NA SALUM VUAI, ZANZIBAR;
KWA miaka mingi sasa,
sekta ya habari visiwani Zanzibar, licha ya kupata mafanikio kadhaa, lakini
imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazobana uhuru wa waandishi
kutoa na wananchi kupata habari.
Ingawa uhuru umeongezeka
kwa kiasi fulani, lakini bado baadhi ya watu wamejenga dhana kwamba waandishi
wa habari ni maadui wanaopasa kuogopwa kama nyoka mwenye sum kali.
Mara kwa mara, waandishi
wa vyombo vya habari ama wameripoti kunyimwa taarifa au kuamriwa kutozitangaza
hasa pale kunapokuwa na matukio yanayoshtua umma ambayo yana chembechembe za
uzembe wa viongozi na watendaji wakuu wa serikali.
Hali inakuwa mbaya zaidi
pale ambapo hata viongozi wa serikali na taasisi zake wanapokataa kutoa
ushirikiano kwa waandishi endapo watabaini wanatafuta ukweli juu ya taarifa
zinazogusa maslahi yao binafsi.
Hata hivyo, viongozi kama
hao wanakuwa marafiki wakubwa kwa waandishi wanapotaka kutangazwa vizuri na
kusifiwa kwa mambo wanayodhani yanaweza kuwajenga.
Ili kuondoa vikwazo hivyo,
marekebisho ya sheria ya habari kimekuwa kilio kikubwa kwa waandishi, wakidai
sheria mpya inayokwenda na wakati uliopo na isiyokuwa na masharti yanayoumiza.
Ifahamike kuwa, uhuru wa
habari na kutoa maoni, ni miongoni mwa haki za binadamu zilizomo katika
mikataba mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Hiyo inatokana na masuala
ya haki hizo za binadamu kuanza kuingizwa katika mikataba hiyo mnamo mwaka 1950
baada ya dunia kuweka Azimio la kuzilinda kimataifa (Universal Declaration of
Human Rights-UDHR) lililofikiwa mwaka 1948.
Kama hiyo haitoshi, barani
Afrika, suala la haki za binadamu liliainishwa katika mkataba wa Afrika
kuhusiana na jambo hilo lililopitishwa mwaka 1981.
Mwandishi wa makala haya
pamoja na kupekua nyaraka tofauti zinazozungumzia haki ya kutoa na kupata
maoni, pia alizungumza na baadhi ya waandishi wa habari wakongwe sambamba na
wanaharakari kadhaa ambao ni wadau wa habari.
Mazungumzo hayo
yalijielekeza katika umuhimu wa kutaka kuharakishwa kwa sheria mpya ya habari
itakayokata minyororo inayokwaza upatikanaji wa habari nchini, lakini pia
isiyotafuna.
Mwenyekiti wa Jumuia ya
Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar Hawra Shamte, akitoa mada katika
warsha ya kuchechemua waandishi juu ya sheria mpya ya habari iliyofanyika Juni
25, 2022 ukumbi wa sanaa Rahaleo, alikuwa na haya ya kusema:
“Haki ya uhuru wa
kujieleza ambayo pia inahusu haki ya uhuru wa habari inalindwa chini ya Ibara ya 18 ya Katiba ya Zanzibar,”
alisema.
Ibara hiyo 18 (1) inasema:
“Bila ya kuathiri sheria nyengine za nchi, kila mtu anayo haki ya uhuru wa
maoni (kujieleza), kutafuta, kupokea na kusambaza habari na mawazo yake kupitia
chombo chochote cha habari bila kujali mipaka ya nchi na pia anayo haki na
uhuru wa kutoingiliwa mawasiliano yake.
Ibara hiyo hiyo kifungu
namba 2, kinasema:
“Kila raia anayo haki ya
kupewa taarifa wakati wote wa matukio mbalimbali nchini na duniani kwa jumla
ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia masuala yenye
umuhimu kwa jamii.
Hata hivyo, kwa mujibu wa
Shamte, akinukuu mapungufu yaliyomo kifungu cha kwanza kama yalivyooneshwa
katika rasimu ya marekebisho pendekezwa ya sheria ya habari, kinanyang’anya
haki na hivyo kifungu hicho kina makucha.
Hapo ilipoelezwa katika
kifungu hicho cha Katiba, maneno; “Bila kuathiri sheria nyengine yoyote ya
nchi”, kinamaanisha kuwa, kufurahia uhuru wa kujieleza, kutafuta, kusambaza
habari, unategemea sheria nyengine za nchi.
Aidha Ibara ya 24 ya
Katiba ya Zanzibar imeweka mipaka ya jumla ya haki na uhuru ambayo inasomeka
kama ifuatavyo:
“Haki za binadamu na
uhuru, kanuni zake ambazo zimeainishwa katika Katiba hii, hazitatekelezwa na
mtu kwa namna ambayo itasababisha kuingiliwa au kukandamiza haki na uhuru wa
watu wengine au maslahi ya umma.”
Aya iliyotajwa hapo juu,
inaweka bayana kwamba haki na uhuru huo
unaweza kuwekewa mipaka na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi ikiwa KIZUIZI HICHO NI CHA LAZIMA na kinakubalika
katika mfumo wa kidemokrasia.
Katika nukuu hizohizo,
Shamte alionesha wasiwasi kuwa kifungu hicho kinatoa nafasi kwa Baraza la
Wawakilishi kuweka mipaka ya kufurahia uhuru wowote ikiwa ni pamoja na ule wa
kujieleza.
Kwa maoni hayo na mengine
mbalimbali kuhusu uhitaji wa sheria mpya ya habari hapa Zanzibar, uko ulazima
Katiba hiyo pia ifanyiwe marekebisho ya haraka na ni wajibu wa waandishi wa
habari kuchagiza jambo hilo lifanyike
sasa bila ya ajizi.
Haja ya uharaka huo
inakuja kwa vile zipo sheria nyengine nyingi zinazoathiri uhuru wa habari na
haki ya kujieleza, kwa mfano sheria za usalama wa Taifa, Baraza la Wawakilishi,
Takwimu na ile ya makosa ya mtandaoni ambayo imetungwa Tanzania Bara na
haijaridhiwa Zanzibar lakini inatumika.
Pamoja na mapungufu mengi
yaliyomo kwenye sheria ya habari Zanzibar, takriban wadau wote niliotaka maoni
yao, wameshauri kuwepo maeneo yanayokataza matumizi makubwa ya nguvu kwa
wanahabari pale wanapozuiwa kutafuta taarifa, kupiga picha na baada ya
kuzitangaza habari ambazo zitahisiwa kwenda kinyume na sheria za nchi, au japo
kwa upande mmoja kutopendezewa tu kutolewa kwa taarifa husika.
Wengine walikwenda mbali
kwa kusema wakati sasa umefika kuongeza maradufu uhuru wa habari na kujieleza
kwa kukopia mfumo wa ‘Hyde Park’ unaotumika nchini Uingereza.
Hyde Park ni eneo
mashuhuri lililoko Westminster katikati ya London lililoanza karne nyingi nyuma
ambalo watu wako huru kukutana na kujadili siasa na mambo mengine ya kijamii
yanayohusu jamii zao.
Kwa jina maarufu, eneo
hilo hujulikana kama ‘Kona ya Spika’ na zamani Polisi walikuwa wakiwazuia watu
kwa kuwatoa nje, hadi ilipoamuliwa kuundiwa nafasi ili kuwapa watu uhuru kujadili
mambo wayatakayo kwa amani.
Kila Jumapili watu husimama juu ya sanduku maalumu
na kutoa maoni yao kwa uhuru juu ya siasa, dini au chochote.
Inasemekana kuwa sababu ya watu kutakiwa wasimame
juu ya sanduku, yatokana na sharti kwamba haipaswi mtu kuikosoa serikali ya
Uingereza huku akiwa amekanyaga ardhi ya nchi hiyo.
Kauthar Is-hak ni Ofisa Habari na mwandishi
mwandamizi katika Idara ya Habari Maelezo Zanzibar.
Alisema dunia ya sasa ni tofauti naya kale ambapo
teknolojia imetawala na ndiyo inayowaleta watu pamoja kwa muda mfupi na kwa
haraka zaidi.
Alieleza kuwa mitandao ya kijamii imerahisisha mawasiliano
na hakuna kitu kinachoweza kufichwa.
“Huu si wakati wa kufungana midomo, ni kweli uhuru
una mipaka lakini ni vigumu kuwadhibiti watu wasitoe joto lao. Muhimu sheria
zisiwabane watu kwa kuwa tu kundi la wateule fulani hawataki mambo yajulikane,”
alifafanua.
Kauthar alikosoa mtindo wa baadhi ya viongozi na
watu wengine wenye nyadhifa kubwa, kuwaelekeza waandishi wa habari juu ya mambo
ya kuandika na kutangaza, akisema kufanya hivyo ni woga na kutojiamini juu ya
utendaji wao.
Kuhusu adhabu kwa vyombo vya habari, Kauthar alisema
hilo ni jambo linalohitaji kutazamwa kwa jicho la tatu kwa maslahi ya wengi na
taifa kwa jumla.
Alimkariri Waziri wa Habari na Teknolojia Tanzania
Nape Nnauye katika hutuba aliyoitoa hivi karibuni kwenye sherehe ya kuadhimisha
miaka 60 ya shule kuu ya habari na mawasiliano ya umma ya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam.
Katika sherehe hizo, Nape alisema kitendo cha
kulifungia gazeti, redio au televisheni pale mwandishi mmoja anapoandika habari
potofu dhidi ya mtu au taasisi yoyote, si busara kukifungia chombo cha habari.
“Tuchukulie mfano wa sekta ya afya, iwapo daktari au
muuguzi amekiuka maadili, ni yeye ndiye wa kuhukumiwa na haifungiwi hospitali
kwani kufanya hivyo kutaathiri wengi zikiwemo familia za wafanyakazi,”
alimkariri Waziri Nnauye.
Mwanamama huyo alikwenda mbali kwa kushauri Zanzibar
katika kutanua wigo na kuongeza uhuru wa habari na kujieleza, ifike pahala
ikopie utamaduni wa Uingereza, wa kuruhusu watu kutumia eneo la Hyde Park kutoa
madukuduku yao bila kuguswa ili mradi tu hawafanyi hivyo nje ya sehemu
hiyo.
Alisema ingawa watu wanaweza kutumia fursa hiyo
kusema maneno makali, lakini hakutakosekana ushauri wenye tija ambao kamati
itakayoundwa kufuatilia uhuru huo wa kujieleza, watayaorodhesha na kuyafikisha
serikalini kwa kufanyiwa kazi.
Jumuiya za vyama vya watu wenye ulemavu ni miongoni
mwa wadau wa habari, na mwandishi wa makala haya alizungumza na Mratibu Jumuiya
ya Watu Wasioona Zanzibar (ZANAB) kupata
maoni yake.
Alikiri kuwa huu ni wakati muafaka Zanzibar ipate
sheria mpya ya habari ili kukidhi matakwa ya uhuru wa kujieleza na kuwa na
serikali inayoendeshwa kwa misingi ya uwazi na ukweli.
Alifahamisha kwamba, uzoefu unaonesha mara nyingi
baadhi ya viongozi wanaviogopa vyombo vya habari labda kwa kuwa miongoni mwao
hawako safi kwa asilimia 100.
Alikumbushia kuwa Zanzibar ilikuwa na sheria Namba 5
ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu ya mwaka 1988 ambayo
ilionekana na mapungufu yaliyokuwa yakikwamisha haki ya uhuru wa vyombo vya habari na uandishi wa
habari visiwani humu.
Alisema hata baada ya marekebisho hayo imeonekana
kuwa bado sheria iliyopo sasa haitekelezeki vizuri.
Alitaja sababu za kutokutekelezeka huko, kuwa ni
kutokana na ukweli baadhi ya viongozi hawako tayari kuwapa waandishi taarifa
wazitakazo kikamilifu japokuwa zina maslahi kwa umma.
“Mbali na kunyimwa habari, vikwazo haviishii hapo,
kwani mara kwa mara kumeripotiwa kesi za baadhi ya wanahabari kutishwa, vifaa
vyao kuzuiliwa na kupekuliwa, na hata kuwekwa kizuizini kwa madai yanayopambwa
rangi za kufanya uchochezi na kuvuruga amani ya nchi,” alifafanua.
Adil alisema kwamba waandishi wa habari ni wadau wa
maendeleo, na pia ni jicho linaloona mbali, hivyo kupitia harakati zao wana
uwezo mkubwa wa kuibua changamoto mbalimbali pamoja na kupaza sauti za
wasiosikika ili kuleta mabadiliko chanya.
Alibainisha kuwa umefika wakati sasa viongozi na
watendaji wa sekta za serikali na binafsi wawaone waandishi kuwa ni marafiki
badala ya kuwaweka kwenye kundi la maadui.
“Kwa maoni yangu, mtendaji au kiongozi hana haki ya
kukidhibiti chombo cha habari au kumuwekea vikwazo mwandishi asitoe taarifa.
Dawa hapa ni watendaji wasiotaka kuripotiwa maovu yao ikiwemo wizi wa mali ya
umma na rushwa, ni kubadilika na kufuata sheria,maadili na miongozo ya kazi,”
alisisitiza.
Alitaka sheria ijayo, iepuke kuwapa viongozi mamlaka
makubwa zaidi kuvidhibiti vyombovya habari ikiwemo haki ya kuvifuta.
Aidha alitaka baadhi ya maneno yasitumike kwenye
sheria hiyo, ikiwemo neno KUDHIBITI ambalo linajitokeza sehemu nyingi katika
sheria ya sasa.
Alisema maneno kama hayo pamoja na uwezo uliochupa
mipaka kwa wenye mamlaka, yanaweza kutumika vibaya endapo kiongozi atakuwa na
chuki binafsi kwa mwandishi au chombo anachokitumikia, au kutegemea anavyoamka.
Alieleza matarajio yake kwamba, sheria mpya
inayosubiriwa kwa hamu itakuja kufuta mapungufu yaliyopo na kuweka msingi wa
kutumika miaka mingi bila malalamiko na hivyo kuchukua muda mrefu kabla kuibuka
haja ya kuipitia na kuirekebisha tena.
Jamila Mahmoud Juma ni Mkurugenzi wa Chama cha
Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), alisema kutokana na maendeleo ya
teknolojia yaliyopo sasa, dunia imekuwa wazi na ndogo kufikika, hivyo sheria
ijayo ya habari pia izingatie haki ya mtu kupata taarifa kupitia mitandao ya
kijamii.
Alisema ingawa kila mtu anapaswa kufuata sheria, mabadiliko ya teknolojia yasiachwe
kuhalalisha watu kuchafuana, ingawa ni busara mitandao ipewe heshima yake kwa
kuwekewa taratibu zinazolinda hadhi ya mtoa na mpokea habari.
“Kudhibiti mitandao na kasi ya upatikanaji taarifa
duniani ni jambo gumu kwa sasa, hata hivyo, mamlaka zinapaswa kuweka sheria
madhubuti ambazo hazitapendelea upande wowote, bali zitamzindua mtumiaji kifaa
cha kielektoniki awe makini kuepuka kumdhuru mtu mwengine,” alisema.
Hata hivyo, alishauri viongozi wajifunze na kuukubali utamaduni wa
kukosolewa hasa inapokuwa mkosoaji/mwandishi amelenga kutetea na kulinda
maslahi mapana ya taifa.
Alieleza kuwa kukifungia chombo cha haabari au
mwandishi hauwezi kuwa ufumbuzi wa tatizo, lakini serikali inapohisi imekosewa
au mtu anapoona amekashifiwa,atumiemabaraza ya usuluhishi au hata vyombo vya
sheria kutafuta haki.
“Kutokana na utandawazi uliotawala dunia,
tukiendekeza mchezo wa kufungiafungia vyombo na waandishi, itafika siku
tutaamka asubuhi hakuna hata gazeti moja au vituo vyote vya redio na
televisheni vimefungwa. Tusifike huko na sheria ijayo isiweke ugumu kama huo,”
alihitimisha.
Baadhi ya wadau waliotoa maoni yao, walishauri Zanzibar itakapofanyia
marekebisho Katiba yake iige mfano wa nchi jirani ya Kenya na nyengine kwa
kuingiza matakwa ya mkataba wa Afrika Mashariki kuhusu haki za binadamu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) Dkt. Suleiman Seif Omar, alisema
Kenya ilifanya jambo jema kwani katika marekebisho ya Katiba yake yaliyofanywa
mwaka 2010, uhuru wa kujieleza na kupata habari umepewa umuhimu na uzito unaostahili katika Ibara za 33, 34 na 35.
“Kwa mfano Ibara ya 33 (2) imesisitiza kuwepo uhuru wa kuendesha vyombo
vya habari vya kielektroniki, vya uchapishaji na aina nyengine zote za vyombo
vya habari,” alitoa mfano.
Kilichomkuna zaidi, ni Ibara hiyo inaposema, “Serikali haitapaswa; (state
shall not);
-Kudhibiti au kuingilia mtu yeyote anayejishughulisha na utangazaji,
utoaji au usambazaji wa uchapishaji wowote au usambazaji wa habari kwa chombo
chochote”. Aidha;
Kuadhibu mtu yeyote kwa maoni au mtazamo wowote au maudhui ya matangazo
yoyote, uchapishaji au usambazaji.
Eneo jengine alilovutiwa nalo ni ;
33(3) Utangazaji na vyombo vyengine vya habari vya kielektroniki vina
uhuru wa kuanzishwa, kwa kuzingatia tu taratibu za leseni ambazo;
(a) Nii muhimu kudhibiti mawimbi ya hewa na aina nyenginezo za usambazaji
wa mawimbi; na
(b) Havipaswi kudhibitiwa na serikali, maslahi ya kisiasa au maslahi ya
kibiashara.
33(4) Vyombo vyote vya habari vinavyomilikiwa na Serikali vitakuwa;
(a) Huru kuamua kwa uhuru maudhui ya uhariri wa matangazo yao au
mawasiliano mengine;
(b) Kutokuwa na upendeleo; na
(c) Kutoa fursa ya haki kwa uwasilishaji wa maoni tofauti na maoni
yanayopingana.
Hata hivyo, Dkt. Seif ambaye ni Meneja wa zamani wa Baraza la Habari
Tanzania (Zanzibar), alitoa tahadhari kwamba pamoja na kutaka sheria mpya ya
habari isiyokuwa ngumu, alikumbusha wajibu wa wanahabari kuzingatia taarifa
zinazojenga zaidi badala ya zile zinazochochea vurugu na mifarakano.
“Ni haki yetu kudai sheria yenye mazingira rafiki kwa kazi zetu,lakinini
wajibu wetu pia kukumbuka usalama wanchi yetu na kujitahidi kalamu na kamera zetu
zisiwe chanzo cha mifarakano na kusambaratisha taifa kwani likizama tutaangamia
sote,” aliweka kituo.
Comments
Post a Comment