NA HAJI NASSOR, PEMBA
KIKUNDI cha ‘Kheri liwe’ kilichopo Likoni shehia ya Kengeja wilaya ya Mkoani
Pemba, kimesema mafunzo, mawazo na fikra walizopewa na TAMWA-Zanzibar, sasa
zimezaa matunda baada ya kujipatia zaidi ya shilingi milioni 2.8 ikiwa ni faida
kwa miaka mitatu iliyopita.
Wanakikundi
hao, walisema baada ya kuanzisha mpango wa kuweka fedha na kukopa ‘hisa’ ambao walishawishiwa na TAMWA, na
kufanya biashara ndogo ndogo, utengenezaji sabuni na kilimo cha mboga, sasa
wameona matunda yake.
Wakizunguma na
mwandishi wa habari hizi kijijini hapo, wanakikundi hao, walisema kumbe
walichelewa kujikusanya na kama wengeanza miaka ya nyuma zaidi, kwa sasa
wengeshapiga hatua kubwa zaidi.
Walieleza kumbe
zipo fursa kadhaa endapo jamii itazifanyiakazi kupitia vikundi hivyo, na kisha
kuwezeshwa kimafunzo na fikra za jinsi ya kukusanya fedha na kisha kujikopesha
wenyewe.
Mwenyekiti wa
kikundi hicho Fatma Nahoza Juma, alisema sasa kila mwanachama ameshapata faida,
iwe wakati wanapogawana faida au kukopa fedha anapokuwa na shida.
“Kikundi
hichi tulikianzisha kama utani, wakaja watendaji wa TAMWA Pemba, wakataka
tujiwekee akiba na huku tutafute biashara ambayo wanunuzi ni sisi wenyewe
tulifanya hivyo, na sasa tuko vizuri,’’alieleza.
Aidha
Mwenyekiti huyo alisema waliendesha biashara ya bidhaa ya sukari, na hapo
walilazimishana kuikopa wanakikundi na kujiingizia faida.
Aliongeza
kuwa, pia wanapolima kama mchicha, bilingani na tungule wateja wa kwanza ni
wao, na kupata faida ambayo sasa wanajivunia kupitia kikundi chao.
Mshika fedha
wa kikundi hicho cha ‘Kheri liwe’ Maimuna
Ngwali Ali, alisema paketi moja ya kilo 50 ya sukari walikuwa wananunua kwa
shilingi 72,000/= pamoja na gharama za usafiri na kisha wanajipatia faida ya
shilingi kati ya 25,000/= hadi shilingi 30,000/=.
Alisema
wamekuwa wakifanya hivyo kwa miaka miwili sasa ambapo hujipatia faidi ya shilingi
360,000/= kwa mwaka na kwa miaka miwili pekee wameshavuna faida ya shilingi
720,000/= kwenye bidhaa ya sukari.
“Utaratibu
wetu katika kuhakikisha tunaingiza faida, basi lazima kila mwanachama wetu anunue
bidhaa ama atupe faida ambayo tumepanga tuiingize, mfano kila kilo moja ya sukuri,
ipo faidi ya shilingi 500/=,’’anafafanua.
Kwa upande
wa kilimo cha mboga, ambacho nacho walishauriwa na TAMWA Pemba, wameshajipatia
wastani wa shilingi 180,000/= ndani ya miezi sita.
“Kilimo cha mboga nacho, tunakiendesha na mavuno ya
kwanza tulipata shilingi 50,000/= mavuno ya pili 130,00/= na sasa baada ya
kuvuna tunatarajia kujipatia wastani wa shilingi 300,000/=,’’alifafanua.
Mshika fedha
huyo, ameipongeza TAMWA kwa mpango wao ambao unaelekea kupunguza umaskini,
pindi wanaoelekezwa wako tayari kujiletea maendeleo.
Mwanachama
wa kikundi hicho, Khalfan Salim Khalfan na mwenzake Rukia Vuai Khamis walisema,
vikundi hivyo ni vizuri maana vinatoa heshima ya mwanamke katika jamii.
“Heshima ya
mtu ni kazi, ndio maana TAMWA imetupa heshima kwa kutupa mafunzo ya kilimo,
sabuni na uwekaji hisa, sasa hatuna wasiwasi,’’alieleza Rukia.
Kwa upande
wake, Katibu wa kikundi hicho cha kheri liwe cha Kengeja, Mwajuma
Shaban Khamis, alisema sasa wanaangalia kubuni mradi mwengine, wa ufugaji kwa
siku zijazo.
Aidha Katibu
huyo, aliwataka wafadhili wengine kujitokeza ili kuwawezesha katika ziara za
kimafunzo, kwa vikundi vilivyopiga hatua zaidi, ili wazidi kunufaika macho.
“Kwa maendeleo
tuliyonayo, lazima tuwapongeze wenzetu wa TAMWA kwa ushauri, elimu, maelekezo
na fikra zao na sasa tunajivunia,’’alieleza.
Ofisa
Uwezeshaji wa TAMWA- Pemba Asha Mussa Omar, alisema huo ni mpango maalum,
ulioandaliwa kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Alisema, ni
kweli vipo vikundi kadhaa kisiwani Pemba ambavyo wamekuwa wakiviwezesha, lakini
baadhi yao vimekuwa havifanyi vizuri kwa kutokuwa tayari.
“Vikundi
vyengine kama kilichopo Mkanyageni, Mavungwa, Mbuzini, Chake chake na hicho cha
Kengeja vimekuwa vikijiongeza na kubuni miradi ambayo huzaa tija,’’alifafanua.
Kikundi
hicho cha ‘kheri liwe’ cha Kengeja wilaya ya Mkoani ambacho kinajishughulisha
na kuweka wa hisa, kilimo cha mboga, utengenezaji sabuni na biashara, kina wanachama
zaidi ya 25 na kimeanzishwa mwaka 2008.
MWISHO.
Comments
Post a Comment