NA HAJI NASSOR, PEMBA:::
SHERIA nambari 5 ya Wakala wa Habari,
Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988, ambayo imefanyiwa marekebisho mwaka 1997, inavyo
vifungu 81, vilivyobebwa na sehemu 1O.
Pamoja na marekebisho
hayo yaliyofanywa miaka 9, baada ya sheria hiyo kupita na sasa ikielekea kuwa
na umri wa miaka 21, lakini bado kuna vifungu vinatajwa kuuweka chini ya ulinzi
uhuru wa habari Zanzibar.
Ndivyo ilivyo kuwa
sheria hiyo, kwa wakati huo na miaka hiyo ilitungwa na kisha kusainiwa na rasi
wa wakati huo wa Zanzibar kwa nia nzuri, ingawa kwa sasa uzuri huo haupo tena.
WADAU WATAKA SHERIA MPYA
Ndio maana, kwa mfano
Shirika la Internews Tanzania kwa kushirikiana kwa karibu na TAMWA-Zanzibar na
wakati mkubwa na Baraza la Habari Tanzania MCT, wamekuwa wakita sheria bora na
fariki Zanzibar.
Kwani Mratibu wa
Internews Tanzania ofisi ya Zanzibar, Zaina Mzee, anasema sheria hiyo kwa sasa,
inakinzana pakubwa na dhana ya demokrasia na utawala bora unaochapuzwa na uhuru
wa habari duniani kote.
‘’Ni kweli sheria hiyo
kwa wakati wake, ilikuwa mzuri mno lakini kwa wakati huu, sasa sisi Internews
na wenzetu TAMWA-Zanzibar tunashirikiana ili kuona tunakuwa na sheria moja ya
habari Zanzibar,’’anasema.
Anasema waandishi wa
habari wa Zanzibar ni sawa na wengine duniani kote, hawana haja kuwekewa sheria
yenye vifungu vya maajabu na wakati mwengine vinavyozorotesha utawalabora na
uwajibikaji.
‘‘Kwa mfano ndani ya
sheria hiyo nambari 5 ya Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988,
ambayo imefanyiwa marekebisho mwaka 1997, kuna vifungu haviendani na hali ya
sasa,’’anasema.
Alikishangaa kifungu
cha 14 (1) kinachomlazimisha mchapishaji gazeti lililochapwa Zanzibar kwa kila
siku na kwa gharama zake, kuwasilisha nakala mbili kwa Mrajisi wa magazeti.
Akaeleza kuwa,
kinachosikitisha kuwa nakala hizo ziwe kwenye aina ya mfumo, karatasi zile zile
zilizochapishwa kwa ajili ya kusambaazwa au kuuzwa.
‘’Sheria hii kwenye
kifungu hichi, ni sawa na kuuweka chini ya ulinzia uhuru wa habari Zanzibar,
maana pamoja na gharama anazopata mchapishaji wa gazeti, anatakiwa tena kuingia
gharama za kuwasilisha nakala mbili,’’anafafanua.
Mkurugenzi wa
TAMWA-Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali, anasema biashara ya magazeti ilivyongumu,
kisha mchapisha sheria inamlazimisha kuwasilisha nakala mbili bure, hili sio
sahihi.
Anasema, hili ni tatizo
na linahitaji kutafuatiwa dawa ya haraka, maana Mrajisi alipaswa alinunue kwa
gharama zake, ili kumsaidia mtu aliyeekeza kwenye sekta ya habari.
‘’Kwa hakika uwepo wa
vifungu kama hivi na nvyengine, ni kuunyong’onyesha uhuru wa habari na
uwajibikaji kwa waandishi hapa visiwani,’’anasema.
Kifungu hicho cha 14
(3) kinafafanua kuwa nakala hizo zitawekwa kwa ajili ya kumbu kumbu, katika
eneo au mahala maalum.
Kifungu chengine
kilichotajwa na wadau na waandishi wa habari kuwa si rafiki kwa uhuru wa habari
Zanzibar ni kile cha 30 na 31.
Kifungu cha 30 cha
sheria hiyo, kinafafanua uwezo wa waziri kusimamisha uchapishaji wa gazeti lolote
ndani ya Zanzibar lililosajiliwa chini ya sheria hii.
‘’Endapo waziri ataona kwamba ni
kwa maslahi ya umma, au ni kwa maslahi ya amani na utulivu, atatekeleza kwa
kuamuru usimamishwaji wa kuchapishwa kwa gazeti husika,’’kinafafanua
kifungu hicho.
Kwenye kifungu cha 31
kimempa waziri husika, uwezo wa kukataza uchapishaji wa gazeti, ingawa kwa
ushauri wa Bodi, ataona kukatazwa huko ni kwa maslahi ya umma au ni kwa maslahi
ya amani na utulivu.
Hapa mwandishi Salma
Said aliwahi kusema kuwa, sheria kumpa uwezo mkubwa waziri sio sawa, maana wapo
wengine wanaweza kufanya uamuzi huo, kwa maslahi yao binafsi.
Akahojiwa kuwa, ndani
ya sheria hiyo neno maslahi ya umma hayana tafsiri ya kujitosheleza, hivyo
inaweza kujitokeza kwa waziri kuzuia uchapishaji kwa maoni yake.
Mwandishi Amina Massoud
Jabiri wa redio Jamii Mkoani, anasema kwa vile suala la kusambaaza na kupata
habari ni haki ya kikatiba, sio busara kupewa uwezo waziri husika.
Mratibu wa Internews Tanzania
ofisi ya Zanzibar Zena Mzee, anasema waandishi wa habari, hawatakiwi kuingiliwa
kama zilivyosekta nyingine, wakati wanapokuwa wanatekeleza wajibu wao.
‘’Mbona daktari
anapokuwa anatibu hakuna anayemuingilia, Polisi akilinda usalama yuko huru,
sasa iweje kwa sekta ya habari iwekewe vifungu vikali,’’anahoji.
Mwandishi Najat Omar wa
the Chanzo online anasema, wakati ndio huu kwa Zanzibar kuwa na sheria
inayokwenda sambamba na ulimwengu wa leo.
Mwanasheria wa Shirika
la Magazeti ya serikali Zanzibar Juma Khamis Juma, anasema sheria inapotoa
fursa ndogo, inaweza kuzaa janga wakati wa utekelezaji.
Mchambuzi wa sheria za
habari Zanzibar Imane Duwe, anasema, kazi inayofanywa na waandishi sio kwa
maslahi yao, bali ni utekelezaji wa haki ya kikatiba.
‘’Haki za kikatiba
wakati zinapotekelezwa hazitakii kuwekewa masharti mazito, kama yalivyo kwenye kifungu
cha 14, 26, 27, 30 na 31 cha sheria ya nambari 5 ya Wakala wa Habari, Magazeti
na Vitabu ya 1988,’’anasema.
Hata kifungu cha 27 (1)
ni miongoni mwa vifungu kinachompa Mamlaka Ofisa yeyote wa Polisi, kukamata
gazeti lolote, popote litakapoonekana limechapwa au kuchapishwa au ambalo kwa
maoni yake tu, atalituhumu kuchapishwa kinyume na sheria.
Ambapo kifungu cha 27
(3) pia kinampa Mamlaka hakimu kumuamuru Ofisa yeyote wa cheo cha mkaguzi au
zaidi, ikiwa ana sababu ya maana ya kuamini kwamba, atachelewa kupata hati ya
upekuzi anaweza kutekeleza uwezo alio nao kwa mujibu wa sheria.
Vifungu hivi kwa
nyakati za sasa, havipaswi kuwepo katika sheria hiyo kutokana na kuwa sio
rafiki kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Meneja wa radio Jamii
Micheweni Ali Massoud Kombo anasema, sio sahihi kwa Ofisa Polisi kupewa mamlaka
hayo, kwani uhuru wa habari, itakuwa bado haujakuwepo nchini.
"Ikiwa afisa
atakuwa na ugomvi na mwandishi, anaweza kufanya upekuzi au kukamata gazeti,
hali ambayo itasababisha taharuki katika vyombo vyetu,’’ anasema.
Mwanasheria wa serikali
Ali Amour Makame anasema kwamba, sio sahihi kifungu hicho kuwepo kwa sababu,
kisheria halitakiwi kuwepo neno ‘kwa
maoni yake’ na haifai kwa Afisa Polisi kupewa mamlaka hayo kwani, habari inaweza
kuwa sahihi kwa mujibu wa maadili yao, lakini yeye isimfurahishe.
‘’Elimu za Polisi
tunazijua, iweje wapewe mamlaka hayo kwa taaluma nyengine?, hii sio sahihi, kinachoshangaza
zaidi ni pale sheria hii ilipoeleza kwamba kwa maoni yake, akituhumu, hichi
kitu hakipo kwenye sheria’’, anafafanua.
Fat-hiya Mussa Said
ambae ni Mratibu wa TAMWA Pemba anaefahamisha, Polisi wana mamlaka ya kulinda
raia na mali zao na kulinda amani ya nchi, ndio maana walipewa mamlaka hayo,
lakini kwa wakati wa sasa kifungu hicho kinahitaji maboresho.
"Kitakapoboreshwa
kifungu hicho, waandishi watakuwa huru kufanya kazi zao za kihabari na wananchi
watapata habari, uhuru wa kutoa maoni na kujieleza", anasema.
Afisa Mdhamini MCT
Zanzibar Shifaa Said Hassan anasema, pamoja na kuzieleza sheria hizo na
mapungufu yake tangu 2010, lakini bado inaendelea kutumika, jambo ambalo
linawapa wakati mgumu katika kuendeleza tasnia ya habari nchini.
"Haya mamlaka
aliyopewa Ofisa Polisi sio sahihi kwa kweli na wala haileti picha nzuri, mimi naona
ni udhalilishaji wa waandishi na vyombo vyetu, tuendelee kuzisemea sheria hizi
ili vifungu vinavyotukwaza viondoshwe", anafafanua Shifaa.
NINI KINAFANYIKA
Mkuu wa taaluma wa Chuo
cha uandishi wa habari na mawasiliano ya Umma Zanzibar Imane Duwe, anasema
kwanza kufutwa kwa sheria hiyo kongwe na kuwa na sheria rafiki kw auhuru wa
habari.
Mwananchi Asha Salim
Ali mkaazi wa Wete anasema, ili kuwe na uhuru wa vyombo vya habari kuna haja ya
kuvifanyia maboresho vifungu vyote vinavyominya uhuru wa habari.
Khamis Mohamed mkaazi
wa Gombani Chake Chake anafahamisha kuwa, Ofisa wa Polisi asipewe mamlaka hayo
na badala yake iundwe bodi maalumu ya kuweza kuchunguza tuhuma na
itakapothibitika chombo kimekiuka sheria ndipo kichukuliwe hatua.
"Mimi
iliyonishangaza ni hii kwamba Ofisa Polisi hata akituhumu tu anaweza kukamata
gazeti au hata kitabu cha mwandishi, kwa kweli hii sio sahihi hata
kidogo", anafahamisha.
Mratibu wa Iternews
Zanzibar Zaina Mzee, anasema kwa sasa wako bega kwa bega kati yao na
TAMWA-Zanzibar na waandishi wa habari, ili kuviibua vifungu kandamizi.
Anasema anaamini
serikali hii ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi,
itachapuza upatikanaji wa sheria mpya na rafiki ya habari Zanzibar.
MWISHO.
Comments
Post a Comment