IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA
MKUU wa Wilaya ya Wete Pemba Dk. Hamad Omar Bakar amewapongeza wananchi wa Shehia ya Mlindo kwa uthubutu wao wa kujitolea katika kupambana na vitendo viovu ikiwemo udhalilishaji, wizi wa mazao na mifugo.
Akikabidhi vitambulisho kwa vijana wa ulinzi shirikishi (Polisi Jamii) kwenye mkutano uliofanyika katika shehia hiyo, Mkuu huyo aliwataka wanakikundi cha Polisi Jamii kuvitumia vitambulisho hivyo kama ilivyokusudiwa kwa lengo ni kudhibiti vitendo viovu.
Alisema kuwa, wananchi hao wamefanya jambo zuri la kujitolea kwa kuanzisha kikundi cha kupambana na vitendo viovu, hivyo ni vyema wakaendelea kushirikiana kuhakikisha wanavidhibiti na shehia I abaki katika hali salama.
"Kuna vitendo vya udhalilishaji na wizi ambavyo vinawaliza wanajamii kila kona, lakini naamini kwa kikundi hiki mlichokiunda basi mtafanikiwa kiyadhibiti, nawapongeza sana," alisema Mkuu huyo.
Aidha aliwataka wanajamii kuacha tabia ya kusuluhisha kesi za udhalilishaji majumbani na badala yake wafike kwenye vyombo vya Sheria ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa watendaji wa makosa hayo.
"Muhali ni kikwazo cha maendeleo na husababisha vitendo hivyo kuongezeka, hivyo tujitahidi kuripoti na kutoa ushahidi ili wahalifu wasiwe na nguvu ya kutenda makosa," alifahamisha.
Kwa upande wake Mkaguzi wa shehia hiyo Inspekta wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Khalfan Ali Ussi alisema, kupatiwa vitambulisho kwa Polisi Jamii itarahisisha kuwafikia na kuwaibua wahalifu kwa wepesi zaidi, jambo ambalo awali ilikuwa ni changamoto.
Aliwataka wanakikundi hao kuzingatia Sheria za nchi, kanuni na maadili katika utendaji wa kazi zao kwani wameshajengewa uwezo juu ya kujua majukumu, wajibu na mipaka yao juu ya kutekeleza kile wanachotakiwa kukifanya.
"Ulinzi muanze nyinyi wenyewe kwanza na baadae mulinde jamii, hii itawasaidia kufanya kazi zenu vizuri huku jamii ikiwamini, pia naiomba jamii iwape mashirikiano vijana hawa ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na bila ya vikwazo," alisema Mkaguzi huyo.
Katika risala iliyosomwa na Ali Kombo Hamad kwa niaba ya wenzake alisema, uwamuzi wa kuanzisha kikundi cha ulinzi shirikishi ni kuhakikisha jamii inaishi katika mazingira salama.
MWISHO.
Comments
Post a Comment