NA HAJI
NASSOR, PEMBA:::
KIFUA kikuu ni
ugonjwa wa kuambukiza, unaosababishwa na vimelea aina ya bakteria, kitaalamu vinaitwa
‘Mycobacterium tuberculosis’.
Vimelea hivi kikawaida havionekani
kwa macho matupu, mpaka muhusika atumie kifaa maalum kinachoitwa darubini.
Ugonjwa
wa kifua kikuu kitaalamu unaoitwa ‘Tuberculosis’ TB’ ni miongoni mwa magonjwa 10,
yanayosababisha vifo kwa wingi duniani kote.
Pamoja na
kwamba, ugonjwa huo umeenea ulimwenguni, lakini kutokana na hali ya kiuchumi
kwa nchi za bara la Afrika ulivyo, ndio nao umekuwa hatari zaidi.
Tafiti
zilizofanywa na Shirika la Afya Ulimwenguni ‘WHO’ zinaarifu kuwa, inakisiwa
watu milioni 10 wameugua kifua kikuu ‘TB’ duniani kote, hadi kufikia mwaka
2020, na kati ya hao watu milioni 1.5 wamefariki dunia.
Utafifi
huo ukagundua kuwa, kwa Zanzibar inakisiwa kuna wagonjwa 124 katika kila watu 100,000 ambapo hii ni sawa na wagonjwa 1,612 kwa mwaka.
Hadi
mwaka 2021, Zanzibar kuligundulika jumla ya wagonjwa 1,090 ambapo hao ni sawa na
asilimia 68 ya lengo lililowekwa la kuwafikia wananchi kuwafanyia uchunguuzi,
ingawa kulikuwa na vifo sawa na asilimia 6 katika mwaka 2020.
DALILI ZA KIFUA KIKUU
Mtaalamu kutoka kitengo
shirikishi cha maradhi ya ukoma, kifua kikuu na Ukimwi Zanzibar, Said Khamis
Ahmada, anasema kila ugonjwa unazo dalili zake, kama ilivyo kwa kifua kikuu.
Moja kati ya hizo nyingi ni kikohozi cha muda mrefu,
kuanzia wiki mbili ‘2’ au zaidi, ambapo mtu anaweza kukohoa mfululizo au
kukatisha katisha.
‘’Kila mmoja na afya yake, inawezekana mwengine
akapata wiki moja kikohozi hicho, na mwengine akapindukia wiki mbili, na kisha
wakifanya vipimo wakagundulika,’’anasema.
Dalili nyingine ni kukohoa makohozi ambayo wakati
mwengine huchanganyika na damu, ambayo huanza mapesi mepesi mfano wa mafuta ya
nazi na kisha kuwa mazito mfano wa mafua mapevu.
‘’Haina maana kuwa, kila anayetoka makohozi na damu
ana dalili ya kifua kikuu, bali tunaweza kumuita mhisiwa na kisha baada makohozi
kuoteshwa, jawabu litatoka,’’anaeleza.
Hapa chakijifunza ni kuhakikisha kila mwenye homa
kali na kikohozi cha muda mrefu, ni kufika kituo cha afya na kuomba kupewa
chombo maalum, ili kuchunguuzwa makohozi.
Lakini hata kutokwa na jasho jingi wakati wote na hasa
nyakati za usiku, hata kama hali ya hewa ni ya baridi, ambapo mtu huyo
hushauriwa kufanya vipimo.
Dalili nyingine kwa mtu ambae ni mhisiwa wa
ugonjwa wa kifua kikuu ni kukonda na kupungua uzito bila ya kuwepo kwa sababu
maalum.
Maana inawezekana, mwengine amekonda kwa
kufukuzwa kazi, kuachwa, kuolewa, kubaguliwa, kunyanyapaliwa au kuishi na
ugonjwa na mwengine.
Anabainisha kuwa, kwa baadhi ya watu ambao ni
wahisiwa wa kifua kikuu, huwa na dalili ya homa za mfululizo wiki mbili na
wengine Zaidi, hasa wakati wa jioni.
VIPI UCHUNGUUZI WA KIFUA KIKUU UNAFANYIKA?
Wataalamu wanasema, uchunguzi wa kifuakikuu unafanyika kwa njia tatu
kuu, ikiwa ni pamoja na kupima makohozi kwenye maabara kwa kutumia kipimo cha ‘Gene Expert’.
Njia nyingine ni ya kutumia
darubini, kuotesha makohozi katika maabara,
kwa ajili ya ugunduzi wa vimelea na pia kubainisha dawa zinazofaa kuua vimelea
vilivyooteshwa.
Njia nyingine ni ya uchunguuzi wa
kifua kwa kupiga picha ya kifua ‘x-ray’ pale ambapo, vimelea
havijaonekana kwenye darubini.
LIPI LENGO LA MATIBABU?
Wataalamu wa afya ya mwanadamu wanasema kuwa, kila aina ya matibabu
yanayofanyika hospitalini na vituo vya lengo ni kuponyesha mgonjwa husika.
Pamoja na lengo hilo kuu, lakini kwa upande wa ‘TB’ pia
ni kuzuia
maambukizi yasienee katika jamii au ya watu wengine hata mfano wa wanafamilia.
Ndio maana, Mratibu wa Kikfua kikuu na
Ukoma kanda wa Pemba Dk. Hamad Omar Hamad, anasema wamekuwa wakihimiza jamii
wasisubiri kutibu, bali wakimbilie kwenye kinga.
‘’Kila siku tunazungumza kuwa kinga ni bora
kuliko tiba, ndio maana tunataka kila mmoja, kila baada ya muda afanye
uchunguuzi wa afya yake,’’anashauri.
Mratibu huyo akafafanua kuwa, lengo jengine la matibabu ni kuzuia usugu
wa dawa ‘TB sugu’ maana kama mtu atajihisi ana dalili za kifua kikuu, na
kukosa dawa kwa wakati atazalisha ‘TB sugu’.
Kumbe hata lengo kuu la matibabu pia ni kuona kunazuiwa
kwa vifo vitokanavyo na kifua kikuu, ambapo kwa sasa inakadiriwa watu milioni 10, wameugua ugonjwa huo duniani
kote, na hadi mwaka 2020, na kati ya hao, milioni 1.5 wamefariki dunia.
MATIBABU
YA TB YANAKUWAJE?
Mtaalamu wa
magonjwa ya kifua kikuu na ukoma kutoka kitengo shirikishi Zanzibar, Valeria
Rashid, anasema matibabu ya ‘TB’ huchukua kati ya miezi sita (6), hadi mwaka mmoja.
Ambapo mgonjwa anatakiwa kula
dawa chini ya usimamizi ‘nyumbani au kituo
cha afya’ kilichokaribu naye, ili kupata uhakika wa dozi vizuri.
‘’Haina maana kuwa jamii
hatuiamini, lakini kwa umakini na tahadhari, tunapendelea iwe hivyo, ili kuona
dozi anayotumia imemponyesha ama laa,’’anasema.
Waziri wa Afya Zanzibar
Nassor Ahmed Mazrui, anasema vituo vyote vya afya vya watu binafsi na serikali,
vinatoa matibabu bila ya malipo, kwa wagonjwa wote wa ‘TB’.
‘’Ni fursa kwa wananchi kufanya
uchunguuzi wa afya zao, na ikiwa wamegundulika na ‘TB’ wanapewa matibabu bure
katika vituo na hospitali zote za serikali na watu binafsi,’’anaeleza.
Jamii imekuwa ikishauriwa,
hata kupungua ama kuondoka kwa ugonjwa wa Corona, lakini bado njia moja kubwa
ya kuzuia kifua kikuu ni kufunika mdomo na pua, wakati wa kukohoa au kupiga
chafya.
Njia nyingine, ni kuhakikisha
kwamba watu walio karibu na mgonjwa wa kifua kikuu ambao wanakohoa,
wanachunguzwa afya zao ili kuangaliwa kama wana kifua kikuu ama laa.
Jingine ni kila mmoja
kujiepusha na misongamano ili kuruhusu hewa ya kutosha mfano sokoni, kwenye
usafiri wa umma, maeneo ya kielimu na nyumba za ibada.
LIPI
JUKUMU LA VYOMBO VYA HABARI
Septemba 18 mwaka huu, Kitengo shirikishi cha Kifua
kikuu, homa ya ini, Ukiwmi na Ukoma kilikutana na waandishi wa habari wa vyombo
mbali mbali, ili kukisaidia kitengo hicho.
Hapa waandishi hao wa habari, pamoja na mambo mengine
walitakiwa kuielimisha jamii, athari za unyanyapaa kwamba zinaweza kuzuia
mapambano dhidi ya magonjwa hayo.
Akifungua mkutano
huo, Meneja Mpango wa Shirikishi wa magonjwa ya Ukimwi, Kifua kikuu na Ukoma
Pemba Khamis Hamad Khamis, alisema vyombo vya habari, ni nyenzo pana ya kutoa
elimu ya kupambana na magonjwa hayo.
‘’Tafiti
zinaonesha kuwa, hadi mwaka 2020 duniani kulikuwa na watu milioni 10, waliopata
ugonjwa wa kifua kikuu na kati yao, milioni 1.5 waliripotiwa kufariki
dunia,’’alifafanua.
‘’Kama vyombo vya habari
vitafanyakazi kazi zake kwa kina juu ya kutoa elimu ya umuhimu wa kuchunguuza
afya na athari za unyanyapaa, idadi ya wanaochunguuza itaongezeka,’’anasema.
Baadhi ya
waandishi wa habari akiwemo Mchanga Haroub Shehe aluyekuwa wa Shiria la
Utangazaji Zanzibar ZBC, na mwenzake kutoka Sauti ya Ist-qama Salim Ali
Msellem, walisema mikakati endelevu inahitajika ili kutokomeza magonjwa hayo.
mwisho
Comments
Post a Comment