NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
WANAKISOMO cha madarasa ya Elimu ya watu wazima kisiwani Pemba wameiomba Wizara pamoja na wafadhili kuwasaidia miwani, ili waepukane na usumbufu wakati wa kusoma na kuandika.
Walisema kuwa, madarasa hayo ambayo kwa asilimia kubwa ni wanafunzi watu wazima, wakati mwengine wanashindwa kusoma wala kuandika kutokana na kupungua kwa nuru ya macho.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi katika vijiji tofauti, ikiwemo Mjinikiuyu shehia ya Minungwini Wilaya ya Wete,wanakisomo hao walisema wana shauku ya kujifunza zaidi ingawa wakati mwengine inawapa wakati mgumu kuhudhuria darasa.
Walisema kuwa, kuna haja kwa Wizara ya Elimu pamoja na wafadhili wengine kuwasaidia kwa kuwapatia miwani, ili wahudhurie darasani wakiwa na hamasa ya kusoma na kuandika kwa bidii.
Mmoja wa wanafunzi hao Viwe Yusuf Malik mwenye miaka 70 alieleza kuwa, anahudhuria darasa siku zote walizopangiwa lakini inapofika wakati wa kuandika ama anapoambiwa asome kwenye ubao macho yanamsumbua sana.
"Kusoma nimeshajua vizuri kiasi lakini shida yangu ni kuwa na uoni hafifu, hii inaniumiza sana kwa sababu mwalimu anapoandika ubaoni nataka nisome ili nipate uzoefu zaidi, ingawa nashindwa," alisema bibi huyo.
Kwa upande wake mama wa miaka 65 ambae hakutaka jina lake litajwe alieleza kuwa, walipoanza mwanzo kusoma walikuwa wanaona vizuri, ingawa kila umri unapokwenda mbele na wao wanapungua nuru ya macho, hivyo wanahitaji kusaidiwa.
"Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na taasisi nyengine ikiwemo TAMWA na PEGAO zinajitahidi kutusaidia vifaa vya kuandikia na kujifunzia lakini hii miwani bado hatujapatiwa na tuna uhitaji mkubwa," alieleza.
Mwanakisomo Aisha Omar Issa mwenye umri wa miaka 35 alieleza, wamekuwa wakitumia jituhada za ziada kwa kusoma na kuwataka wazee hao waitikie ili wajisikie vizuri katika darasa hilo, hivyo ipo haja ya kupewa miwani kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kusoma na kuandika mara kwa mara.
Mwalimu wa darasa hilo Maryam Juma Hamad alisema, katika darasa lake la wanafunzi 42 kuna vijana na wazee ambao kwa sasa wana uoni hafifu unaohitaji kisaidizi cha miwani.
"Ni miaka minne tangu tuanze darasa hili la watu wazima na wanafunzi wangu wa bidii sana ya kusoma na kuandika, hivyo naomba wasaidiwe miwani," alisema.
Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said alisema, wakati wanahamasisha wanajamii umuhimu wa mwanawake kuwa kiongozi waligundua kuwa, wengi wanashindwa kutokana na kutokujua kusoma na kuandika na ndio maana wakaamua kuanzisha madarasa hayo kwa ajili ya kuwasaidia.
Nae Mratibu wa mradi wa SWIL Pemba Dina Juma Makota alisema, ukosefu wa miwani kwa wanakisomo cha watu wazima ni changamoto kubwa ambayo bado haijapatiwa ufumbuzi, hivyo watafanya juhudi za makusudi kuhakikisha inapatikana.
Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim alisema, wamekuwa wakiwahamasisha wanafunzi hao kuwa pale Serikali inapopata wataalamu wa kambi za macho wafike haraka ili wapimwe na kupata huduma ya miwani kwani Wizara ya Afya kila baada ya kipindi fulani hutoa huduma hiyo na bila ya malipo.
"Haya madarasa mengi yapo vijijini na hizi kambi mara nyingi huwepo mjini kwa hiyo baadhi ya wananchi hukosa taarifa jambo ambalo ni changamoto, lakini tunatumia madarasa hayo kuhamasisha na kuwapa taarifa ya ujio wa madaktari bingwa wanaokuja ili kupima na kupewa huduma ya miwani," alifafanua.
Mdhamini huyo aliwataka wanakisomo hao licha ya changamoto hiyo waliyonayo, waendelee kujifunza kwa moyo mkunjufu ili kujinufaisha na kuwasaidia watoto wao kupata elimu bora kwa maisha yao ya baadae.
MWISHO.
Comments
Post a Comment