MADEREVA na wananchi wanaotumia barabara ya Ole-Kengeja, iliyofunguliwa
mwaka 2020 na aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Dk. Ali Mohamed Shein, wamefurahia
baada ya zoezi la uwekaji wa alama za barabarani kuanza.
Walisema awali, barabara hiyo iliyofunguliwa miaka minne sasa,
haikuwa na alama za barabarani, jambo ambalo lilikuwa likiwapa ukakasi,
wanapokuwa barabarani.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema kwa sasa wamefurahishwa
na uamuzi wa serikali wa awamu ya nane, chini ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi,
kuitaka wizara husika, kuiwekea alama barabara hiyo.
Walisema kuwa, kukosekana kwa alama za barabarani, kulikuwa
kunatishia maisha yao na watembea kwa miguu, kutokana na kukosekana la alama hizo
muhimu.
Mmoja kati ya madereva hao, Mohamed Khamis Hasnuu alisema,
walikuwa wakipata shida hasa kwa wao wageni wa barabara hiyo, jambo ambalo lingeweza
kusababisha ajali.
‘’Hujui wapi kuna skuli, soko, hospitali, mpindo na muunganiko
wa barabara moja na nyingine, maana alama ndio hasa mwelekeo wa barabara,’’alisema.
Nae dereva Abdalla Mohamed Othman, alisema walikuwa wakipata
tabu, wakati wanapokua kazini, jambo ambalo likuwa hawaliwapi raha ya kazi yao.
‘’Kama barabara haina alama za barabarani, inakuwa kama vile
jangwa, hujui wapi kuna daraja kubwa, ndogo, mpindo, skuli jambo ambalo, linaweza
kuchangia ajali zinazoepukika,’’alifafanua.
Muendesha piki piki ‘boda boda’ eneo la Kenya- Chambani Mohamed
Omar Hassan, alisema alishapata ajali mara mbili, wakati anaaza kuitumia barabara
hiyo.
‘’Nilipofika eneo la kwa mlima kwa Mtora, kumbe mbele kuna njia
ya kuingia skuli ya Ukutini, sasa kuna wanafunzi wanafukazana, nilibidi niingie
msingi kwa kuwakwepa,’’alifafanua.
Alieleza kuwa, alikuwa haoni alama yoyote ya barabara hiyo mpya,
jambo ambalo linaweza kupoteza mwelekeo, hasa kwa madereva wapya wa matumizi ya
barabara hiyo.
Abiria Asia Mwalimu Mohamed na mwenzake Maryam Muhene Issa wa
Chambani, walisema wanategemea baada ya zoezi la uwekaji wa alama za barabara,
ni madereva kuziheshimu.
Walisema kutokana na matumizi mabaya ya bara bara, hasa kwa gari
za abiria na waendesha boda boda, hawatarajii alama hizo kusaidia.
Mapema Afisa Mdhamini wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji
Pemba Ibrahim Saleh Juma, alisema kazi hiyo inafanya na kampuni ya M/S. Engineer
Grade Sign LDT, kutoka Tanzania bara.
Alieleza tu, kampuni imepewa kazi hiyo kwa miezi sita, kwa
barabara za Unguja na Pemba, ambapo pia inahusika na uwekaji wa matengenezo ya
pembezoni mwa barabara ili idumu zaidi.
Alisema, serikali ya awamu ya nane, imeona bora kuiwekea alama barabara
hiyo, ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima, hasa pale madereva wanapoamua
kuzifuata.
‘’Uhai na ustaarabu wa barabara ni kuwepo kwa alama za
barabarani, ambazo hizi huwasaidia madereva kujua daraja lipo wapi, mlima upo kilomita
ngapi, soko, skuli, hospitali ili kupunguza mwendo na kwenda kwa tahadhari,’’alisema.
Hata hivyo, Afisa Mdhamini huyo, ameendelea kuwanasihi wananchi,
kutosogelea hifadhi ya bara bara wakati wanapoendesha ujenzi wa nyumba za makaazi,
biashara au nyumba za ibada.
Bara bara hiyo yenye urefu wa kilomitya 35, ndio barabara refu kwa
Zanzibar, imepitia wilaya za Chake Chake na Mkoani na shehia 15, ikiwemo Ole,
Vitongoji, Mfikiwa, Ukutini, Chambani, Kendwa na Kengeja.
Bara bara hiyo ina upana wa mita 7.5 na imejengwa kwa kiwango
cha lami ya moto, ina uwezo wa kutumiwa na gari zenye uzito wa tani 10, inayo
madaraja 16 na culvert ndogo ndogo 118, pamoja na miundombinu ya kupitishia
huduma za kijamii ikiwemo mabomba ya maji.
Gharama za ujenzi huo ulifanywa kupitia mkopo wa Benki ya wanachama
wa nchi zinazotoa mafuata kwa wingi duniani (OFID), ikishirikiana na serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ambapo hadi kukamilika kwake imegharimu shilingi bilioni 30.935,
kati ya hizo mkopo kutoka OFID, ni shilingi bilioni 24.2 na serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imechangia shilingi bilioni 6.735.
Mwisho
Comments
Post a Comment