NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
SERIKALI
ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi imedhamiria kwa vitendo
kukiinua kisiwa cha Pemba kiuchumi.
Hii imekuja, baada ya kuonekana kisiwa cha Pemba kwa miaka
mingi, kimeachwa nyuma, katika masuala ya ukuaji wa uchumi.
Lakini Dk. Mwinyi, hakuwa nyuma katika kuhakikisha wananchi wa
Pemba wanapata maendeleo kama wenzao wa Unguja, na ndio maana akatenga maeneo
maalum, kwa ajili ya uwekezaji mkakati.
Na miongoni mwa mambo, ambayo ameyafanya ili kuvutia wawekezaji
ni kuimarisha miundombinu mbali mbali, pamoja na kuweka punguzo la bei kwa mwekezaji
atakaeekeza.
Kuna mpango wa kujengwa uwanja wa ndege wa kimataifa, bandari
ya kisasa pamoja na kuimarisha miundombinu ya barabara, umeme na maji katika
maeneo yaliyotengwa kwa uwekezaji, ili uwekezaji uwe wa kiwango kizuri.
Kutokana na punguzo la bei lililowekwa kisiwani Pemba, itawahamasisha
wawekezaji kufika kwa wingi na hiyo, ni hatua moja wapo ya kukifanya kisiwa
hiki, kukua kiuchumi na kupata maendeleo.
Hii itawafanya wageni waekeze miradi mbali mbali, jambo ambalo
litasaidia kunogesha zile ajira 300,000 ambazo Dk. Mwinyi aliwaahidi wananchi
kipindi cha kampeni zake.
Pamoja na kwamba, kuna uwekezaji tangu hapo awali, lakini sasa
Serikali ya awamu ya nane, imekuja na uwekezaji mkakati, ili kuimarisha zaidi
suala la uwekezaji katika visiwa hivi.
Kwa sababu uwekezaji mkakati, ni tofauti na ule wa kawaida
kutokana na kiwango cha fedha, kinachohitajika kwenye uwekezaji mkakati kuwa ni
cha juu zaidi.
Pemba ni kisiwa ambacho kina malighafi nyingi na maeneo mengi
ya uwekezaji, kwa kuliona hilo Dk. Mwinyi ameunda Wizara maalumu kwa ajili ya
kushughulikia masula ya uwekezaji, ambayo yataimarisha uchumi wa wananchi wa
kisiwa hicho.
Fadhila Hassan Abdalla ni Afisa Mdhamini Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi
na Uwekezaji Pemba anasema, Serikali imepanua wigo kwa kuweka uwekezaji mkakati,
ambao ni lazima mradi wake utakaoanzishwa uwe ni wa kiwango kikubwa.
Hiyo itasaidia kukuza kipato cha wananchi na kuimarisha uchumi
wa nchi, kwani watapata ajira za muda na za kudumu na hivyo, maisha yao
yataimarika.
Lakini kutokana na kwamba, Serikali kutaka kukifungua kisiwa
cha Pemba kiuwekezji, imeamua kupunguza bei kwa mwekezaji atakaefika kisiwani
hapa kuwekeza, ukilinganisha na kule kisiwa cha Unguja.
Lengo ni kuwa, wawekezaji hao wafike kwa wingi kuwekeza, hali
ambayo itapelekea kuimarika kwa kipato cha mtu mmoja mmoja na kuimarisha uchumi
wa nchi, kutokana na fursa zitakazokuwepo za kiuchumi.
Mwekezaji anaetaka kuekeza kisiwa cha Pemba, anatakiwa kulipa
kuanzia dola milioni 10, huku upande wa Unguja ni dola milioni 100, hii
inaonesha dhahiri, dhamira ya Rais wa Zanzibar, kuifungua Pemba kiuchumi.
‘’Uwekezaji mkakati kwa kisiwa cha Unguja ni lazima mradi uwe
na mtaji kuanzia dola milioni 100 na kwa Pemba ni lazima uanze na dola milioni 10,
na muekezaji atapewa cheti cha kwamba yeye ni muekezaji mkakati,” anaelezea.
Kuwekwa dola milioni 10, kwa Pemba ni matakwa ya kiserikali,
kuona kwamba miaka mingi haijafunguka kiuchumi na awamu ya nane inataka kuifungua.
Kwa hiyo, kuna fursa unazipata ukiwa mwekezaji mkakati au wa
kawaida katika kisiwa cha Pemba, ambapo fursa hizo ni miongoni mwa masuala ya
kodi na uingizaji wa vifaa, ambavyo vitatumika wakati wa ujenzi.
“Kwa mujibu wa sheria, muwekezaji mkakati anapewa miaka isiyopungua
mitano (5) kuendesha biashara zake bila ya malipo, ukiachia mambo mengine
anayopaswa kulipa, sasa hiyo ni fursa na Serikali imefanya hivyo makusudi kwa
ajili ya kuchapuza uchumi,” anaelezea.
Na sasa tayari wameshapokea wawekezaji mkakati katika kisiwa
cha Pemba kwa sababu kwenye visiwa vitano, ambavyo vitawekezwa, ni uwekezaji
mkakati, lakini pia wana mradi wa hoteli ya nyota saba, amabayo itajengwa Makangale
kwenye fukwe ya Vuma Wimbi.
Wanamategemeo makubwa kwamba, uwekezaji wa miradi mikakati
utaongezeka, katika kisiwa hiki kwa sababu ya asili yake, mazingira pamoja na
fursa kubwa walizopewa wawekezaji ambazo zimepangwa makusudi kwa mujibu wa
sheria.
“Kwa sasa hivi
wawekezaji mkakati kisiwani hapa ni saba (7) na wawekeji wa kawaida tunayo
miradi 17, inayotoa huduma, huku miradi 11 ikiwa katika hatua ya ujenzi na
miradi kumi (10), ipo katika hatua ya awali.
Uwekezaji wa kawaida, kwa mkoa wa Kaskazini Pemba ni miradi 25
yenye ajira 600, ambapo miradi 11 inatoa huduma, miradi mitano (5) ipo katika
hatua ya ujezi na miradi tisa (9) ipo katika hatua ya awali.
Katika eneo la Chamanangwe, kuna miradi maalumu minne mikubwa iliyojitokeza
hadi sasa, eneo hilo limetengwa mahususi kwa ajili ya viwanda na lina ukubwa wa
ekari 55.7.
“Kuna miradi ya maji pale, tumeshapokea mradi wa utengenezaji
wa bati unaomilikiwa na mradi wa ‘Safina Group Limited’ ambao una mtaji wa
zaidi ya Dola milioni 2, upo mradi wa kiwanda cha mwani na mradi wa kiwanda cha
tomato paste, ambao huu una mtaji wa dola 500,000 ,” anaeleza Mdhamini.
Katika eneo hilo la Chamanangwe, wana miradi hiyo minne ya
viwanda ambapo kuna wawekezaji tayari, wanatoa huduma lakini wengine tayari
vyeti vyao vimeshatolewa, ambao wapo katika hatua za awali za kuandaa michoro
na kufanya makisio kwa ajili ya kuanza shughuli.
Kwa Kaskazini Pemba miradi mengi iliyopo ni ya hoteli, hivyo
miradi minne ya Chamanangwe ni maalumu katika maeneo ya viwanda na ni tofauti
na ile miradi 25, ambapo ikijumlishwa ni miradi 29.
Upande wa Mkoa wa Kusini wana miradi ya kawaida 13 ambayo miradi
mitano (5), ipo katika hatua ya ujenzi na miradi iliyo katika hatua ya awali ni
mitatu (3).
Miradi saba, ambayo ni ya uwekezaji mkakati, mingi ni ya
visiwa vidogo vidogo na ule wa hoteli ya nyota saba, itakayojengwa katika eneo
la fukwe ya Vuma Wimbi Makangale wilaya ya Micheweni Pemba.
Na ndio maana, eneo jingine
la ujio wa miradi ya aina hii, inakuja pia kutekeleza kwa vitendo Ilani ya uchaguzi
ya CCM ya mwaka 2020/2025 Ibara ya 139 (c) (ii) ya ‘kuimarisha ukusanyaji
wa mapato ya ndani kutoka wastani wa shilingi bilioni 800.0 kwa mwaka 2019 hadi
kufikia shilingi trilioni 1.55 kwa 2025’.
MAFANIKIO
Uwekezaji mkakati, utaleta mafanikio makubwa katika kisiwa cha
Pemba kutokana na kuwa, ni uwekezaji ambao utakuwa na faida kubwa.
Ni kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, kwani miradi itakuwa ni
mikubwa, hivyo itaajiri watu wengi kuanzia katika hatua ya ujenzi na pia baada
ya kumaliza wataajiri wafanyakazi.
“Hata mapato Serikalini yatakuwa tumeyakuza kwa kiasi fulani
na jamii itafaidika katika hiyo miradi, hata ule mradi kuwepo tu kwenye eneo basi
huduma nyingine za kijamii, zitaongezeka kwa asilimia kubwa,” anaeleza.
Wanachokitazamia zaidi katika miradi hiyo, wanataka mwekezaji
anapohitaji wafanyakazi wa zile kada, ambazo zitakuwa zinapatikana kisiwani hapa,
basi wawaajiri wananchi ili wafaidi uwekezaji kwa kukuza vipato vyao.
“Tunawashajiisha wawekezaji wa miradi mikakati na hii ya
kawaida, wakiwa wamewekeza wenyeji zaidi, basi ile faida inabaki hapa, tofauti
na miradi mengine ambayo moja kwa moja ni ya kigeni,” anafafanua.
Na kama wawekezaji watafurika kisiwani Pemba, hapa tutaitekeleza
Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025, ambayo imedhamiria kukuza pato la
taifa, kutoka thamani ya shilingi bilioni 2.4 kwa mwaka 2015 hadi shilingi trilioni
3.1 kwa Zanzibar.
Mwisho
Comments
Post a Comment