NA
MARYAM SALUM, PEMBA@@@@
MFUKO
wa Maendeleo ya Jamii Tanzania ‘TASAF’ kupiti mpango wa kunusuru kaya maskini, umekua
ni kama kivuli, wakati wa kiangazi eneo la jangwani.
Mpango huu wa kunusuru kaya masikini, toka kuanza kwake nchini
umeweza kusaidia wananchi wengi, waliokuwa kwenye jua kali la kimaisha, na sasa
wamepata kuvuli.
TASAF kupitia miradi yake mbali mbali ya maendeleo, imeweza
kuwakomboa wananchi wengi kiuchumi, ambapo wengi wao wamekomboka kimaisha.
Wananchi wa shehi ya Ving’ambwa kijiji cha Vikunguni ni
moja kati ya wanufaika wa mpango huo, ambapo baadhi ya wanufaika hao wameanza
kupata mafanikio makubwa kupitia miradi hiyo.
Iko misemo mingi ya kiswahili ukiwemo mtaka cha mvunguni
sharti ainame’, wengine wakasema ‘abebwae hujikaza’ mgagaa na upwa hali wali
mkavu ikiwa na maana pana kwa mujibu wa jambo lenyewe.
WALENGWA
VIKUNGUNI CHAKE CHAKE
Fatma Khamis Mbarouk mkaazi wa Vikunguni shehia ya
Ng’ambwa Chake Chake, ni miongoni mwa wanufaika, anasema kwa sasa maisha yake
yako juu ikilinganishwa na hapo kabla.
Anasema mpango huo uliofanywa na TASAF wa kunusuru kaya
masikini tokea kuanza kwake, umesaidia
na kuwakomboa wananchi wengi, akiwemo yeye.
Yeye kila baada ya mwezi hupata ruzuku ikiwemo ya watoto
wanaokwenda skuli kuanzia msingi hadi sekondari na Klinik, ingawa kwa upande wa
hutofautiana kati ya mlengwa mmoja na mwengine.
“Wapo wanaopata ruzuku ya shilingi 30,000 hadi shilingi
40,000 na zipo fedha nyengine ambazo kila mlengwa hupatiwa na mfuko huo ambazo
ni shilingi 20,000 anaeleza mlengwa huyo.
Fatma, anasema kinachompa uhakika wa maisha na hasa
baada ya ujio wa TASAF, ambapo pamoja na ruzuku ya msingi anayoipata, lakini
anafurahishwa na kuwepo kwa ajira za muda.
‘’Hata uchimbaji wa mitaro, misingi ya barabara au
ujenzi wa matuta ya kinga ya maji, tukiyafanya kwa ajili ya wananchi wote,
tunalipwa ujira wetu,’’anasema.
Aisha Maliki anasema kwake TASAF ni kama mkombozi wa wanyonge
nchini, ambapo wengi wao wameweza kuona njia kiuchumi, kutokana na fedha za
ruzuku wanazopewa.
‘’Kwa hakikia TASAF kwangu imekuwa kama mtoto wangu wa
kumzaa, jinsi na namna inavyonienzi hasa katika eneo kukuza pato na uchumi
wangu,’’anaeleza.
Anaona TASAF kuandaa mpango huo kwa makusudi, umechangia
kwa kiasi kikubwa kuwatoa wananchi walio wengi kwenye unyonge na umaskini hasa
wa kipato.
‘’Kwa hakikia TASAF imetusaidia mno, maana tumekuwa
tukipata ruzuku ambazo sasa tumeshazihamishia kwenye vikundi vya ushirika na
sasa tumeshauaga umaskini,’’anaeleza.
CHANGAMOTO
KWA WALENGWA
Aisha Massoud Mohaamed, anasema moja ni fedha zao
kuingizwa kwenye mfumo wa kielektroniki, ambapo upatikanaji wa ruzuku hiyo moja
kwa moja, huwa mgumu.
Anainisha kuwa, TASAF awali walikuwa wakikabidhwa fedha
mkononi, na sasa baada ya kuwepo kwa ulazima wa rukuzu yao kupita benki ama
njia za kisasa, wamekuwa wakipata changamoto.
‘Mara unakumbana na mkato usiootegemea, mara unakwenda
kwa wakala hana salio na wakati mwengine mfumo unakuacha hupati kabisa, na hapo
ndio unarudi kwenye umaskini,’’analalamika.
Bimkubwa Issa anasema, hata mfumo wa wao kwenda benki
kutoa fedha zao, ni changamoto inayowaumiza, hasa kutokana na hali zao za
kipato kuwa kidogo kisha kukumbana na mikato ya benki.
“Chakushangaza tunapokwenda benki au kwa mawakala kutoa
fedha katika akaunti zetu, fedha hazitoki kamili kama tulivyoambiwa hapo
mwanzo, hivyo tunaomba kama kunamakato yoyote,” anafahamisha.
Hata Salma Ali Mohamed na wenzake Fatma Khamis Mbarouk, na
Mtumwa Ali Omar wakaazi wa shehia ya Vikunguni, wanaoma kero kubwa kwao ruzuku
waliokusudiwa wao kisha kuingia kwenye mfumo wa mikato.
Waliiomba Tasaf kuendeleza mfumo huo kuwaangalia
wananchi wenye hali duni kiuchumi, hasa kwa wale ambao hawajabahatika kufikiwa
kwa fursa hiyo kuwasaidia kwa njia moja ama nyengine ili nao waondokane na
utegemezi.
Asha Rashid Khamis mkaazi wa Vikunguni ameishukuru Tasaf
kwa kuwaona wananchi wenye hali duni kiuchumi, kwa kuwapatia fedha za
kuwasaidia watoto wao kwa matumizi ya Skuli, Afya na mahitaji mengine ya
lazima.
SHEHA
Sheha wa shehia ya Vikunguni Issa Rihani Abass, anasema
kuwa katika shehia yake wapo wananchi 2, 500 kati yao wananchi 226 ndio
wanufaika wa mradi wa kunusuru kaya masikini kupitia TASAF.
Anasema TASAF imewakomboa wananchi wa shehia yake kwa
kuwepo kwa vikundi kwa njia moja ama nyengine, wanachama wake wameondokana na
umasikini.
“Nashukuru katika shehia yangu TASAF imewakombowa
wananchi wengi waliokatika umaskini baada ya kuwapatia miradi kupitia mpango wa
kunusuru kaya maskini”, anasema.
Kuhusu changamoto za fedha za ruzuku kupitia kwenye
mfumo wa kielektroniki na benki, anasema limekuwa changamoto kwa wananchi hao
waliotarajiwa kuondolewa na umaskini.
‘’Kwa hakika tunazo taarifa kuwa mfumo huo umezaa
changamoto, na TASAF tumeshawapelekea, kwa hivyo wanazifanyia kazi ili kuona
walengwa wetu wanakuwa huru kupata fedha hizo.
TASAF
Mratibu wa TASAF Pemba Mussa Said, anasema kumekuwa na
malalamiko mengi kwa walengwa wao, aingawa anaona inatokana na uwelewa kuwa
chini juu ya mifumo.
“Wengi wao hutoa pesa kwa mawakala bila kujua kima cha
fedha kilichomo na kilichobaki kwenye akaunti, hivyo kupelekea kuwepo kwa
changamoto hiyo kwa walengwa,” anaeleza.
Ndio maana akashauri kuwa, kutokana na changamoto hiyo,
ni vyema kwa walengwa husika kutoa fedha zao benki, ili kuondokana na
malalamiko yasiyokuwa ya lazima.
Anafahamisha kuwa kwa sasa suala hilo haliwezi kuepukika
kirahisi rahisi kutokana na mfumo wa malipo ya Serikali kufanyika kwa mfumo huo
wa kutoa benki.
Ingawa anaeleza kuwa, TASAF kwa sasa imo kwenye mazungumzo
na Benki, ili walengwa wa kaya maskini wasiweze kukatwa fedha zao pale
wanapokwenda kutowa fedha zao.
Aidha anawashauri walengwa ambao uelewa wao ni mdogo
katika kujua salio lao wanapotaka kwenda kutoa fedha zao kwenye akaunti,
kuhakikisha wanachukua ndugu zao wenye uelewa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF
Tanzania, Mkurugenzi Uratibu TASAF Haika Shayo, alisema baada ya kuzuka
malalamiko, walikaa na viongozi wa serikali za mitaa, kuwapa mafunzo ya
ufafanuz ambayo anaamini yamesaidia kufanikisha lengo la mpango, na kupunguza
malalamiko.
“Sote tunafahamu
lengo ni kuwa na uwelewa wa pamoja na kuweza kuwahudumia walengwa, mutakuwa
mabalozi wa mpango kwa kuwafahamisha wananchi wetu pale wanapokuja katika
shehia zenu,” alisema.
Naye Ofisa ufuatiliaji na tathmini wa TASAF Pemba
Abrahman Khamis, anasema changamoto zilizomo kwenye mfumo, anatarajia sasa
masheha na madiwani wawaelimishe walengwa wao.
Hata hivyo kwa upande wa masheha waliahidi kwenda
kusimamia kikamilifu, shuhuli zote za TASAF zinazofika katika shehia zao, kwani
wao ndio viongozi wa Serikali kwenye shehia husika.
Mpango wa kunusuru TASAF ambao ulianza mwaka 2014, upo
kwenye shehia 78, na tayari hadi kufikia mwaka 2019, zaidi ya shilingi bilioni
14.4 zimeshawafikia walengwa kwa Pemba pekee.
Kwa hilo sasa walengwa hao 14,280 wamefanikiwa kuanzisha
vikundi 942 kati ya hivyo 700 vimeshasajiliwa, kwa ajili ya kuendeleza miradi
kama ya ufugaji, kilimo, kuweka na kukopa, wakitokea shehi za Ng’ambwa,
Kinyasini, Chimba, Kiwani, Konde, Makangale, Ndagoni pamoja na Tumbe.
MWISHO.
Comments
Post a Comment