasema Najjat.
Mwanasheria Shadida Omar kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki
za Binaadamu Tanzania (THRDC), anasema ili kuona uhuru wa kujieleza unafanikiwa
kwa manufaa ya jamii, waandishi wanadhima ya kupaza sauti kwa kupata sheria
mpya ya habari inayokwenda na mabadiliko ya dunia ya sasa.
“Hapa kwetu Zanzibar zipo sheria nyingi zinabadilishwa mara
kwa mara na katika muda mfupi, inashangaza hizi sheria zinazohusu sekta ya
habari zinacheleweshwa wakati inajulikana wazi kuwa ni za zamani zinazokwaza
uhuru wa habari,” anahoji.
Mwanasheria huyo anaitaja mojawapo kuwa ni Sheria ya
Uchaguzi Zanzibar, Na. 11 ya mwaka 1984 ambayo imerekebishwa kupitia Sheria Na.
4 ya mwaka 2017. Sasa inaitwa Sheria ya kufuta Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya
mwaka 1984 na kutunga Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2017 na masuala mengine
yanayohusiana nayo. Sheria hii mpya ilisainiwa na Januari 16, 2018.
Mshauri Elekezi na Mwalimu wa Uandishi wa Habari Tanzania na
Afrika Mashariki, Salim Said Salim anasema demokrasia sahihi hutegemea “sana”
uhuru wa vyombo vya habari katika nchi, kwa sababu vyombo vya habari vina dhima
ya kuchangia maendeleo ya nchi kwa kupaza sauti na kuwawajibisha viongozi
wanaotumia mamlaka kinyume cha sheria.
“Hii Sheria ya Habari ina miaka takriban 20 sasa tokea kuanza
kuilalamikia, tunapewa ahadi kila siku lakini bado hatujaona utekelezaji wake.
Kama ni mtoto tayari angekuwa anasoma chuo kikuu,” anasema veterani aliyeanza
kuwa mwandishi wa habari mwaka 1965.
Mwenyekiti wa Kamati ya Habari Zanzibar (ZAMECO) ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Abdalla Mfaume anasema
jitihada zinahitajika kwa waandishi kuendelea kudai sheria mpya ya habari
itakayotoa fursa kwa wote kupata haki bila ya ubaguzi na kuleta maendeleo
katika nchi.
Mfaume anaimarisha hoja ya Dk. Mzuri anayeamini kampeni ya
kupigania sheria mpya za habari lazima iendelee. Anasema, “Tumewahi kuzungumza
na Mhe. Rais kuhusu sheria hizi, na Waziri (wa Habari) pia, nadhani inabidi
tupange kuzungumza nao tena ili tuone hili linakwendaje. Haitapendeza hata
kidogo kumaliza mwaka huu (2024) hatujapata mabadiliko ya sheria za habari.”
Msimamo huu aliutoa katika tamati ya maadhimisho ya Mei 23
baada ya kusikiliza kauli za viongozi wa serikali kuwa mara mapendekezo yapo
kwa kamati ya makatibu wakuu, mara kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mara imerejeshwa
kwa mwanasheria ili kutafsiriwa kwa Kiswahili.”
MWISHO.
Comments
Post a Comment