NA HAJI NASSOR, PEMBA:::
KWA zaidi ya miaka 10 sasa wadau wa
habari wamekuwa wakipaza sauti zao kutaka sheria mpya na bora ya habari
Zanzibar.
Wadau mfano
Baraza la Habari, TAMWA-Zanzibar na hata Shirika la Internews Tanzania ofisi ya
Zanzibar wamekuwa wakiungana na waandishi kuhakikisha sheria moja ya habari
inapatikana.
Mratibu wa
Internews ofisi ya Zanzinar Zaina Mzee, anasema moja ya sababu ya kutaka sheria
mpya ya habari Zanzibar, ni kuona zile mbili zilizopo zinafutwa.
‘’Ipo sheria ya Tume ya Utangaazaji
Zanzibar nambari 7 ya mwaka 1997, pamoja na marekebisho yake, pamoja na ile ya sheria
nambari 5 ya Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988, ambayo imefanyiwa
marekebisho mwaka 1997.
Anasema
sheria hizo, zimekuwa na vifungu ambavyo sio rafiki kwa kuimarisha uhuru wa
habari pamoja na uhuru wa kujieleza katika jamii.
Anaeleza
kuwa, pamoja na ukongwe wake sheria hizo mbili kuu zinazosimamia vyombo vya
habari, lakini kubwa zimekuwa zikiwabana waandishi katika kutekeleza haki ya
kikatiba.
‘’Katiba
ya Zanzibar ya mwaka 1984, kwenye kifungu chake cha 18 kimeweka wazi suala la kupata,
kusambaaza habari habari tena bila ya kujali mipaka ya nchi,’’anasema ilivyoeleza
sehemu ya katiba.
Mkurugenzi
wa TAMWA-Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali anasema, kwa wakati uliopo sasa Zanzibar
na duniani kote, lazima suala la kuwepo kwa sheria au vifungu vyenye ukakasi
havina nafasi.
‘’Kwa
mfano kwenye sheria mbili hizo, vipo vifungu vilivyompa uwezo mkubwa Waziri wa
kulifungia au kuzuia uchapishaji wa gazeti, akihisi kwa maoni yake, kunataka
kuchapishwa habari iliyokinyume na maadili,’’anasema.
Ndio
maana TAMWA-Zanzibar imekuwa karibu mno na wadau wake kama vile Shirika la
Internews, MCT na waandishi wa habari, kuhakikisha Zanzibar kuna kuwa na sheria
rafiki.
Mwandishi
Salim Said Salim, anasema huu sio wakati tena wa sheria zinazoongoza vyombo vya
habari, kumpa uwezo mkubwa Mkurugenzi, au Waziri.
‘’Inashangaaza
kuona katika sheria za habari, hadi leo kuna maneno kama waziri anaweza,
mkurugenzi akihisi, Polisi anaweza kupekuwa, haya yote yanaleta ukakasi kwenye
kazi za vyombo vya habari,’’anasema.
Mwandishi
Khadija Kombo wa ZBC Pemba, anasema ukakasi wa sheria za habari hapa Zanzibar,
wakati mwengine huwarejesha nyuma waandishi, kuibua changamoto za wananchi.
‘’Inawezekana
waandishi wa habari wanataka kuibua changamoto kubwa inayowahusu wananchi,
lakini vipo vifungu ambavyo vinatishia utendaji wao wa kazi,’’anasema.
Meneja
wa redio Jamii Mkoani Said Omar Said, anasema uwepo wa vifungu kandamizi kwenye
sheria za habari, wakati mwengine huwakosesha kujiamini waandishi katika kazi.
Mwanasheria
wa Shirika la Magazeti ya serikali Zanzibar na mhariri wa habari wa shirika
hilo, Juma Khamis Juma, anasema kwenye utekelezaji na tafsiri za vifungu vya
sheria, hakutakiwi kuwepo neneo lenye utata.
‘’Kwa mfano
neno waziri anaweza, akiona inafaa, akihisi na mengine yanayofanana na hayo,
huwa ni hatari kuwepo kwenye maelezo ya utekelezaji wa sheria,’’anasema.
Khamis Iddi
Mabrouk na mwenzake Issa Haji Khamis wa Kangagani, wanasema waandishi
wasipokuwa huru, hata wananchi hawatokuwa huru, kufanya uamuzi sahihi.
Hidaya Mjaka
Ali wa Vitongoji mwenye ulemavu wa viungo, anasema, wanavitarajia mno vyombo
vya habari, kuibua changamoto za jamii.
Mwanasheria wa serikali Ali Amour
Makame anasema kwamba, sio sahihi kifungu hicho kuwepo kwa sababu, kisheria
halitakiwi kuwepo neno ‘kwa maoni yake’.
Sheria ya
Tume ya Utangaazaji Zanzibar nambari 7 ya mwaka 1997, kwenye kifungu chake cha 13
(5) kimeutia doa huru wa habari Zanzibar.
‘’Mtu yeyote
asiyeridhika na uamuzi wa Tume kutoa au kataka maombi, anaweza kukata rufaa kwa
Waziri kwa namna ya njia itakavyoelezwa na kanuni,’’kinaeleza kifungu hicho.
Ambapo hapa,
momba leseni, anapokataliwa na Katibu Mtendaji wa Tume, akate rufaa kwa waziri,
ambae ndie aliyemteua au kusababisha kupatikana kwa Katibu huyo.
Wadau wa
sheria wanasema, jambo hilo lina utata, maana Katibu Mtendaji wa Tume ya
Utangaazaji na waziri anayehusika na utangaazaji, ni kiungo kimoja.
Mwandishi wa
Shirika la Utangaazaji Zanzibar ‘ZBC’ Khadija Kombo anasema, kama Tume imekataa
kutoa leseni, kifungu kingelekeza vyenginevyo, kwa mfano kukimbilia mahakamani.
Kifungu
chengine chenye maneno yenye ukakasi kwa ukuaji wa wa uhuru wa habari ni cha 27
(1), ambapo waziri husika au mwengine aliyeidhinishwa, anaweza kutoa amri
kumtaka mpewa leseni, atangaaze jambo lolote ambalo kwa maoni ya Waziri, lina
maslahi kwa umma au uslama wa taifa.
Hapa wadau
wa habari wanasema, kifungu hicho kipo kishari shari, maana kimebainisha uwezo
wa Waziri, kumlazimisha mpewa leseni kutangaaza jambo ambalo anaona tu ni kwa
maslahi ya umma au usalama wa taifa.
Mdhamini wa
Baraza la Habaeri Tanzania ‘MCT’ Zanzibar Shifaa Said Hassan, anasema neno kwa
maslahi ya umma, sheria hiyo haijalitafsiri, hivyo waziri anaweza kutumia
mwanya huo kutangaaza jambo ovu.
Hata
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA-
Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali, anasema, neno usalama wa taifa, sheria hiyo kwenye
vifungu vyake 30 na sehemu sita halikutajwa.
‘’Hapa mpewa
leseni, amewekwa njia panda, maana Waziri akiamka vibaya anaweza kutumia mwanya
huo, na kutoa taangazo ambalo halina maudhui na nchi, huku sheria
ikimlinda,’’anasema.
Ndio maana
Mratibu wa Shirika la Internews Zanzibar, Zaina Mzee, anasema vifungu ambavyo
vinampa uwezo mkubwa waziri, au vyenye utata, kwa sasa wanasimama kutaka
viondolewe.
Kama habari ni
haki ya kikatiba, sheria zinazosimamia ni vyema zisiwe na maneno au amelezo
yanayoashiria kumpa mtu mmoja uwezo, kama vile anajiamulia kufanya mambo yake
binafsi.
Mwandishi
Malik Shahran wa ZCTV anasema, suala la habari ni haki ya binadamu, si vyema
kuwepo kwa sheria inayoonesha nguvu za mtu mmoja kufanya uamuzi.
‘’Maneno
kama Waziri akiweza, atakavyoona inafaa au kwa maoni yake, yanapekelea wengine
kukosa hamu ya kuingia kwenye sekta ya habari,’’anasema.
Mwandishi wa
Mwanahalisi mtandaoni Jabir Idrissa, anasema athari kubwa ni wawekezaji sekta
ya habari, kukosa hamu ya uwekezaji, na kundi kubwa kukosa ajira.
Mwenyekiti
wa Klabu ya waandishi wa Habari Zanzibar ‘ZPC’ Abdalla Mfaume, anasema moja ni
kuzisemea sheria na vifungu kandamizi, ili waandishi wa habari wafanyekazi zao
kama ilivyo, kwa makundi mengine.
Rahma
Suleiman wa Gazeti la Nipashe, anasema waandishi na wadau wa habari, waungane
kusindikiza mswada wa sheria habari Zanzibar ulipofikia, upelekwe hatua
nyingine.
Mchambuzi wa
sheria za habari Zanzibar Imane Duwe, anasema maneno kama ‘uwezo wa Mkurugenzi, Waziri,
akiona inafaa, akihisi, kwa maoni yake’ kwenye sheria mpya ya habari
yasitumike.
Maryam Salum Habib mwandishi wa
habari wa Gazeti la Zanzibarleo Pemba anasema, Mamlaka hayo aliyopewa Ofisa wa
Polisi anaweza kukamata gazeti, atakapojisikia tu kukamata na sio kwa kufanya
kosa.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari
Tanzania (MCT) Kajubi Mukajanga anasema, waandishi wasipozielewa sheria zao,
mchakato wa kupitisha utakuwa kwenye mikono ya wanasheria na wanasiasa, na
hivyo watapendekeza wanavyotaka.
Anasema, kuna vifungu vingi ambavyo
vinahitaji kufanyiwa marekebisho ikiwemo cha 27 (1), (3), kwani vinawanyima
waandishi uhuru na kuwakosesha wananchi haki ya kutoa maoni na kujieleza.
MWISHO.
Comments
Post a Comment